Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Safisha safisa sasa kuingia ndani ya CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

HOFU imetanda ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya kuwapo kwa tetesi kuwa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho imepanga kukisafisha chama kwa kuwatosa kwenye uongozi baadhi ya wanachama wanaodaiwa kuwa mzigo.
Tanzania Daima Jumapili, limedokezwa kuwa Rais Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM ndiye atakayekiongoza kikao hicho huku ajenda kubwa zikielezwa ni kutafutana namna ya kuzima moto uliowashwa na CHADEMA pamoja na kukisafisha chama ili kirejeshe imani kwa wananchi.
Miongoni mwa watu wanaodaiwa kukalia kuti kavu ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba, ambaye inadaiwa amekuwa ni miongoni mwa watu wanaowagawa wanachama pamoja na kufanya uteuzi kwa masilahi ya kundi fulani.
Makada wa CCM wameidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa tangu kuteuliwa kwake Makamba ameshindwa kuvaa viatu vya aliyemtangulia Philip Mangula, ambaye alisifika kwa kujenga umoja ndani ya chama pamoja na kushirikiana na viongozi wa upinzani katika shughuli mbalimbali.
Walidokeza kuwa Makamba ameshindwa kumshauri Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete, hatua madhubuti dhidi ya wanachama wanaodaiwa kukiyumbisha chama kiasi cha kukifanya kipoteze imani na umaarufu wake kwa wananchi.
Inasemekana matokeo mabaya iliyoyapata CCM yamechangiwa zaidi na makundi yasiyoelewana ndani ya chama hicho pamoja na kuwapitisha wagombea wasiotakiwa na wananchi katika kuwania nafasi za ubunge na udiwani, hivyo kuzusha hasira kwa wanachama na wananchi walioamua kuwapigia kura wapinzani.
Taarifa kutoka Ikulu zilizoifikia Tanzania Daima Jumapili zimedokeza kuwa mara baada ya Rais Kikwete kumaliza kikao cha NEC, Rais Kikwete ataanza ziara za mikoani zenye lengo la kuwashukuru wananchi kwa kukichagua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuongoza kwa awamu ya tano.
“Ndugu yangu ratiba niliyoisikia baada ya kikao cha Dodoma, Mheshimiwa Rais Kikwete atapita mikoani kuwashukuru wananchi waliomchagua. Sina hakika sana ataanzia mikoa gani ila atapita kote pamoja na shukrani pia kufanya kazi za kukiimarisha chama,” kilisema chanzo kimoja.
Duru za siasa ziliidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa ziara hizo za Rais Kikwete zinalenga kupunguza moto uliowashwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho hivi sasa kimekuwa kikifanya maandamano na mikutano katika mikoa ya Kanda ya Ziwa kupinga malipo ya Dowans ya sh bilioni 94, mgawo wa umeme na hali ya maisha.
Maandamano hayo ya CHADEMA yameonekana kumtisha Rais Kikwete ambaye katika hotuba ya mwisho wa mwezi Februari alikionya chama hicho kuacha kufanya uchochezi wa kuwahamasisha wananchi kuiondoa serikali iliyopo madarakani kinyume cha katiba.
Rais Kikwete alisema CHADEMA inahatarisha amani na utulivu uliopo na kuwataka wananchi wakatae ushawishi huo wa CHADEMA kwani unaweza kuwasababishia mauti ambayo hata hivyo hakuyafafanua yatapatikana vipi.
Hata hivyo hotuba hiyo ilipingwa vikali na CHADEMA, ambao walisema wao hawafanyi uchochezi wowote bali Rais Kikwete na CCM wanahofia wananchi kutambua haki zao na kuzidai ahadi walizopewa kwenye kampeni za uchaguzi za mwaka 2005 na 2010.
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na wabunge wengine wanaonekana kuwanyima usingizi wanachama na vigogo wa CCM kiasi cha kupanga mikakati ya kuwakabili.
Miongoni mwa mikakati hiyo ni ziara inayofanywa hivi sasa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, katika Mkoa wa Kagera, ambako mbali na kufanya shughuli za serikali pia atakuwa akifanya zile za chama kwa lengo la kufuta nyayo zilizoachwa na CHADEMA inayoonekana kuwa tishio kwa chama tawala.
CCM wameingiwa hofu zaidi baada ya kubaini kuwa CHADEMA imekuwa ikitumia turufu ya matatizo ya wananchi kujipatia umaarufu na wanaungwa mkono na idadi kubwa ya vijana ambao wanakabiliwa na tatizo la uhaba wa ajira.
Hofu hiyo imesababishwa na matukio ya hivi karibuni katika nchi za Tunisia na Misri, ambapo marais wake walijiuzulu baada ya wananchi kufanya maandamano kwa takriban wiki mbili kupinga hali ngumu za maisha huku wakiwashinikiza marais hao kuachia nyadhifa zao.
Vigogo wa CCM wameanza kuingiwa kihoro kuwa hali hiyo inaweza kutokea hapa nchini kama CHADEMA wataendelea na maandamano yao na mikutano ya hadhara, hivyo wanafanya jitihada za kuzima harakati hizo za chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
Katika ilani ya uchaguzi ya mwaka 2005, CCM ilibainisha kuwa itatengeneza ajira milioni 1.5 ndani ya miaka mitano lakini hata hivyo ahadi hiyo inaonekana kutotekelezwa licha ya viongozi wa chama hicho tawala kutoa takwimu kutimizwa kwa ahadi hiyo.
Hivi karibuni Umoja wa Vijana wa CCM, (UVCCM) kupitia kwa mjumbe wake wa kamati ya utekelezaji, Zainabu Kawawa, ulisema serikali haijafanya jitihada za kutosha kukabiliana na tatizo la ajira hasa kwa vijana, ambapo kila mwaka wahitimu 700,000 kutoka vyuoni huingia mitaani kutafuta kazi.
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, naye alisema serikali inapaswa kuwa makini na suala la ukosefu wa ajira kwa vijana, kwa kuwa ni bomu la muda, ambalo likilipuka amani na utulivu vinavyoimbwa hivi sasa havitakuwa na nafsi.
Matatizo ya ukosefu wa ajira, mgawo wa umeme, kupanda kwa gharama za maisha na nyinginezo ndizo zinaijengea umaarufu CHADEMA na kuonekana ikijali zaidi matatizo ya wananchi kuliko chama tawala kinachodaiwa kushindwa kuzitumia rasimali za taifa kwa faida ya walio wengi.
Serikali ya CCM inadaiwa kuwalinda na kuwakumbatia watu wanaoshiriki kwenye vitendo vya ufisadi wa rasilimali za taifa ambazo kama zingetumika vizuri zingeweza kuwasaidia watu wengi zaidi.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wameidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa NEC itakayokutana wiki hii ndiyo itakayotoa mwelekeo wa chama hicho, kinyume cha hapo chama hicho kitakuwa kinajichimbia kaburi na uchaguzi wa mwaka 2015 kitapata pigo kubwa.
Walieleza kuwa Rais Kikwete anaweza kuweka historia na kukiimarisha chama kama atatekeleza kwa vitendo ahadi ya kuijenga upya CCM ambayo aliitoa kwenye kilele cha sherehe za miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM.
Wachambuzi hao wanaweka bayana kuyumba kwa chama hicho pia kumechangiwa zaidi na uongozi wa Rais Kikwete ambaye anadaiwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya makada wanaodaiwa kuendesha njama za chini chini za kuwamaliza wenzao kisiasa kuanzia majimboni, katani na chamani.
Wanaeleza kuwa sababu ya Kikwete kushindwa kuwachukulia hatua ni kwa sababu ndio waliomsaidia kwa kiasi kikubwa kuingia ikulu mwaka 2005 baada ya kampeni zinazodaiwa zilitumia fedha na nguvu kubwa ikiwemo kuwachafua wagombea wengine waliokuwa wakiwania uteuzi wa kugombea urais.
Wanaongeza kuwa umaarufu wa CCM unazidi kupotea kwa sababu imeshindwa kuboresha maisha ya wananchi kama ilivyoahidi mwaka 2005, 2010 na badala yake kila kitu kimepanda, hivyo kumfanya mwananchi akose imani na chama hicho kilichokaa madarakani kwa miaka 34.
Tags:

0 comments

Post a Comment