Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sasa ni marufuku ndege kuruka Libya. Ujerumani, China, Urusi, Brasil na India zapinga

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter


Baraza la Usalama la umoja wa mataifa limeidhinisha azimio la kuiwekea Libya marufuku ya ndege kuruka kwenye anga yake baada ya kukihitimisha kikao chake cha dharura.




Kulingana na azimio hilo,jamii ya kimataifa ina uwezo wa kufanya kila iwezalo kuishinikiza marufuku huyo itimizwe ila haliruhusu uvamizi wa moja kwa moja kwenye ardhi ya Libya.Hatua hiyo imezua hisia tofauti katika jamii ya kimataifa.
10 kwa 5
Azimio hilo,1973, liliidhinishwa na mataifa 10 kati ya yote 15 wanachama wa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa.Ifahamike kuwa matano yaliyosalia hayakushiriki katika zoezi hilo.Orodha ya mataifa hayo inayajumuisha Ujerumani,China,Urusi,Brasil na India.Kwa upande wake,Marekani imefurahishwa na matokeo ya azimio hilo lililo na azma ya kuyadhibiti mashambulio ya angani.Balozi wa Marekani katika Baraza  la Usalama la Umoja wa Mataifa Dr Susan Rice alisisitiza kuwa lengo la hatua hiyo ni kumwasilishia Kanali Gaddafi ujumbe maalum kuwa "Mosi ni kuwalinda raia…kadhalika kuuwekea mbinyo zaidi uongozi wa Kanali Gaddafi pamoja na vikwazo vikali zaidi.Kwa pamoja vipengee hivi vya azimio 1973 vitafanikiwa na sharti vitimizwe na uongozi wa Gaddafi."

Mashambulio ya angani


Msimamo huo unaungwa mkono na Uingereza,Lebanon na Ufaransa.Kulingana na wanadiplomasia wa Uingereza,Ufaransa na Marekani,vikosi vya Kanali Gaddafi huenda vikashambuliwa kwa anga katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi ya Benghazi.Hata hivyo,viongozi hao wa kimataifa wameyatolea wito mataifa ya Kiarabu kuwaunga mkono katika harakati hizo.Ufaransa iliyokuwa mstari wa mbele kuzipa msukumo juhudi za kuliidhinisha azimio hilo nayo pia imetiwa moyo na matokeo.


EU na ushirikiano


Kwa upande wake Umoja wa Ulaya nao pia umeiunga mkono hatua hiyo.Katika taarifa yao ya pamoja,Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Ulaya,Herman Van Rompuy,na mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya ,Catherine Ashton,azimio hilo linaipa jamii ya kimataifa fursa ya kuwalinda raia wa Libya kwa kufuata misingi ya sheria.Wanadiplomasia hao wa ngazi za juu wameusisitizia umuhimu wa kushirikiana kwa karibu na Umoja wa Mataifa pamoja na jumuiya mbili zinazoiunga mkono hatua ya kuiwekea Libya marufuku ya ndege kuruka kwenye anga yake,Umoja wa Mataifa ya Kiarabu na ule wa Afrika,AU.Umoja wa Ulaya umeandaa vikao maalum vya majadiliano zaidi kuhusu utekelezaji wa hatua hizo ifikapo tarehe 21 mwezi huu.


Msimamo wa Ujerumani


Hata hivyo Ujerumani ambayo haikulipigia kura azimio hilo, imesisitiza kuwa inaziunga mkono juhudi zote za kuwalinda raia wa Libya ila kamwe haitowapeleka wanajeshi wake kushiriki kwenye operesheni yoyote ile ndani ya ardhi ya nchi hiyo.Waziri wa Mambo ya Nje Guido Westerwelle alifafanua kuwa kuna hatari nyingi na uwezekano wa ajali jambo linaloifanya Ujerumani kutokiunga mkono kipengee hicho.
Hali ilivyo mashariki ya Libya:jambo lililolifanya baraza la usalama la UN kuidhinsha marufuku ya ndege kuruka
Mchango wa nyenzo
Msimamo huo unaungwa mkono na Poland itakayotoa usaidizi kwenye suala la nyenzo.Norway kwa upande wake imeeleza kuwa itashiriki kwenye operesheni hiyo ila haijafafanua kwa njia gani.Denmark nayo inasubiri idhini ya bunge kabla ya kuitoa kauli yake kuhusu suala hilo.


Ifahamike kuwa utekelezaji wa azimio hilo utategemea mchango wa zana za angani kwani linayapiga marufuku majeshi yoyote ya nchi kavu kuingia Libya.
Tags:

0 comments

Post a Comment