Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - HABARI ZA LEO - CCM yatamba kuwashinda mafisadi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kina uhakika kitashinda vita dhidi ya ufisadi hivyo mafisadi wote ndani ya chama hicho lazima wawajibike.

Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Nape Nnauye amesema, CCM imedhamiria kumaliza ufisadi, na anayetaka kushindana na chama hicho ajaribu.

“Nataka niwathibitishieni, chama kitashinda vita hii ya ufisadi…waache wajaribu, tumeanza na tutashinda” amesema Nape leo mchana wakati anazungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma.

Amesema, vita dhidi ya ufisadi lazima ianzie ndani ya CCM yenyewe na akatoa mfano kuwa kama upo kwenye chumba chenye giza na umeshika tochi halafu mtu akakuambia nyoka huyoo, huwezi kumulika kwenye miguu ya mwenzako, unaanza kuimulika yako.

Nape amesema, CCM imeanza vita hivyo na itaimaliza na akawaomba wanachama wote wa CCM na Watanzania kwa ujumla wanaouchukia ufisadi wayasusie magazeti na vyombo vyote vya habari vinavyo shabikia ufisadi na rushwa.

“Tumeziba madirisha yote na milango yote, tunataka watu wawajibike” amesema Nape siku chache tu baada ya kusema kuwa, CCM haimuogopi mtu yeyote.

“Vita ya rushwa na ufisadi ni vita yetu sote… mwisho wa siku waathirika ni Watanzania wote” amesema kiongozi huyo wa CCM na akabainisha kwamba, madhara ya mambo hayo mabaya hayachagui itikadi ya mtu.

Nape ametoa mwito kwa waliokuwa wanachama wa CCM na wakakihama chama hicho kwa sababu ya kuchukia rushwa na ufisadi warudi kwenye chama hicho.

Amesema, maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM lazima yatekelezwe, mpango kazi wa kuyatekeleza upo lakini kwa kuwa ni siasa za ushindani hawawezi kuuweka wazi.

“Sasa tunaijenga CCM mpya kwa kuzingatia mahitaji ya wakati na mazingira” amesema Nnauye kwenye ukumbi wa Katibu Mkuu kwenye jingo la White House.

Amewapongeza wanachama wa CCM na Watanzania kwa kuyafurahia maamuzi ya Halmashauri Kuu ya Taifa, na kwamba CCM imewapa wanachokitaka.

Kwa mujibu wa mwanasiasa huyo, maamuzi ya NEC CCM ni pigo kubwa kwa wapinzani kwa kuwa, wanachama wao (wapinzani) wengi wanataka kurudisha kadi ili wajiunge na CCM.

Amesema, wanachama wengi wa CCM wameomba kukutana na sekretarieti mpya ya chama hicho, uongozi wa CCM umekubali hivyo tarehe 14 hadi 17 Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, ataiongoza kukutana na wanachama katika mikoa michache ya Tanzania Bara na Zanzibar.

“Lengo la msingi ni kupeleka kile tulichokiamua kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa” amesema na viongozi wa CCM wanakwenda kwa wananchi ili waone kuwa maamuzi ya NEC ni yao.

Amesema, Aprili 14, saa tisa alasiri, sekretarieti hiyo itafanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Nyerere Square mjini Dodoma, Aprili 15 saa 8 mchana kutakuwa na maandamano mjini Morogoro.

Siku inayofuata saa sita mchana Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete na wanachama wa chama hicho wanatarajiwa kuwapokea viongozi hao Chalinze na baadaye siku hiyo hiyo sekretarieti itakwenda Kibaha.

Aprili 16 sekretarieti hiyo inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama itaongoza maandamano jijini Dar es Salaam, na Aprili 17 itakuwa Zanzibar.

“Tunawathamini wanachama wote, sasa lakini lazima uanzie mahali…lazima pia na kazi nyingine zifanyike” amesema Nnauye na kutamba kuwa Chama Cha Mapinduzi kina nguvu nchi nzima ndiyo maana kimekuwa kinashinda uchaguzi.

0 comments

Post a Comment