Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Pinda aeleza kwa nini alimzuia Magufuli

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametoa ufafanuzi kuhusu kauli yake ya kumzuia Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kuendeleza bomoabomoa inayofanyika nchini, akisema Serikali imelazimika kusitisha kazi hiyo kwa sababu kuna mambo yanayobidi kuchukuliwa hatua kwanza ikiwamo kutoa elimu kwa wananchi.

Alikuwa akizungumza na viongozi wote wa Mkoa wa Kagera wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya siku tisa katika mkoa huo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, mjini Bukoba juzi.

“Sheria inayotumika ni ya mwaka 1937, tunapaswa tuwaelimishe wananchi sheria inasema nini. Katika hali hii, tunapaswa tuangalie zoezi zima linavyoendeshwa sababu kuna watu wamejinyima wakajenga makazi yao ya kudumu, kuna watu wamewekeza miradi katika maeneo haya, hakuna aliyewazuia wasijenge japo sheria ilikuwepo...,” alisema Pinda kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ofisi yake mjini Dar es Salaam.

Alisema Serikali haina budi kujipanga upya kwa sababu zoezi hilo limeleta malalamiko kutoka sehemu mbalimbali na katika hatua ya awali amewaandikia barua wakuu wote wa mikoa akiwataka wampatie orodha ya barabara ambazo zinajengwa na athari zake katika maeneo ya mijini na vijijini.

“Nimemwomba kila Mkuu wa Mkoa alete orodha ya barabara ngapi zinajengwa sasa, ngapi zinatarajiwa kujengwa, nyumba ngapi zitaathiriwa na zoezi hilo; ngapi zilijengwa kabla ya sheria kupitishwa… nataka tupate taarifa inayoonesha mchanganuo wa maeneo ya mijini na vijijini,” alisema Pinda.

“Lazima tuangalie makazi ya watu yalivyojengwa, tuangalie athari zake zikoje, athari haziwezi kuwa uniform (zinazofanana) katika maeneo ya mijini na vijijini… tutafute njia mbadala na kujiuliza, je hapa hatuwezi kupindisha barabara ili kuepuka balaa la kuwabomolea watu na Serikali kuingia gharama za kulipa fidia?”

Alisema katika maeneo mengi, ndani ya mita 30 za eneo la barabara kuna majengo ya taasisi za umma au ya huduma za kijamii kama vile hospitali, benki, misikiti na makanisa. “Je tuzibomoe zote hizo kwa sababu sheria inasema hivyo,” alihoji na kuongeza kuwa: “Inabidi tufanye analysis (tathmini).”

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema anacholenga ni kumsaidia mtu wa chini aondokane na umasikini kwa vile anaamini fedha inayotolewa na Serikali ni nyingi, lakini inahitaji usimamizi wa kutosha.

“Sisi tuliopewa dhamana ya kuwasaidia wananchi tunapaswa tuungane bila kujali kama wewe ni kiongozi wa dini, wa NGO au wa sekta binafsi. Tukitaka kwenda mbele, tuungane kwa pamoja kumsaidia Mtanzania aweze kusonga mbele,” alisema.

Akisisitiza umuhimu wa kutumia fedha ya Serikali alisema, wakurugenzi watendaji wa halmashauri hawana budi kujitoa ili wawaendeleze watu waliokabidhiwa kuwaongoza.

“Ningependa kuona tuna viongozi wanaoumwa na kero za wananchi, wakurugenzi jiulizeni ni fursa zipi zilizomo katika wilaya zenu… Mkurugenzi mzuri ni yule mwenye kiu ya kuendeleza watu aliokabidhiwa na siyo kuwa mtu wa mshahara tu,” alisisitiza.

“Ninasema hivi kwa sababu fedha za miradi zinazoletwa kwenu kutoka Serikali Kuu ni nyingi, lakini hazijafanya kitu cha msingi cha kumkomboa mtu wa chini kutokana na umasikini,” alisema.

Amewataka wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri na watendaji wote Serikali kila mmoja kuhakikisha kuwa ana Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

“Kama kuna watu bado hawana, naagiza sasa kila mmoja awe nayo, nikifanya ziara katika mkoa mwingine niwakute wanazo. Huwezi kusimamia maendeleo wakati huna nyaraka hizo,” alisisitiza.
Tags:

0 comments

Post a Comment