Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA KITAIFA , HABARI ZA LEO - Chadema wataka uchunguzi mauaji ya Tarime

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana kilihitimisha ziara yake katika mikoa ya nyanda za juu kusini kwa kufanya maandamano na mkutano mkubwa wa hadhara mjini Iringa.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Mlandege, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alitoa tamko la kuitaka serikali iunde tume huru ya majaji wa mahakama kuchunguza mauaji yaliyotokea Tarime kwenye mgodi wa North Mara unaomilikiwa na kampuni ya Barrick.
Mbowe alisema tayari chama hicho kimeshawatuma wanasheria wake, Tundu Lissu na Mabere Marando, kwenda Tarime kufuatilia suala na kuchukua hatua za kisheria za kupigania haki za wananchi wa eneo hilo ambao alisema mara kwa mara wamekuwa wakikandamizwa na wawekezaji wa mgodi huo.
Alisema uchunguzi uliofanywa na CHADEMA umebaini kuwa watu waliouawa ni tisa na si watano kama ilivyoelezwa na vyombo vya dola.
Pia alieleza kuwa tangu mwaka 2006 hadi sasa, takriban raia 20 wameshauawa kwa kupigwa risasi kutokana na mgogoro uliopo baina ya Barrick na wananchi wa eneo hilo.
“CHADEMA hatuungi mkono uhalifu lakini pia hatuko tayari kuona Watanzania wakiuliwa kwa risasi kama wanyama ndani ya nchi yao, kwa sababu tu serikali imeamua kuwa upande wa Barrick. Tutapigania haki zao hadi zipatikane,” alisema Mbowe na kushangiliwa.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, aliutumia mkutano huo kupinga kile alichokiita propaganda za CCM zinazolenga kumchonganisha na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Akipinga propaganda hizo alisema si kweli kuwa yeye ana ugomvi na Mbowe kama inavyoenezwa na vyombo vya habari vyenye uhusiano wa karibu na CCM.
Alisisitiza kuwa CHADEMA ni moja na imara na kamwe hatakuwa tayari kugombanishwa na mwenyekiti wa chama chake kwani ndiye aliyemjenga kisiasa na kiuongozi tangu akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu.
“Kataeni propaganda zenye lengo la kuigawa CHADEMA kwa kuwachonganisha viongozi. Zitto siwezi kumpinga Mbowe kama wanavyodai…Zitto nimekuwa Zitto kwa sababu ya Freeman Mbowe. Ndiye aliyenijenga tangu nikiwa chuoni. CHADEMA yetu ni moja na itaendelea kuwa imara…propaganda za kutugawa zimeshindwa, sasa tunachukua nchi,” alisema Zitto na kushangiliwa.
Wabunge, makada waandamizi waiwashia moto CCM
Katika mkutano huo, wabunge na makada waandamizi wa CHADEMA walitoa hotuba mbalimbali za kuelezea ubaya na udhaifu wa CCM na serikali yake.
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Utalii, alisema katika Bunge lijalo la bajeti ataitaka serikali ianze kutenga fedha kwa ajili ya kujenga chuo kikubwa cha utalii ili kuwaandaa vijana kuajiriwa kwenye mbuga na vivutio vya utalii vilivyo kwenye mikoa ya nyanda za juu kusini.
“Tuna mbuga kubwa za Ruaha, Katavi, Udzungwa na vivutio vingi vya utalii lakini vijana wa mikoa ya Mbeya, Iringa, Rukwa, Ruvuma na Njombe hawajaajiriwa vyakutosha katika sekta ya utalii kwa sababu ya kukosa chuo kilicho karibu nao. Ninakwenda kuwasha moto bungeni ili vijana wa mikoa hii nao wapate elimu na fursa ya karibu ya kujiajiri kwenye utalii,” alisema Msigwa na kushangiliwa.
Aliwataka wakazi wa mikoa ya nyanda za juu kusini na Watanzania kwa ujumla kuiunga mkono hoja hiyo, kwani kujengwa kwa chuo hicho kutachochea vijana kuajiriwa au kujiajiri katika sekta ya utalii kama ilivyo katika mikoa ya kaskazini ya Arusha na Kilimanjaro.
Naye Kada mwandamizi wa chama hicho, Thomas Nyimbo, alisema CCM imefilisika sera ndiyo maana inafanya siasa za udini na ukabila.
“Iringa ina raslimali za kutosha kuendesha uchumi wa nchi hii lakini kwa sababu ya ufisadi na sera mbovu za CCM, Iringa na Tanzania bado tuko nyuma. Ukiona mtu leo anatoa hoja ya udini na ukabila ujue amefilisika hoja na ni mjinga,” alisema Nyimbo.
Mbunge wa Viti Maalum kutoka Zanzibar, Mariam Salim Msabaha, katika hotuba yake iliyotawaliwa na vijembe dhidi ya CCM, aliwataka wakazi wa Iringa waendelee kukikataa chama hicho kwani kimeshindwa kwa makusudi kuwaletea maisha bora kama waliyonayo watoto wa vigogo, akiwemo Ridhiwan Kikwete.
“Waambieni CCM tunataka maisha bora kama ya Ridhiwan Kikwete. Na wasiwadanganye kuwa wamejivua gamba….nyoka akijivua gamba anateleza, humpati tena,” alisema na kushangiliwa.
Kwa upande wake mbunge wa viti maalum kutoka mkoa wa Iringa, Chiku Abwao, alikemea kile alichokiita fitna chafu za CCM zinazolenga kuwafanya wananchi wa jimbo la Iringa Mjini wamchukie mbunge wao, Mchungaji Peter Msigwa.
“Maandamano na mikutano yetu vinaitia homa CCM, sisi tunaendelea…mwendo mdundo, fitna zao za kutaka Msigwa ashindwe zimeshindwa na umati huu mkubwa ni ushahidi tosha,” alisema.
Wakati huo huo Mwandishi wetu Francis Godwin kutoka Iringa anaripoti kuwa
maandamano ya kufunga mikutano ya kitaifa katika mikoa ya nyanda za juu kusini ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana yalitikisa mji wa Iringa huku Chama cha Mapinduzi (CCM) kikikwama kuhujumu maandamano hayo.

Hujuma inayodaiwa kufanywa na CCM ni ile ya kujaribu kuwachanganya wananchi kwa kuwatoa madarasani wanafunzi shule ya sekondari ya wazazi Mwembetogwa ili kuushikilia kwa muda uwanja wa Mwembetogwa ulikokuwa ufanyike mkutano huo wa CHADEMA.
Hali kadhalika baadhi ya vijana wanaosadikika kuwa walipandikizwa na CCM kwa nia ya kuvuruga maandamano hayo walinusurika kipigo baada ya mmoja wao kuangusha kofia na skafu ya CCM iliyochanwa na kuchomwa moto majira ya saa 5 asubuhi kabla ya kuanza maandamano hayo eneo la Kihesa.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi umebaini kuwepo kwa njama za hali ya juu za CCM kutaka kuvuruga maandamano hayo mojawapo ya wazi ni ile ya kuuzuia uwanja wa Mwembetogwa ili CHADEMA isitumie katika mkutano wake wa jana na badala yake kuwatoa wanafunzi madarasani na kuutumia uwanja huo.
Mwandishi wa habari hizi alishuhudia walimu wawili wa shule hiyo wakiwa katika uwanja huo wa Mwembetogwa wakisimamia zoezi la wanafunzi hao kufanya tamasha ambalo linadaiwa kuanza kuandaliwa ndani ya wiki moja baada ya agizo la CCM mkoa kama njia ya kuhujumu maandamano hayo ya CHADEMA Taifa.
Hata hivyo katika tamasha hilo lililobatizwa kuwa ni tamasha la kusaka vipaji kwa wanafunzi baadhi ya wanafunzi walisema kuwa tamasha hilo limeandaliwa na CCM na sio uongozi wa shule hiyo kama inavyoelezwa na baadhi ya watu.
“Jana vionngozi wa CCM walifika shuleni kwetu na kushinda katika ofisi ya mkuu wa shule kwa ajili ya kuandaa tamasha hili …japo tunashindwa kujua lengo la CCM kuandaa tamasha hili kwani kama lingekuwa ni tamasha la shule tuna ukumbi mkubwa wa shule na siku zote tumekuwa tukifanyia katika ukumbi huo ila leo tumeshangazwa kuambia tuje hapa uwanjani ambako hatujawahi kufanyia tamasha kama hili la ghafla …wanasema ni bonanza la shule mbona katika ratiba za mabonanza yetu hakuna kitu kama hiki,” alisema mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo.
Mwalimu mmoja wa shule hiyo alimweleza mwandishi wa habari hizi kuwa suala hilo limezua mgawanyiko mkubwa katika shule hiyo baada ya mkuu wa shule kuingiza ratiba ambayo haikuwepo na ndio sababu ya walimu wote kutofika katika uwanja huo kuungana na mkuu wa shule ambaye ni kada wa CCM.
Jitihada za kumpata mkuu wa shule hiyo ili kuweza kuelezea malengo ya tamasha hilo hazikuweza kuzaa matunda.
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Iringa mjini Abed Kiponza alipotafutwa kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi ili kujibia madai ya wanafunzi hao kuwa viongozi hao wa CCM walifika shuleni hapo ili kupanga mbinu hiyo ya kuhujumu mkutano wa CHADEMA,alikanusha madai hayo na kuwa kwa sasa yeye yupo chuo kikuu huria cha Tanzania akijisomea kwa zaidi ya wiki sasa na hajapata kuacha darasa hata siku moja.
“Mimi ni Mwislamu na sijazoea kusema uongo; nasoma huku Open University hata sasa nikija hapo ulipo nitakuwa na vifaa vyangu vya shule.”
Mbunge wa jimbo la Iringa mjini Mchungaji Peter Msigwa na mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa Chiku Abwao walisema kuwa CCM ilipanga kuvuruga maandamano hayo ila imeshindwa na nguvu ya umma baada ya wananchi kukubali kutembea umbali wa zaidi ya kilometa zaidi ya 5 kutoka Kihesa hadi Mlandege ulikofanyika mkutano huo wa CHADEMA.

0 comments

Post a Comment