Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - Slaa, ameitaka TAKUKURU kuchunguza mapato ya Rostam Aziz

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchunguza mapato ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, kwa kile alichodai yana uhusiano mkubwa na ufisadi.
Dk. Slaa aliyasema hayo juzi jioni katika mkutano wake mjini Igunga, mkoani Tabora katika mwendelezo wa ziara zake.
Alisema mapato ya Rostam kwa mwaka yanafikia sh bilioni 280, hivyo TAKUKURU haina budi kumkamata na kumchunguza kwani aliwahi kutangaza kuwa hana shida ya kuwa kiongozi au kung’ang’ania madaraka yoyote, kwani pesa alizonazo zinamtosha.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, ikiwa TAKUKURU haitamchukulia hatua Rostam, atawashawishi wananchi kutotoa ushirikiano wowote kwa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na kuwazomea maofisa wake kila wanapowaona.
Akifafanua tuhuma hizo za ufisadi, alisema kuwa kati ya makampuni 17 yanayosemekana kuwa ni ya Rostam hakuna jina lake hata moja.
Alisema kama Rais Jakaya Kikwete angekuwa na nia ya kweli angemshirikisha kuwakamata mafisadi badala ya kuwapa siku 90 kuondoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, ikiwa Kikwete amewapa mafisadi hao siku hizo kuondoka ndani ya chama pamoja na kuachia ubunge, naye hana budi kujipa siku hizo, kwani naye ni fisadi.
Alisema kujitokeza kwa mmiliki wa Dowans Brigedia Jenerali (mstaafu), Sulaiman Mohammed Yahya Al Adawi, ulikuwa ni usanii wa picha ya Rostam kwani baadaye ndiye atakayelipwa fedha hizo za Dowans.
Alisema CHADEMA haitakubali fedha hizo zilipwe na kwamba itaitisha maandamano nchi nzima kupinga.
Dk. Slaa alisema ufisadi mwingine wa serikali katika sakata hilo la Dowans ni serikali kuweka mawakili watatu kinyemela na kupanga kuwalipa sh bilioni tano.
“Nilimtaja Rostam kuwa ni mmoja wa mafisadi kule Mwembeyanga, naye alinitumia vitisho kwa ujumbe mfupi kuwa nina sekunde chache za kuishi hivyo nipige magoti, nisali. Nilimjibu na nasema …nilizaliwa siku moja na nitakufa siku moja, sitaogopa kusema ukweli,” alisema Dk. Slaa.
Katika hatua nyingine, Dk. Slaa alisema moto uliowashwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA) umeifanya serikali ya CCM akiwamo Rais Jakaya Kikwete kushindwa kulala.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikungi katika Jimbo la Singida Mashariki jana aliposimama kuwasalimia wakati akitokea Singida kuelekea Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema Lissu ni mbunge jasiri katika Bunge ambaye amediriki kumnyooshea kidole hata Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema.
Katika hotuba yake hiyo alisema wananchi hawana imani tena na serikali ya Jakaya Kikwete na kama atafanya mchezo hataweza kurudisha imani hiyo wala kumaliza kipindi chake cha utawala.
Alisema mambo mengi yamejitokeza ambayo yamesababisha wananchi kukosa imani naye, yakiwamo ya ufisadi unaofanywa na yeye mwenyewe pamoja na watu walio karibu naye.
“Wananchi wanaona yanayofanyika, mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete, amemaliza shule hivi karibuni lakini leo ni bilionea. Haya yote hayawezi kuvumilika hata kidogo.”
Akiwashukuru wananchi wa kijiji hicho, Dk. Slaa alisema si tu kwamba wamemchagua mbunge wa Jimbo la Singida, bali ni mbunge wa nchi nzima na kwamba ni nyundo itakayotumika kuwaponda CCM.

Akizungumzia suala la CCM kujivua gamba, alisema neno fisadi alilianzisha yeye na chama chake na kwamba anayepaswa kujivua gamba hilo ni Kikwete halafu awavue wengine.

0 comments

Post a Comment