Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo |
ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema viongozi ndani ya Serikali, wamekuwa wakitenda mambo mengi mabaya dhidi ya wananchi na kuficha uozo wao kwa gharama yoyote.Askofu Pengo alisema hayo jana alipokuwa anaongoza Ibada ya Misa kuwaombea watu waliopoteza maisha kwenye milipuko ya mabomu Gongo la Mboto iliyofanika eneo la Hija Pugu, jijini Dar es Salaam.
Kadnali Pengo alisema mambo yanayofanywa na viongozi hao ni pamoja na ufisadi dhidi ya mali za umma na matokeo yake ni serikali kulazimishwa kulipa mabilioni ya fedha kwa Kampuni ya Dowans wakati huduma zinazotolewa kwa wananchi ni hafifu.Alisema sakata la Dowans ni sehemu ndogo kati ya uozo mwingi unaofanywa na vigogo Serikalini na kufichwa pasipo wananchi kuufahamu.Kardinali Pengo alisema imefikia mahali baadhi ya watu wanatenda maovu na kufunga midomo watu na baadhi ya vyombo vya habari na kwamba wako tayari kutoa uhai wa watu wanaodhani ni kikwazo kwao.
Gongo la Mboto
Kadnali Pengo alizungumzia milipuko ya mabomu iliyotokea Gongo la Mboto, kuwa ni ujumbe ambao Mungu alitaka kuutoa kwa Watanzania kuwa hali siyo nzuri na hivyo ni vyema kumrudia yeye (Mungu).
“Kuna weza kusiwe na uhusiano wa moja kwa moja kati ya matukio kama haya na dhambi, lakini bado ujumbe unabaki pale pale, tusiyapuuzie. Kwani watu wa Gongo la Mboto wanadhambi kuliko watu wengine wote wanaoishi Dar es Salaam? La hasha! Tusipotubu nasi tutahangamia vivyo hivyo,” alisema Askofu Pengo.
Akihusisha matukio hayo na baadhi ya matukio yaliyoandikwa katika vitabu vitakatifu, Pengo alisema Nabii Yeremia alitaka kuuliwa kwa sababu tu alitoa unabii ambao siyo mzuri kwa taifa lake.
Alisema wakati huo, watu waliangukiwa na mnara huko Yerusalemu na mfalme alipoletewa unabii juu na tafsiri ya tukio hilo la kuangukiwa na mnara huo, alitaka nabii huyo auawe.
“Viongozi wanapenda tu habari za kuwafurahisha wao na wapambe wao. Wanapenda kusikia tu mambo mazuri hata kama ni ya kipumbavu. Yeremia alivyowaambia ukweli walifanya kila liwezekanalo kumuwa, mpaka wakaenda kumtupa kwenye kisima kilichokuwa na matope,” alieleza Kardinali Pengo:
Aliongeza: “leo Mungu anataka kutufundisha nini Tanzania kwa matukio haya? Siyo mabomu tu, bali hata kutaka kulipa umeme ambao hata hatuupati?, Mabomu na mengine ni mambo tu ya nje. Ni muhimu kwa kila mmoja wetu abadilike ili tuwe salama.”
Kiongozi huyo wa dini alisema ameamua kupasua ukweli hadharani kwa kuwa haogopi watu hao wanaowahujumu Watanzania, kwa sababu ametoa maisha yake kwa ajili ya kueneza neno la Mungu na kukemea maovu na wala haogopi kama watamuua.“Mimi nimesema haya leo, maisha yangu yapo mikononi mwenu, lakini kwa kuwa ni Mungu kanituma nitasema. Mkiniuwa leo au kesho sijali, mkisikia, msiposikia shauri yenu,” alisema akionyesha kukerwa na tabia mbaya ya baadhi ya viongozi wa Serikali akifafanua:
“Mkiniuwa damu yangu iko mikononi mwenu, kwa sababu mtakuwa mmemwaga damu isiyokuwa na hatia. Nasema hivi siyo kuwa naropoka, najua ninachokisema. Kwanini nifungwe mdomo? Nasema haya leo na nyie mkiwa hapa, kama kuna chombo kitakacho kuwa na ujasiri wa kuandika mtaona yatakayotokea.”
Hofu
Kadnali huyo aliyekuwa akizungumza kwa hisia kali, alisema atasema lolote bila kuogopa hata kama vyombo vyote vya habari vikiwemo vya vya kanisa hilo, vitafungwa mdomo ili vifiche wananchi wasifahamu.
Alisema katika kile kinachoonekana ni kufungwa mdomo kwa vyombo vya habari, wiki chache zilizopita wakati wa kusimka Renatus Nkwande kuwa Askofu mpya wa Jimbo jipya la Bunda alisema mambo mengi ya unabii kwa siku za usoni, lakini hayakuandikwa wala kutangazwa chombo chochote cha habari.
Hata hivyo, Kardinali Pengo, hakuweka hadharani mambo hayo ya kinabii aliyoyasema hadharani siku hiyo na kuelezwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Askofu Thadeus Ruwaichi kuwa ni maneno ya kinabii.
Alieleza kwaba kesho yake hakuna chombo cha habari kilichoandika habari hizo kutokana na kile alichosema ni kunyamazishwa.
“Kesho yake baada ya Askofu kusema mambo hayo ambayo ni unabii wa taifa hili, hakuna chombo kilichoandika,” alisema Pengo.Alisema kutokana na viongozi hao kuendelea kuziba watu midomo, sasa Mungu anatumia njia nyinge kufikisha ujumbe ili watu wake waweze kumrudia na kutubu kuokoa taifa lisiangamie.
Hata hivyo, taarifa zilizolifikia gazeti hili kuhusiana na alichosema kiongozi huyo Mkuu wa Kanisa Katoliki nchini wakati akimsimika Askofu mpya wa jimbo la Bunda, aliwataka viongozi wa kanisa hilo kusimama daima katika ukweli hata kama ukweli huo utagharimu maisha yao.Alisema litakuwa kosa kubwa kwa viongozi hao kukubalia kila jambo lililo kinyume na ukweli bila kulitolea neno lolote.
“Simameni daima katika ukweli; liwalo na liwe. Ukiogopa kufa leo utakufa kesho. Ukiogopa kusema ukweli leo eti kwa kuogopa kufa utakufa kesho,” alisema Kadinali Pengo.Kwa mujibu wa Pengo shinikizo linalolisababisha kanisa hilo kutoa wito wa kuwataka watumishi wake wasimame katika ukweli linatokana na hali ilivyo sasa katika jamii ya mgawanyiko miongoni mwa viongozi wa madhehebu ya kidini na watendaji wa serikali.
Kwa mujibu wa Kadinali Pengo, mgawanyiko huo umewafanya watu wanaoitakia nchi mema kushindwa kutimiza jukumu lao ipasavyo wakihofia kukosolewa na kundi jingine lililojijengea tabia ya kuona mapungufu tu hali inayowaumiza wananchi wa kawaida wanaobakia kuteseka kwakushindwa kupata huduma wanazostahili.
“Katika hali hii ni vigumu kwa mtu kutenda mema wala kunuia mazuri, huzuka hali ya kuona mapungufu;hatuoni mema yanayotendwa au kunuiwa na kutendwa na sehemu nyingine,”alisema Pengo kwenye ibada hiyo ya kumsimika Askofu mpya ambayo ilihudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda pamoja viongozi wengine wa vyama vya siasa na serikali.
Kardinali Pengo aliwageukia viongozi wa serikali na kuwataka kushirikiana na wananchi na kusoma alama za nyakati ili waweze kukabiliana na changamoto zilizomo ndani ya kanisa na jamii kwa ujumla kabla ya kuamua chochote.Kauli ya kadinali Pengo iliungwa mkono na Askofu Thadeus Ruwaichi akisema kamwe Kanisa haliwezi kunyamaza bila kuwaambia waamini na watanzania kwa ujumla ukweli juu hali ya mambo ilivyo nchini.
Alitolea mfano suala la umasikini uliokithiri miongoni mwa Watanzania ilihali nchi imejaliwa utajiri wa rasilimali nyingi na kwamba hilo ndilo jambo linalopaswa kuwekwa wazi na Kanisa hilo kwa waaminio na watanzania kwa ujumla ili wazitambue na kuzifanyia kazi kwa maslahi ya wote.
Askofu Ruwaichi alienda mbali zaidi akisema kwamba Kanisa lipo tayari kushirikiana na watu wote ambao wanaitakia mema Tanzania bila kujali imani zao za kidini, itikadi zao za kisiasa, rangi zao wala maeneo wanakotoka ilimradi tu wanaweka maslahi ya taifa mbele.
0 comments