Kwa mara ya kwanza waasi wanaotaka kumpindua Kanali Gaddafi wanajitokeza katika ngazi ya kibalozi na watakutana na na tume maalum iliyoundwa hivi punde inayohusika moja kwa moja na masuala la Libya.
Masuala yanayojadiliwa ni pamoja na kuwapa msaada wa kisiasa, kijeshi na fedha waasi hao pamoja na kuelezewa mchango wa Nato.
Kabla ya mkutano huo, Mawaziri wa Ufaransa na Uingereza walidokezea kuwa wangependa kuona Nato ikijitahidi zaidi kuitenga serikali ya Kanali Gaddafi.
Tume maaulm iliundwa kwenye mkutano wa Mawaziri mjini London tareh 29 Machi na ina wajumbe kutoka Mataifa makuu ya Ulaya, Marekani, Mataifa washirika kutoka Mashariki ya kati pamoja na mashirika kadhaa ya Kimataifa.
Akiwa njiani kuelekea mkutano huo wa Qatar, Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza William Hague ameiambia BBC kuwa itabidi shinikizo zaidi za kijeshi na kisiasa dhidi ya Kanali Gaddafi.
Ufaransa na Uingereza zinataka mataifa wanachama wa Nato kutoa ndege zaidi za kijeshi kwa shughuli ya Libya ambapo Waziri wa Ufaransa wa mashauri ya kigeni,Allain Juppe alisema siku ya jumanne kuwa juhudi za Nato hadi sasa hazitoshi.
Msemaji wa Wizara ya mashauri ya kigeni wa Italy Maurizio Massari amesema kua ''suala la kuwapa silaha waasi lipo kwenye agenda bila shaka''.
Hadi sasa mashambulizi ya anga bado yameshindwa kubadili hali ya mambo kwenye medani ya vita.
Mkuu wa operesheni za Nato nchini Libya Brigadier Generali Mark Van Uhm amesema kuwa anahisi kuwa Nato inajitahidi ''ikizingatiwa zana ilizo nazo''.
Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema kuwa haijapokea ombi kutoka Nato kuongezea shughuli zake huko Libya.
Serikali ya Libya ikarudia shutuma zake za mara kwa mara ikikemea fikra za magharibi.
Msemaji wa serikali Moussa Ibrahim alisema kuwa ''Tuko tayari kupigana ikibidi. Siyo dhidi ya jeshi la Libya tu bali kila mtu na kila kabila la Libya.Akaongezea kwa kulitaja Taifa la Qatar kama shirika tu la mafuta na siyo Taifa halisi.
0 comments