Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Noti za zamani ni halali

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT), imekanusha uvumi unaodai kuwa noti za zamani hazitotumika tena, ikisisitiza noti hizo bado ni halali na zitaendelea kuwa katika mzunguko pamoja na noti mpya hadi zitakapochakaa.

Pia benki hiyo imesisitiza kuwa suala la tatizo la noti bandia si tatizo la Tanzania pekee kwani nchi zote duniani zimekundwa na tatizo hilo na zinaendelea kupambana nalo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Uhusiano na Umma na Itifaki kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, wananchi wameshauriwa kuendelea kutumia noti za toleo la zamani bila wasiwasi wowote.

“Benki Kuu inapenda kukanusha habari hizi za kizushi kuwa siyo kweli na kwamba hakuna mpango kama huo na wala hakuna sababu wala uharaka wowote wa kwenda benki kutaka huduma ya kubadilishiwa noti za zamani ili kupata noti mpya,” ilisema taarifa hiyo.

Kuhusu tatizo la noti bandia, BoT ilisema teknolojia ya vinakili vya rangi imefanya udhibiti wa tatizo hilo kuwa mgumu kwa nchi zote duniani.

“Kwa wale wanaofanya uhalifu huu ni vema wakafahamu ni kosa la jinai na wakipatikana watafikishwa mahakamani, hata hivyo noti halisi ikilinganishwa na ya bandia tofauti zake zinaonekana wazi kwa macho na kwa mguso wa aina ya karatasi,” ilisisitiza taarifa hiyo.

Iliwataka Watanzania kuwa makini na kuhakiki uhalali wa noti kwa kuzichunguza kwa makini noti zote wanazopokea kwa kutumia alama za usalama kama zinavyoanishwa kwenye matangazo na vipeperushi vinavyotolewa na Benki Kuu.

Hivi karibuni, kutokana na taarifa za kuwapo kwa noti za bandia kuzagaa, Spika wa Bunge Anne Makinda, alitoa agizo kwa Waziri wa Fedha, kufuatilia suala hilo na kutoa taarifa bungeni.
Tags:

0 comments

Post a Comment