Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KISIASA , HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Korti yaamuru Dk Slaa, Mbowe wakamatwe

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


Ni kwa kushindwa kuhudhuria kesi ya maandamano Arusha
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha imetoa hati ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani hapo kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.Pamoja na viongozi hao wa kitaifa, mahakama hiyo pia imeamuru wabunge wawili wa chama hicho, Phillemon Ndesamburo (Moshi Mjini) na Godbless Lema (Arusha Mjini) nao wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo baada ya kushindwa kuhudhuria mara kadhaa katika kesi inayowakabili ya kufanya kusanyiko lisilo halali Januari 5 mwaka huu.


Hakimu Mkazi, Charles Magesa alitoa hati hiyo jana baada ya washtakiwa hao na wenzao watano pamoja na wadhamini wao, kutofika tena mahakamani bila taarifa yoyote ili kuendelea na kesi hiyo. Washtakiwa wengine ambao mahakama imetaka wakamatwe na kufikishwa mahakamani hapo Juni 24 mwaka huu ni; mchumba wa Dk Slaa, Josephine Mushumbusi, Richard Mtui, Aquiline Chuwa na mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.


Pamoja na washtakiwa hao kutofika mahakamani, hata mawakili wao, Method Kimomogolo na Albert Msando pia hawakuwepo mahakamani wakati hati hiyo inatolewa. Washtakiwa Joseph Selasini (Mbunge wa Rombo) na Dadi Igogo pia hawakuwepo mahakamani jana, lakini mahakama haikuamuru wakamatwe kama ilivyo kwa wenzao kutokana na wadhamini wao kujitokeza na kuwaombea udhuru.


Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa mahakamani hapo, Selasini anahudhuria vikao vya Kamati ya Bunge mjini Bagamoyo na Igogo yuko kwenye mitihani jijini Dar es Salaam.Washtakiwa waliohudhuria mahakamani jana ni Nai Steven, Mathias Valerian, John Materu, Daniel Titus, Juma Samuel, Walter Mushi, Peter Marua na Erick Makona.


Hakimu Magesa alisema washtakiwa walioshindwa kufika mahakamani jana ambao baadhi yao ni wabunge, wangeweza kuwakilishwa na mawakili wao ambao wangetoa udhuru kama wangekuwa na nia ya dhati ya kuhudhuria kesi inayowakabili.


Kabla ya kutoa hati hiyo, hakimu Magesa aliwaita washtakiwa hao mmoja baada ya mwingine kwa majina na kugundua kuwa kati ya washtakiwa 19, wanane hawakuwepo mahakamani.Baadaye akahoji endapo kulikuwa na mdhamini yeyote ndani ya ukumbi wa mahakama mwenye taarifa za washtakiwa wasiokuwepo na kugundua kuwa hakuwapo pia.


Wakili wa serikali, Edwin Kakolaki aliiomba mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali ambapo hakimu Magesa aliahirisha shauri hilo hadi Juni 24, mwaka huu.


Hata hivyo, uchunguzi wa Mwananchi jana ulibaini kuwa wakati hakimu huyo akitoa kibali cha kukamatwa kwa viongozi hao jana, wabunge wote wanaokabiliwa na kesi hiyo, wanaelezwa kuwa wapo jijini Dar es Salaam ambako wanahudhuria vikao mbalimbali vya kamati za Bunge.


Kauli ya Ndesamburo
Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo ambaye ametakiwa kukamatwa aliliambia gazeti hili jana, "Ninachojua ni kwamba mara ya mwisho kesi hiyo ilipotajwa mwezi uliopita, washtakiwa wote tulimwomba hakimu kupitia kwa mawakili wetu tusiwepo mahakamani leo (jana) kwa sababu mbalimbali.”
Ndesamburo alitaja moja ya sababu hizo kuwa ni wabunge walioshtakiwa katika kuhitajika kwenye vikao vya kamati za bunge.


"Bwana mwandishi siyo kwamba tumefanya ujeuri. Tuliomba hakimu kupitia kwa wakili wetu kuwa leo maadamu kesi inakuja kwa ajili ya kutajwa, tukaomba tusiwepo mahakamani na alikubali," alieleza Ndesamburo.
"Kama isingekuwa ni ruhusa, tusingekuwa hapa. Tungeweza kwenda Arusha... Taarifa unayoniambia imenishangaza sana."


Ndesamburo alisema washtakiwa wote wana taarifa kwamba wasingekuwa mahakamani jana kwa kuwa tayari wana ruhusa.Kuhusu hatua ambazo watachukua kutokana na amri hiyo ya mahakama, alisema asingeweza kusema lolote jana, ila watawasiliana na mwanasheria wao ili kujua namna watakavyokabiliana na hali hiyo.


Viongozi na wanachama hao wa Chadema walikamatwa na kufikishwa mahakamani baada ya vurugu zilizotokea Januari 5, mwaka huu kutokana chama hicho kufanya maandamano ya kuwahamasisha wananchi wa Arusha na mikoa jirani kushiriki kutoa maoni yao juu ya kuandikwa upya katiba ya nchi na kupinga matokeo ya uchaguzi wa meya wa Arusha.


Katika matukio hayo, watu watatu waliuawa na polisi kufutia mapambano baina ya polisi na wananchi. Polisi walitumia risasi za moto na mabomu ya machozi kudhibiti maandamano hayo ambayo Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema alitangaza kuyapiga marufuku saa chache kabla ya kuanza.


IGP Mwema aliyapiga marufuku maandamano hayo akibainisha kwamba taarifa za kiintelijensia zilikuwa zimebaini kwamba kungekuwa na vurugu wakati wa kufanyika kwake.


"... Kuna taarifa za kiintelijensia kwamba kunaweza kutokea fujo na uvunjifu wa amani,” alisema IGP Mwema katika mkutano wake na waandishi wa habari.


Dk Slaa, Mbowe na wabunge hao watatu wa Chadema walikamatwa na kufikishwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Januari 7 mwaka huu chini ya ulinzi mkali na kusomewa mashtaka yanayowakabili.


Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Zakaria Elisante alidai mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Charles Magesa kuwa watuhumiwa hao, walikuwa wametenda kosa la kufanya mkusanyiko kinyume cha sheria.


Elisante alidai kwa kufanya kosa hilo, watuhumiwa hao, wamevunja Sheria Namba 74, 75 kifungu cha 16 kama ilivyofanyiwa marekebishoa mwaka 2002 na pia Sheria ya Polisi, sura 45 kifungu cha 322 ambayo pia ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002.


Hata hivyo, watuhumiwa wote walikana makosa hayo na mawakili wa serikali alieleza kutokuwa na pingamizi na dhamana zao.Mawakili wa utetezi, Method Kimomogolo na Albert Msando, walieleza mahakama kuwa watuhumiwa wote wana wadhamini ambao baadaye walidhaminiwa kwa thamani ya Sh 2 milioni kila mmoja.


Mchumba wa Dk Slaa, Josephine Mushumbusi na watuhumiwa wengine watatu walisomewa mashtaka yao wakiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha, Mount Meru walikokuwa wakiendelea na matibabu yao.

0 comments

Post a Comment