FAMILIA za ndugu waliopigwa risasi na kufa katika mgodi wa African Barrick North Mara, zimeigomea Serikali kuzika miili ya marehemu wakitaka ufanyike kwanza uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo. Mbali na kugomea mazishi, familia hizo pia zimekataa kupokea rambirambi za polisi katika msiba huo, zikidai kuwa rambirambi hizo hazina umuhimu kuliko maisha ya ndugu zao.
Hatua hiyo ilimchanganya Kamishina wa Oparesheni na Mafunzo wa Polisi, Paul Chagonja ambaye aliwakilisha Jeshi hilo kuwasihi wananchi hao bila mafanikio. Mbele ya wananchi hao waliofurika eneo la hospitali, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema anaunga mkono msimamo wa kukataliwa kwa rambirambi hizo za Serikali, akieleza kuwa hajawahi kusikia Jeshi la Polisi linaua na kuzika kisha kutoa ubani.
“Hapa tunatafuta haki wala si siasa kama wanavyopotosha, lini polisi wakaua majambazi kisha wakazika na kutoa rambirambi? Kuna kitu kimefichika hapa, hivyo mimi nasema kama ni rambirambi sisi tutatoa, lakini pia ninyi wananchi hamuwezi kuchangia hata Sh1,000?,” Alihoji na kujibiwa "tunawezaaa."
Alisema kuwa baada ya kujadiliana na kupata utaalamu wa kisheria kutoka ngazi za juu, Chadema kimekubaliana na familia na viongozi kuwa maiti hazitachukuliwa mpaka kesho, siku ambayo Waziri Kivuli wa Sheria na Mambo ya Katiba,Tundu Lissu, wakili Mabere Marando na mjumbe wa tume ya haki za binadamu watakapofika.
“Takwimu zinaonyesha kuwa watu 23 wameuawa na polisi eneo hilo, presha ya kuzika ya nini wakati hawatafufuka? alihoji na kuendelea:"Tunataka liwe fundisho, tumezitaarifu balozi za Canada na Norway na wanaweza kuja huku, huduma hizi tutadili nazo sisi, huwezi kuogopa gharama katika kudai haki,”alibainisha.Chagonja, RPC wapingana Wakati Lema akieleza hayo, Kamishna Chagonja amekanusha taarifa zilizotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu Mkoa wa Kipolisi wa Tarime, Constantine Massawe kuwa waliouawa walikuwa majambazi.
“Jamani hawakuwa majambazi mimi ndiye mkubwa nimekuja, kauli yangu ifanyiwe kazi si hizo zilizokwishatolewa. Walivamia mgodi tu, ndiyo maana tunataka kutoa rambirambi na kuwataka wazikwe," alisema.
Alisema lengo la kufika kwake ni kueleza msimamo wa Serikali kuwa tume itaundwa kuchunguza mauaji hayo na wahusika watakaobainika watachukuliwa hatua bila kuangalia nyadhifa zao.
“Tunaomba ndugu wakubali kuchukua miili ya marehemu, wakubali kuzika maana kukaa na maiti bila kuzika haisaidii, mimi nimetumwa kwa kazi hiyo, wengine wanawapotosha,”alidai. Hata hivyo, Kamishna Chagonja hakueleza tume hiyo itaundwa lini na itahusisha watu gani, akieleza kuwa hatua hiyo inafanywa na ngazi ya juu zaidi.
Wakati Kamishna Chagonja akisema hayo, Kamanda Massawe alilazimika kuikana kauli yake akisema "jamani sijasema majambazi, bali wavamizi,”
Diwani aingiwa hofu
Diwani wa Kata ya Matongo, Bathlomeo Machage alisema kuna vitisho vinavyoendelea kwa baadhi ya watu kwa madai kuwa wanagomea uchukuaji wa maiti hizo na kuwa watabambikiwa kesi za mauaji.“Mimi naambiwa nilimpiga mbunge kama mimi nazuliwa je wananchi wa kawaida inakuwaje? Alihoji na kuendelea: "Haya mambo yanatakiwa uongozi wa serikali wawepo hapa kama DC na mbunge, ambao hawapo inakuwaje polisi ndio washinikize suala hilo?”
Wakati huohuo baadhi ya askari polisi mjini hapa wameonyesha kufurahia kitendo cha wananchi kuushambulia kwa mawe msafara wa Mbunge wa Tarime Nyambale Nyangwine na mwenyekiti wa halmashauri wakisema: "Afadhali wameonja joto la jiwe"
Polisi hao wamechekelea kuvunjika kwa ziara hiyo baada ya kusikia kuwa tayari mbunge huyo amemwandikia barua Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime na Rorya kutaka polisi itaje majina ya askari wake waliowaua watu hao ili sheria ichukue mkondo wake.
Baadhi ya askari ambao hawakutaka kutajwa majina yao waliliambia gazeti hili kuwa kitendo cha mbunge na msafara wake kupigwa mawe, kinaonyesha wazi kuwa hata askari waliohusika na mauaji walikuwa wakijihami.
Walidai kuwa hali ilivyo kwa sasa eneo hilo kumechafuka na kama hatua za makusudi za Serikali hazitachukuliwa haraka, mauaji yataendelea kwa kuwa askari hawatakubali kufa kibudu wakiwa na silaha.
DC azungumza
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, John Henjewelle aliliambia gazeti hili kuwa Serikali imeshachukua hatua za makusudi za kuitaka kampuni ya African Barrick North Mara kuwalipa fidia stahiki wahusika waweze kupisha haraka iwezekanavyo.
“Tayari hilo linashughulikiwa tena na wataalamu wa Serikali wanahusishwa kusimamia kuhakikisha sheria ya fidia inatumika, watu walipwe stahili zao wapishe, maana inakuwa ngumu kiusalama kufanya kazi za uchimbaji na wananchi wako ndani ya eneo ,”alisema.
Alikwenda mbali zaidi na kudai kuwa mchakato huo unakwamishwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa na vijiji kwa kuwashawishi wananchi wasikubali kuhama maeneo hayo.
Mwenyekiti wa Kijiji
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kewanja, Kata ya Kemambo, Tanzania O’mtima aliliambia Mwananchi kuwa mauaji yanayofanywa si suluhisho bali yanazidisha chuki kubwa.“Nakupa takwimu za kutoka mwaka 2009 nilipoingia madarakani, vijana watano kutoka kijijini kwangu wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi, acha waliojeruhiwa na kuwa walemavu, ni wengi sana,”alidai.
Madai ya wizi wa maiti
Kaka wa mmoja wa watu waliouawa kwa kupigwa risasi na askari polisi, Marwa Mwita Mwasi, ameibuka na kudai kuwa maiti ya mdogo wake imeibwa na kutoroshwa usiku wa manane.Alisema mdogo wake Chacha Mwasi aliuawa Mei 16 mwaka huu baada ya kupigwa risasi na askari polisi. Mwili wake ulihifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.
Marwa alidai kuwa Mei 17 mwaka huu baada ya kukosa mwafaka kati ya Serikali na wao, alitoka na kwenda kwa jamaa yake kwa ajili ya kusubiri utaratibu Mei 18 kama watazika ama la."Nikiwa kwa ndugu yangu, mke wangu saa 5 za usiku Thereza Bhoke, alinipigia simu akitaka kujua niko wapi, nikamwambia niko Tarime, akadai mbona maiti imeletwa na wewe haupo inakuaje?” Alisema.
Alisema aliambiwa kuwa maiti imefikishwa katika Kijiji cha Bisarwa Bhukenye na magari ya Serikali, lakini yeye aliwaambia kuwa hakushirikishwa kuchukuliwa kwa mwili huo na kuwa waliuiba kwa nia ya kutaka kudhoofisha msimamo wao.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Pracidia Rweyemamu alikiri maiti hiyo kuchukuliwa na kuwa walijitokeza ndugu wakiwamo katibu tarafa.“Ni kweli niliombwa na ndugu wa familia nami natokea huko nikaomba halmashauri wakatoa gari. DC akatoa laki moja za jeneza na wakati wa kuchukua, kamati ya ulinzi na usalama ilikuwapo, mimi nilisaidia tu na nimekuwa nikitoa msaada mara kwa mara,”alieleza katibu tarafa aliyejulikana kwa jina moja la Machango.
Nao Fidelis Butahe na Patricia Kimelemeta wanaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja amewataka wananchi wanaoishi karibu na migodi kufuata sheria na taratibu ili kuondoa tofauti zinazojitokeza baina yao na wawekezaji.
Waziri Ngeleja alisema hayo jana kwenye uzinduzi wa bodi mpya ya Wakala wa Ukaguzi wa Migodi (TMAA),uliofanyika jijini Dar es Salaam.“Kuna migogoro inayotokea kwenye baadhi ya migodi. Hii inatokana na baadhi ya wanasiasa kuchochea vurugu ambazo zinaweza kuhatarisha amani kwenye maeneo yao. Wajibu wa watu hao ni kushirikiana pamoja ili kuondoa tofauti yao,”alisema Ngeleja.
Aliongeza kuwa Serikali kupitia kampuni ya mgodi wa Barrick wameandaa mradi wa kuwasaidia wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kimitaji ili waweze kupata vifaa vya kisasa vya kuchimbia madini.
0 comments