USHUHUDA zaidi umezidi kueleza kwamba tiba inayotolewa Loliondo na Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile (78), inaponya magonjwa mbalimbali sugu yakiwamo magonjwa ya ukimwi na kisukari.
Taarifa za kiushuhuda zilizolifikia Tanzania Daima Jumapili kwa zaidi ya wiki moja sasa kutoka kwa maofisa wa serikali wilayani Ngorongoro na baadhi ya wagonjwa walioeleza kuinywa dawa ya mchungaji huyo maarufu kwa jina la Babu, zimesema tiba hiyo inatibu kwa imani na kwamba tayari wapo wagonjwa kadhaa wa ukimwi waliopimwa hospitalini baada ya kuitumia dawa hiyo na kuonekana hawana virusi vya ugonjwa huo tena.
Mmoja wa mashuhuda wa uponyaji wa tiba hiyo inayotolewa katika Kijiji cha Semunge wilayani humo, ni Mollel Lucas, ambaye amejitambulisha kuwa ni ofisa wa serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro anayeshughulikia masuala ya maendeleo ya jamii.
Kwa mujibu wa Mollel, yeye na baadhi ya watendaji wenzake ndio waliokuwa wa kwanza kushuhudia uponyaji wa dawa hiyo baada ya mwanakikundi mmoja kilicho chini ya kamati ya halmashauri kuinywa dawa ya babu huyo na baadaye kupimwa hospitalini na kuonekana hana tena virusi vya ukimwi alivyokutwa navyo awali.
Akifafanua zaidi ushuhuda wake huo, alisema katika halmashauri yao kuna kamati inayoitwa SIMAC inayofanya kazi za kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi na kamati hiyo pia ina kikundi cha kuwasaidia watu wanaoishi na virusi vya ugonjwa huo kwa kuwapa misaada mbalimbali.
Alisema taarifa juu ya tiba hiyo iliwafikia kupitia mwanachama mmoja wa kikundi hicho aliyekuwa amefiwa na mumewe na ambaye baada ya kupima katika hospitali za wilaya na mkoa aligundulika kuwa ameambukizwa virusi hivyo.
Alisema dada huyo alikuwa pia akitumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs) lakini hali yake haikuwa nzuri, lakini baada ya kupewa dawa ya mchungaji huyo hatimaye alianza kujisikia vizuri na hatimaye kubaini kuwa amepona.
“Bahati nzuri huyo dada anakaa karibu kabisa na mchungaji huyo kwa hiyo aliweza kupata tiba ya Mwasapile …ni mmoja wa watu wa mwanzo kabisa kutibiwa, tunamjua vizuri.
Baada ya kutumia tiba hiyo hali yake ilibadilika na kurudi kama zamani ndipo aliporudi kwa mchungaji Mwasapile na kumuelezea kuhusu afya yake …na Mwasapile alimtaka akapime kwa mara nyingine ili kuona kama ugonjwa huo umekwisha,” alieleza.
Alisema aliporudi katika hospitali aliyofanyia kipimo mara ya kwanza madaktari walistaajabu kukuta hana virusi vya ukimwi lakini waliamini kuwa walikosea vipimo vyao na kumtaka akapime hospitali za juu zaidi.
“Alipopima katika zahanati ya Digodigo ambapo kuna huduma hiyo aligundulika hana virusi hivyo, wakaamua kumwandikia ili kupata uhakika katika hospitali teule ya Waso, ambayo ilikuwa imemuanzishia dozi ya ARVs lakini nako walipompima hawakukuta virusi hivyo,” alisema na kuongeza:
“Taarifa za dada huyo ambaye ni mwanachama wa kikundi cha halmashauri zilizagaa kila kona hata baadhi ya wanachama wengine wakalazimika kwenda kunywa dawa hiyo.”
Kwamba, hali hiyo ilisababisha wagonjwa waliokuwa wakitumia dawa za kupunguza makali ya ukimwi kupungua idadi yao, na halmashauri ikalazimika kutuma Mratibu wa Ukimwi wa wilaya upande wa afya kwenda kuonana na babu Mwasapile kumshauri asitishe dawa yake.
“Hiyo ilikuwa Juni 2010 lakini hata baada ya kurejea watu ndiyo walizidi kumiminika kwa mchungaji huyo, hivyo halmashauri ilibidi ikae na mkuu wa wilaya ili kuona namna ya kumzuia babu huyo, maana wengi walikuwa wakikatiza dozi,” alieleza.
Alisema hata hivyo hawakuweza kwani ilibidi kurudi tena kwa Mchungaji Mwasapile Juni 26, 2010 na kumuomba awasaidie kuwaambia wagonjwa hao wasiache kutumia ARV’s pindi wanapokunywa tiba hiyo ambayo mti wake kwa Kimasai unajulikana kama Lawa.
“Kama SIMAC tulikaa na mkuu wa wilaya na kumuelezea hofu yetu ya watu kukatiza tiba za ARVs tukimwomba hasimamishe huduma za mchungaji huyo lakini ilishindikana, kwani usafiri ukawa shida baada ya watu kugundua kuwa halmashauri ina mpango wa kuzuia,” alisema.
Alisema wakati huo kutoka makao makuu ya Wilaya ya Ngorongoro mpaka kufika kwa Mchungaji Mwasapile nauli ilikuwa sh elfu tano, lakini ilianza kuongezeka kadiri watu walivyokuwa wakitoa taarifa za sifa ya tiba hiyo.
Molleli alisema katika kipindi hicho tiba hiyo ilikuwa ikidaiwa kutibu kwa siku 21 lakini hadi kufikia Desemba mwaka 2010 ilidaiwa kuwa inaponya ndani ya kipindi cha siku saba pekee.
Mwingine aliyeelezwa kuwahi kuitumia tiba hiyo ambaye alikuwa alidhaniwa angefariki dunia muda wowote kutokana na maradhi ya ukimwi ni mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Babati aliyekuwa mahututi lakini baada ya kunywa dawa hiyo alipona na kuendelea na kazi.
“Ni wengi sana waliokunywa dawa hiyo na kupona… hasa wanachama wa kikundi chetu, lakini ilipofika Desemba dawa hiyo ilijulikana zaidi kwa kuponya magonjwa mengi, ikiwamo kisukari na presha (shinikizo la damu),” alisema.
Aidha, kuna taarifa pia zinazomhusu mtaalamu mmoja wa masuala ya maji katika wilaya hiyo, kwamba aliponywa ugonjwa wa kisukari na hivi sasa afya yake imeimarika huku akiwa na uwezo wa kutumia vyakula mbalimbali ambavyo mwanzoni alikatazwa kabisa kuvitumia.
Ushuhuda mwingine ulioelezwa ni wa kijana mmoja ambaye alikuwa akipewa dawa za ARVs kwa takriban miaka 18 lakini mara baada ya kutumia tiba hiyo sasa anaonekana amepona kabisa magonjwa nyemelezi yaliyokuwa yakimsumbua. (majina ya wote waliotajwa kupona kwa sasa yanahifadhiwa).
Hata hivyo, wapo mashahidi wengine waliojitokeza na kuwa tayari kuripotiwa kwa majina yao kuhusu uponyaji uliofanywa na tiba hiyo na miongoni mwao wamo maaskofu wa KKKT.
Kanisa hilo la Kilutheri limesharipotiwa likitoa msimamo wake kwamba: “Linaitambua na kubariki dawa inayotolewa na Mchungaji wake mstaafu anayefanyia shughuli zake Loliondo, Ambilikile Mwasapile”, huku baadhi ya maaskofu wa kanisa hilo wakithibitisha kwamba wamekunywa dawa hiyo na kuponywa.
Kwa nyakati tofauti, maaskofu wa kanisa hilo, Thomas Laizer wa Dayosisi ya mkoani Arusha, Dk. Martin Shao wa Dayosisi ya Kaskazini, walisema huduma inayotolewa na Mchungaji Mwasapile ni sahihi na imeanza siku nyingi na kwamba wao ni miongoni mwa watu wa mwanzoni waliowahi kunywa dawa hiyo na kupona.
Askofu Laizer alisema kwa mujibu wa imani na taratibu za KKKT, mchungaji huyo yupo sahihi na kwamba hawana mgogoro naye.
“Ifahamike kwamba kazi ya utoaji dawa haikuanza jana, ilianza siku nyingi na mimi kama askofu niliyembariki Mchungaji Mwasapile, nililetewa taarifa na wachungaji wengine pamoja na wakuu wangu wa majimbo juu ya mafunuo ya mchungaji na ndipo tulipoanza kufuatilia na kufanya mahojiano naye na kanisa likagundua kwamba tiba yake ipo sahihi,” alisema Askofu Laizer.
Askofu Laizer alisema binafsi alikuwa akisumbuliwa na kisukari pamoja na shinikizo la damu kwa muda mrefu, lakini baada ya kupewa dawa ya mchungaji huyo amepona na hajapata kunywa dawa nyingine.
“Dawa inayofanyika pale inaambatana na sala na imani, lakini watu wanashangaa.
“Mke wa Askofu mwenzangu Akyoo alikuwa hawezi kutoka, alikuwa akisumbuliwa na kisukari, lakini baada ya kupewa dawa hiyo juzi nilipompigia simu akasema amepona na yupo kwenye harusi,” alisema.
Hata hivyo gazeti hili halikufanikiwa mara moja kupata uthibitisho wa vyeti vya baadhi ya wagonjwa hasa wa ukimwi ambao wamedaiwa kupona, kwani wengi wameamua kuwa wasiri kutokana na unyeti wa ugonjwa huo.
Wakati huo huo watu watano wamefariki dunia na wengine kumi na nne kujeruhiwa vibaya katika ajali iliyohusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso katika eneo la Kijiji cha Esilalei, Mto wa Mbu wilayani Monduli, yaliyodaiwa kuwa yalikuwa yakielekea Loliondo kwa babu huyo.
Magari hayo yalikuwa katika mwendo wa kasi kwa sababu ya kile kilichoelezwa kuwa dereva alikuwa akijaribu kuwawahisha abiria wake kwenye tiba ya babu huyo.
Katika ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 11:30 alfajiri ya jana katika eneo hilo madereva wa magari yote mawili yenye nambari za usajili T.606 ABU na T. 681 ABX na mtu na mkewe walifariki papo hapo.
Habari za ajali hiyo zilizothibitishwa na Ofisa Mnadhimu wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa, zilieleza kuwa ajali hiyo kwa mujibu wa taarifa za awali ilisababishwa na vumbi lililotanda eneo hilo hivyo kufanya madereva wote wawili kukosa mwelekeo na kugongana.
“Ni kweli ajali hiyo imetokea alfajiri ya leo na watu watano wamefariki dunia na wengine kumi na watatu wamejeruhiwa nadhani kwa taarifa za awali tunaweza kueleza kuwa zimesababishwa na mwendo wa kasi, kwani magari hayo mawili moja lilikuwa linatoka Loliondo na jingine linakwenda Loliondo kwa ‘Babu’ si unajua shauku ya kupata tiba’, alisema kamanda huyo.
Kamanda Mpwapwa aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni Zakayo Laizer (36) ambaye alikuwa dereva katika gari namba T. 606 ABU na dereva mwingine ni Beatus Morris Kiboa (39), ambaye alikuwa dereva katika gari nambari T. 681 ABX. Wengine ni Raphael Kiboa (65) na mkewe aliyetajwa kwa jina la mama Kiboa (62) na Ismail Ngozi Mohamed (38).
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo na hali zao kuelezwa kuwa haziridhishi ni pamoja na Kordin Silangei (55), Elibariki Raphael (58), Asna Hassan (60), Namayani Legeri (40), Kirita Mediliyeki (65), Ngaisi Francis (38) na Sangau Magalla (90).
Majeruhi wengine ni Estomih Ole Muunyo (54), Erick Lukas aliyetajwa kuwa ni mwanafunzi, Evalyne Lukas (40), Mama Tivae (28), Anord Michael (11) na Elibariki Kiboa (49), ambao kwa mujibu wa Kamanda Mpwapwa majeruhi wote wamelazwa katika Hospitali ya Serikali wilayani Monduli.
Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi zaidi kujua chanzo cha ajali hiyo na kuwaonya madereva kuacha kuendesha gari katika mwendo wa kasi.
Tangu kuibuka kwa mchungaji huyo makundi kwa makundi ya watu wakiwamo vigogo wa serikali, viongozi wa dini na vyama vya siasa, wamekuwa wakimiminika kijijini Samunge usiku na mchana kwa ajili ya kwenda kuwahi tiba hiyo.
0 comments