Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Maandamano makubwa yatekelezwa Mbeya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

CHADEMA jana ilitekeleza maandamano makubwa jijini Mbeya yaliyowashirikisha mamia ya wakazi wake, wakiwamo wafuasi wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Maandamano hayo yaliyoongozwa na viongozi wa ngazi ya juu kitaifa wa Chadema, yalianzia katika eneo la Mafiati na kuishia kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi ya Luanda- Nzovwe.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,  Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi walikuwa mstari wa mbele kuongoza maandamo hayo, huku wakishangiliwa na wananchi wa Jiji hilo.
Pia alikuwepo Mbunge wa Mbozi Magharibi, Silinde David na Wabunge wa Viti Maalum, Susan Kiwanga, Joyce Mukya na Grace Kiwelu.Pikipiki, baiskeli na magari yaliyokuwa yamepambwa bendera za Chadema yalitanda katikati ya Jiji la Mbeya kuanzia mchana, huku baadhi ya wapenzi wa chama hicho wakipiga kelele za kumkashifu, Sambwee Shitambala kwa kukihama chama hicho na kukimbilia CCM.
Kabla ya kuhamia CCM, Shitambala alikuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoani Mbeya.
Maandamano hayo ya Chadema yalilenga kuishinikiza Serikali iachane na mambo kadhaa, ikiwamo muswada wa kubadilisha Sheria ya Ununuzi wa Umma ili kuruhusu ununuzi wa vitu chakavu, mchakato wa katiba uondolewe mikononi mwa CCM, kuunganisha nguvu ya umma ili kupinga bidhaa kupanda bei na kutaka uchaguzi wa Meya wa Arusha ufanyike upya.

Wakati maandamano hayo yakiwasili katika Viwanja vya Shule ya Msingi ya Luanda-Nzovwe tayari umati mkubwa wa watu ulikuwa umeshafurika kuwasubiri viongozi wa kitaifa wa chama hicho.Polisi walionekana maeneo mbalimbali yalikopita maandamano hayo wakiendelea kulinda usalama wa watu na mali zao.
Wafuasi wa Chadema walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali, huku wengine wakisema kama Dk Slaa si Rais wa Tanzania basi ni Rais wa Mbeya.Wengine walikuwa wamebeba mabango yanayokebei hatua ya CCM ya kujivua gamba na mengine yakilalamikia maoni ya Katiba mpya yanavyoendeshwa.
Wakati akifungua tawi la chama hicho katika chuo cha Teofilo Kisanji (TEKU), kabla ya maandamano hayo kuanza, Dk Slaa alimtaka Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kuacha kuvitisha vyama kwa barua kuwa visifungue matawi vyuoni."Tendwa ajue kuwa wanafunzi nao ni wananchi na ajue kuwa sisi kama Chadema tunafuata taratibu, hivyo asitutishe," alisema Dk Slaa.
Mbowe kupinga kodi
Akizungumza katika mkutano wa hadhara, Mbowe alisema chama hicho kitapinga ongezeko la kodi yoyote bungeni katika bajeti ijayo mpaka kieleweke na kwamba Serikali isipofanya hivyo watapigana bungeni kwa maslahi ya wananchi.

Mbowe alisema ongezeko la kodi linawaumiza wananchi na Serikali imekaa kimya wakati hali ya maisha inaendela kuwa mbaya. Mbowe alisema kuwa mapambano hayo watayafanya bungeni, ikishindikana watayahamishia kwa wananchi ili Serikali ielewe kuwa hali ya maisha kwa wananchi wa chini si nzuri."Wabunge wa Chadema tutaendelea kukomaa mpaka kieleweke kwa kuwa hatuvunji amani, bali tunawahangaikia wananchi ili wawe na maisha bora," alisema Mbowe.
Mbowe alisema kuwa Taifa lina msiba mkubwa wa umaskini na Chadema itapambana bungeni na nje ya Bunge mpaka kieleweke.Alisema kuwa Serikali imezoea kupanda kodi ambayo husababisha kupandisha gharama ya maisha kwa wananchi kwa kuwa serikalini hawana shida.

"Kama Serikali inataka kuona uwezo wetu wa kuhamasisha Watanzania wapandishe kodi katika bajeti ya mwaka huu," alisema Mbowe.Alisema wamekuwa wakifanyiwa hila kuwazuia kutumia haki yao ya kidemokrasia bungeni kwa madai kwamba wabunge wa Chadema wanavunja kanuni, lakini haielezwi ni kanuni gani zimevunjwa.


Dk Slaa na bei ya bidhaa
Naye Dk Slaa alisema lazima Serikali ishushe bei ya sukari na mafuta kwa kuwa kutofanya hivyo ni kama Serikali haipo."Haiwezekani wanavuana magamba halafu wananchi wanaendelea kuteseka. Magamba ni yao, hivyo wananchi waangaliwe," alisema Dk Slaa.
Alisema kuwa wataendelea kuandamana kwa vile ni haki iliyopo kikatiba, hivyo Jeshi la Polisi haliwezi kuzuia au kutishia kuzuia maandamano yao.

"Tunawahamasisha Watanzania kuangalia hali ya maisha yao kwa sababu ni haki yetu ya msingi, na tunataka wananchi waionyeshe Serikali yao mambo yanayowasumbua," alisema Dk Slaa.
Akihutubia mkutano huo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, alimtaka Dk Slaa asimjibu Ridhiwani Kikwete katika hizo siku alizotoa, bali ampe Rais Kikwete siku saba za kuhakikisha kuwa mafisadi wote wanatokomea.
Alisema mapambano yake yataendelea bungeni kwa kuwa suala lake na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, bado halijaisha, hivyo Bunge lijalo litawaka moto. "Pinda alinibeep bungeni nikampigia, Makinda akapokea. Lakini mvutano wangu na Pinda haujaisha, nikiingia bungeni mtanisikia," alisema Lema.

0 comments

Post a Comment