Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Tundu Lissu kizimbani, akosa dhamana

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WABUNGE wawili wa Chadema Tundu Lissu na Esther Matiko na baadhi ya wafuasi na viongozi wa chama hicho, akiwamo Mwita Waitara, wamewekwa rumande baada ya kukosa dhamana katika kesi ya uchochezi inayowakabili.


Awali kabla ya kufikishwa katika Mahakama ya Wilaya Tarime jana, viongozi hao na waandishi wa habari wanne, walitiwa mbaroni na Polisi kwa tuhuma za uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani wilayani hapa.


Baada ya hapo, Lissu, Matiko na Waitara walifikishwa mahakamani na kushitakiwa kwa uchochezi na kusababisha uvunjifu wa amani.


Mbele ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Tarime, Yusto Ruboroga, Mwendesha Mashitaka Husein Kiria, alidai kuwa, washitakiwa hao walishiriki katika uchochezi na kutishia uvunjifu wa amani.


Akitaja masharti ya dhamana, Hakimu Ruboroga aliwataka washitakiwa kuwasilisha hati za mali zisizohamishika na barua ya watendaji wa vijiji na kata.


Hata hivyo, washitakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande hadi leo, uamuzi wa kupewa dhamana utakapofikiwa.


Nao ni Mabere Makubi wa Televisheni ya Channel Ten, Anna Mroso (Nipashe); Berdina Nyakeke (The Citizen) na Anthony Mayunga (Mwananchi) anayefanyia kazi Mugumu, Serengeti.


Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Tarime- Rorya, Constantine Massawe alitangaza awali kukamatwa kwa watu hao jana alipozungumza na waandishi wa habari.


Alisema, Mbunge huyo na wenzake, walikamatwa kwa uchochezi kwa kushawishi wafiwa kususia miili ya ndugu zao wane kati ya watano waliouawa katika mapambano ya polisi na zaidi ya watu 800 waliovamia Mgodi wa North Mara, Mei 16, ambapo polisi saba walijeruhiwa.


Alisema, baada ya baadhi ya wafiwa kuchukua miili hiyo juzi ikiwa ni ya Chacha Ngoka wa kijiji cha Kewanja; Mwikwabe Marwa na Chawali Bhoke wa Mugumu na Emmanuel Magige mkazi wa Nyakunguru na kuisafirisha kwao, wafuasi hao wa Chadema waliwafuata hadi Nyakunguru.


Alisema walipofika, waliishawishi familia ya Magige kuuchukua mwili huo na kuupeleka Polisi kwa nia ya wanahabari hao waliofuatana nao kuupiga picha ili kuonesha taswira kuwa Polisi imetelekeza miili hiyo na kupotosha jamii na kujenga chuki kwa Jeshi hilo na wananchi wa Tarime. Watuhumiwa hao waliokamatwa Nyakunguru wakiwa na Lissu ni Mwita Waitara na Diwani Charles Ndesi.


Wanahabari hao kutoka Musoma na mwingine kutoka Serengeti, wamekuwa wakituhumiwa wilayani Tarime kwa kushirikiana na wafuasi wa Chadema kushawishi wananchi kususia miili ya ndugu zao na kuchochea vurugu.


Mwishoni mwa wiki, Makubi alishitakiwa na mwandishi wa habari hii kwa kutaka kumshambulia na kumtishia maisha katika mji mdogo wa Sirari, wakati kundi la wana Chadema likishawishi vijana wa Sirari kwenda Tarime na Nyamongo kushiriki maandamano na vurugu.

0 comments

Post a Comment