Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk. Slaa amponda Tendwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Willibrod Slaa amesema pamoja na ofisi yake kupokea barua ya onyo kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa chama chake hakitachukua hatua yoyote kwa madai kuwa Msajili huyo amepoteza sifa.

Dk. Slaa amesema ,Tendwa ameshindwa kushughulikia matatizo yanayowasilishwa kwake na vyama vya upinzani na kutolea mfano malalamiko yaliyotolewa na chama chake kuhusu wafuasi wa chama hicho kupigwa mabomu ya machozi wakati wa maandamano yaliyofanyika Arusha mwanzoni mwa mwaka huu.

Dk. Slaa amesema, kitendo cha msajili wa vyama kufumbia macho matatizo ya vyama vya upinzani na kufanyia kazi malalamiko ya CCM tu ni kukilinda chama hicho, jambo ambalo alisema linawafanya wapinzani wakose imani naye.

Kwa mujibu wa Slaa, kuna barua nyingi za malalamiko zimewasilishwa kwa Tendwa kuhusu mambo mbalimbali ambayo wanaamini kama angekuwa anataka kuvitendea vyama vyote usawa, angeanza na hayo badala ya kushughulikia ya sasa.

“Tendwa hawezi kutuandikia barua sisi wakati yeye ni mlinzi wa CCM. Yeye ameshapoteza sifa za kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,” Slaa alisema na kukata simu.

Dk. Slaa ameyasema hayo kufuatia barua ya Tendwa aliyomwandikia Katibu huyo wa Chadema na nakala kusambazwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge na Uratibu, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu) na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika barua hiyo ya Machi 2 yenye kichwa cha habari ‘Ukiukwaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa’; Tendwa ameitaka Chadema kuacha mara moja tabia na vitendo vya uchochezi, huku akisisitiza kuwa, kinyume cha hapo hatua kali za kisheria zitafuata.

“Vitendo hivi si tu vinavunja heshima ya chama chenu, bali vinahatarisha amani na usalama wa nchi, hatuwezi kuacha viendelee bila kuchukua hatua,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Tendwa mwenyewe.

Akielezea kiini cha kuandika barua hiyo ya onyo, Tendwa ameeleza: “Hivi karibuni kumejitokeza vitendo vya uvunjaji sheria ya vyama vya siasa kwa baadhi ya viongozi wa chama chako (Chadema) kwa kisingizio cha kutekeleza haki ya kikatiba. Ikumbukwe, kwamba Katiba imetoa wajibu kwa kila mtu kuitii na sheria za Jamhuri ya Muungano.

“Katika mikutano ya Chadema iliyofanyika Arusha, Mwanza na Musoma, viongozi wa Chadema wamesikika wakitoa lugha za vitisho, kashfa, uchochezi, matusi kinyume cha Sheria namba 5 ya Vyama vya Siasa ya 1992 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 pamoja na Kanuni na Maadili ya Vyama vya Siasa za mwaka 2007.

"Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inakemea na kutoa onyo kwa viongozi wa Chadema kuacha tabia na vitendo hivi … vinginevyo hatua za kisheria zitafuatwa kwa mujibu wa sheria.”

Kauli ya Msajili haitofautiani na ya Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais – Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira, aliyeonya juu ya kauli za Chadema huku akisisitiza kuwa Serikali ina ukomo wa kuvumilia endapo chama hicho hakitajirekebisha.

Baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani waliojitokeza kuipinga Chadema ni Mbunge wa Bariadi ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa UDP, Mwenyekiti wa TLP ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema, ambao kwa nyakati tofauti wameitaka Chadema kufanya maandamano ya amani na yenye kulenga ustawi wa nchi.

“Mimi nasema maandamano wafanye hata watembee usiku mzima, lakini suala la amani kwao liwe la kipaumbele katika nchi yao,” alisema Cheyo. Mrema alionya kuwa, kauli za Chadema zinalenga kuharibu amani ya nchi na kuwataka kutoweka mbele ubinafsi.

Chama Cha Jamii (CCK), kupitia Mwenyekiti wake, Costantine Akitanda, nacho kimeiomba Serikali kuichukulia hatua Chadema kutokana na mikutano na kauli zao kuashiria kuliletea Taifa machafuko na kuhatarisha amani ya wananchi wake.

Akizungumza juzi Dar es Salaam, Akitanda, alisema kuwa wana wasiwasi na kauli zinazotolewa na viongozi wa chama hicho kwenye mikutano yao.

Alisema kuwa, hawailalamikii mikutano inayofanywa kwa kuwa ni haki kisheria isipokuwa kauli iliyotolewa na Dk. Slaa kumtaka Rais Kikwete kutoa majibu waliyoyataka ndani ya siku tisa ni sawa na kuleta uchochezi baina ya wananchi na Serikali.

“Mfano kauli ya kumpa Rais siku tisa, vinginevyo awapishe Ikulu, inaweza kuleta tatizo. Mikutano isitumike kujenga chuki bali iwezeshe kuelimisha wananchi kuhusu mambo ya maendeleo, kwenye siasa hakuna uadui,” alisema Akitanda.

Tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 31 mwaka jana na mgombea urais wa CCM, Rais Kikwete kuibuka mshindi, huku chama chake kikizoa wabunge na madiwani, uongozi wa Chadema umekuwa ukiibua malumbano, kuanzia wakati wa kutangazwa kwa matokeo ya urais, uchaguzi wa mameya na wenyeviti wa halmashauri na sasa katika maandamano yanayotajwa, kuchochea vurugu nchini.
Tags:

0 comments

Post a Comment