Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mwanyi alipojiuzulu uwaziri wa mambo ya ndani mwaka 1977

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Uadilifu wa Mzee Mwinyi huu hapa

Barua yake ya kujiuzulu yathibitisha
Ni changamoto kwa wanaojiuzulu sasa Alishinda umakundi, visasi na chuki
Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi.

Wakati Taifa likipita katika kupindi kigumu cha kupima uadilifu wa viongozi, wengine wakijiuzulu na kuendelea kulalamika, Nipashe imefanikiwa kupata barua ya kujiuzulu aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Ali Hassan Mwinyi, ikithihibitisha jinsi kiongozi huyo alivyo juu kwa viwango vya utiifu na uadilifu.

Katika barua hiyo ambayo inasambazwa kwenye mitandao kwa sasa, inaonyesha jinsi Mwinyi alivyojiuzulu kwa unyenyekevu Januari 22, 1977 wadhifa wa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Kiongozi huyo ambaye mwaka 1985 alikuja kukwea tena ngazi kuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika barua aliyomwandikia Rais wake, Mwalimu Julius Nyerere, anaeleza jinsi binafsi alivyoguswa na mauaji ya watu wanaoshukiwa kuwa wachawi katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza mwaka 1975.

Kwa maneno yake Mwinyi alisema: “Kisiasa nakiri kuwa nahusika, siwezi kukwepa kwa sababu dhamana yangu ya uwaziri inaambatana na wajibu unaonitaka nijue yanayotendeka wizarani na pia niweze kudhibiti na kuhakikisha mwenendo mwema wa Jeshi la Polisi.”

Mwinyi alijikuta katika matatizo hayo baada ya Jeshi la Polisi kuendesha operesheni ya kusaka wauaji wa wachawi katika mikoa ya Mwanza na Shinyanga, na alikiri kwamba:

“…vyombo vinavyohusika na utekelezaji, polisi ikiwemo, vilivuka mipaka ya wajibu wao na vikajipa madaraka ya kuogelea katika vitendo viovu vya kishenzi, kinyama na kikatili hata baadhi ya watu waliokamatwa kwa kushukiwa tu kwamba wanahusika wakafa na wengine wakapata vilema vya kudumu.”

Ingawa Mwinyi aliweka bayana kwa bosi wake, Mwalimu Nyerere, kwamba kijinai asingehusika kwani hakushiriki wala kushauri, kuagiza wala kuelekeza mambo hayo yafanywe hivyo, aliandika barua isiyo na kinyongo kabisa na yenye unyenyekevu mkubwa kwa Rais Nyerere.

Kwa unyeyekevu mkubwa, Mwinyi alisema: “Kwa hiyo, Mwalimu, nakuomba mambo matatu. Kwanza naomba radhi mimi nafsi yangu na pia naomba radhi kwa niaba ya askari wote walio wema. Pili, naomba vilevile uelewe sehemu yangu katika kosa hili. Tatu, kwa fedheha hili, naomba unikubalie kujiuzulu.”

Kupatikana kwa barua ya Mwinyi ya kujiuzulu na kuwekwa hadharani inaweka mizania mpya kabisa ya uadilifu katika uwajibikaji wa viongozi wa umma wanapoingia matatani na kutakiwa kujiuzulu.

Miongoni mwa viongozi wakuu waliowahi kujiuzulu katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne, Edward Lowassa, pamoja na mawaziri wawili waliopata kusimamia Wizara ya Nishati na Madini kwa nyakati tofauti za utawala wa awamu hiyo, Dk. Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi.

Viongozi hao, ingawa barua zao za kujiuzulu kwa Rais Jakaya Kikwete hazijapata kuwekwa hadharani, lakini kwa kauli na maelezo yao bungeni wakati wanatangaza kujiuzulu walionyesha kuwa walionewa tu kufikishwa katika hatua hiyo.

Kwa mfano, Lowassa alisema wazi “ameonewa na kudhalilishwa sana” kuhusu suala la mkataba tata wa kuzalisha umeme wa dharura ambao ulitolewa kwa kampuni feki ya Richmond.

Tangu kujiuzulu kwa Lowassa na wenzake wawili, umezuka mpasuko mkubwa miongoni mwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), vita ikipiganwa kuonyesha kwamba kujiuzulu kwa viongozi hao ulikuwa ni uonevu.

Mivutano hiyo ya wabunge ndiyo ilifanya hata Halmashauri Kuu ya CCM kuunda kamati ya wazee watatu wa busara ikiongozwa na Ali Hassan Mwinyi na wajumbe ni Spika wa zamani wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulrahman Kinana na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, kusaka suluhu ya uhasama huo.

Wakati kamati hiyo ikiendelea na kazi ya kusaka suluhu ya uhasama huo, suala la Richmond ambalo ni chimbuko la kujiuzulu kwa viongozi hao watatu, limezidi kuwa tete kila kukicha, zaidi likijitokeza katika makundi ya wapinga ufisadi na wale wanaolezwa kuutetea.

Kwa barua ya Mwinyi ambayo gazeti hili limeamua kuichapisha ilivyo kwa nia ya kuamsha uadilifu unaofanana na kiongozi huyo wa awamu ya pili, ni fursa nzuri sasa kwa viongozi wote wa umma wanaoachia ngazi si tu kukubali kuachia ngazi, ila kuishi maisha yanaoonyesha kwamba hawana kinyongo na hatua waliyochukua.

Mzee Mwinyi kwa maudhui ya barua yake ya mwaka 1977 haikuwa jambo la ajabu kuja kuwa Rais wa Tanzania miaka minane baadaye, huku akionekana kama kiongozi aliyeshinda vishawishi na kila aina ya hila kwenye uongozi wake.

Tags:

0 comments

Post a Comment