MWENYEKITI wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, amesema kauli iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Wiliam Ngeleja, kwamba serikali inamiliki mgodi wa makaa ya mawe wa Kiwira ni ya kisiasa na imekwenda kinyume cha taratibu za mikataba ya uendeshaji wa mashirika ya serikali.
Zitto alimpinga Waziri Ngeleja juzi baada ya wafanyakazi wa mgodi huo kusoma risala kwa kamati yake, ambayo pamoja na mambo mengine, walihoji msimamo wa serikali kuhusu uendeshaji wa mgodi huo tangu mbia wa awali ausalimishe.
Akisoma risala hiyo, Kaimu Meneja wa mgodi huo, Aswile Mapamba, alisema Septemba 26, mwaka 2009, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, alifanya ziara katika mgodi huo na kusema kuwa mgodi huo sasa umerudi serikalini kutokana na mwekezaji kushindwa kuuendesha na kulipa watumishi wake.
Kupitia risala hiyo, alieleza Julai 2005 Kampuni ya Kiwira Coal Mines Limited ilibinafsishwa rasmi kwa Kampuni ya kizalendo ya TanPower Resources ambayo ilikuwa inamiliki hisa asilimia 70, huku serikali ikimiliki asilimia 30, lakini tangu Waziri Ngeleja atoe kauli hiyo hakuna uzalishaji wowote unaoendelea zaidi ya wafanyakazi kulia na malipo yao kila mara hata kukosa mshahara kwa wakati.
“Tangu kauli ya Waziri Ngeleja, hakuna uzalishaji wowote kiwandani wa makaa ya mawe na mpaka sasa mgodi bado haujapata taarifa ya Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na hakuna mafao waliyolipwa wafanyakazi hadi sasa zaidi ya kulipwa mishahara ya miezi kumi na tano tu,” alisema Aswile.
Aidha, alisema awali mgodi huo ulikuwa ukizalisha umeme na kuuza kwa TANESCO kila uniti moja kwa sh 43, ikiwa ni bei rahisi zaidi kuliko ile ya umeme wa Kampuni ya Dowans ambayo ilikuwa ikiuza kwa TANESCO uniti moja kwa sh 85 huku IPTL nayo ikiuza uniti moja kwa sh 95.
Meneja huyo alisema tamko la Waziri Ngeleja liliamsha ari kwa watumishi wa mgodi huo kupata moyo na kuwa na matumaini ya kuzalisha makaa ya mawe ili kuondokana na tatizo la umeme nchini.
Akijibu maswali ya wafanyakazi hao, Zitto alisema kitendo cha Waziri Ngeleja kutoa tamko hilo kimekwenda kinyume cha sheria kwani waziri huyo anajua fika kuwa bado juhudi zinafanywa na kamati yake kwa kushirikiana na serikali kuangalia jinsi ya kuurudisha mgodi huo serikalini au ikiwezekana kuukabidhi kwa mbia mwingine kwa mujibu wa sheria.
Alisema tangu Tanzania ilipopata uhuru wake hadi sasa imefanikiwa kuzalisha umeme megawati 1,034, ikiwa ni tofauti na mahitaji ya sasa ya nchi ambayo ni makubwa kwa sababu ya kukua kwa kasi kwa sekta ya viwanda.
Zitto ambaye ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisema pamoja na juhudi zilizofanyika bado hakuna ushahidi wa kisheria unaoonyesha kwa uhakika kuwa mgodi huo umerudi serikalini.
“Mgawo wa umeme na ubovu wa miundombinu umeiathiri sana TANESCO….wanapata hasara ya dola milioni moja kwa mwaka. Tungekuwa na juhudi za makusudi za kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe nchi ingeondokana na hali hii.
Ni muhimu serikali iangalie kwa makini jinsi umeme unavyoathiri uchumi wa nchi na watu wake”, alisema Zitto.
“Kama mgodi huu ungekuwa chini ya serikali leo msingewaona waendeshaji wa Kampuni ya Kiwira Coal Power Limited (KCPL) hapa, sasa tambueni bado kampuni hii ndiyo inayoendesha mgodi huu ingawa kwa kusuasua. Juhudi za makusudi zinafanywa ili kuondokana na hali hii,” alisema Zitto.
Alisema kutokana na umuhimu wa mgodi huo hivi sasa kamati yake inaunga mkono hatua ya Shirika la Hifadhi ya Jamii nchini (NSSF), kujitokeza na kutaka kuuendesha mgodi huo.
“Hapa mwenyekiti kuna tatizo na ninakubaliana nawe mwenyekiti kwamba waziri alizungumza siasa kuliko hali halisi tunavyoiona…kwa nini waziri alifanya hivyo? Lazima atupe majibu ya kina,” alisema mjumbe mwingine wa kamati hiyo ya Bunge, Murtaza Mangungu, ambaye ni Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM).
Alisema tangu serikali itoe tamko la kulipa malimbilikizo ya madeni ya watumishi wa kiwanda hicho, bado mwekezaji aliyeingia ubia na serikali na Kampuni ya Tan Power Resources kupitia Kampuni yake ya KCPL, inaonyesha kuwa bado ndiye mmiliki halali wa mgodi huo.
Mgodi huo uliotarajiwa kuongeza uzalishaji wa makaa ya mawe kutoka tani 44,000 kwa mwaka hadi tani 270,000 umeelezwa kusababisha masoko ya nje kukosa makaa ya mawe kufuatia kusimama kwa shughuli zake za uzalishaji.
Mwaka 2008 Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ilifanya ziara na kukutana na mwendeshaji wa Kampuni ya KCPL, Francis Tobaro na kugundua kuwa hakuna uzalishaji unaoendelea katika mgodi huo.
Wamiliki wa Mgodi huo wa Kiwira hapo awali walitajwa kuwa ni Nick Mkapa, Fostar Mkapa na B. Mahende na wengine ni D. Yona na Danny Yona Jr (kupitia Devconsult Ltd), wote wakiwa ni sehemu ya wamiliki wa mgodi huo uliopo wilayani Ileje, mkoani Mbeya.
Mgodi wa Kiwira ulianzishwa mwaka 1983 na kuanza uzalishaji Novemba 11, 1988 lakini baadaye ulibinafsishwa kwa Kampuni ya Tan Power Ltd inayomiliki hisa asilimia 80 huku serikali ikimiliki asilimia 20 ya hisa hizo.
0 comments