Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Halmashauri Moshi Kufukua Madhambi. Wahofia kuvunjwa Manispaa ya Moshi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WASIWASI umewakumba wakazi wa Manispaa ya Moshi huku wengine wakitabiri kuvunjwa kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kwa kile kinachoelezwa kuwa ni hatua ya baraza la madiwani kujikita zaidi katika kutafuta madhambi ya maamuzi yaliyofanywa na baraza lililopita.

Uchunguzi wa Mwananchi  uliothibitishwa na baadhi ya maofisa usalama umebaini kuwapo kwa msuguano wa chini chini kati ya baraza hilo lenye madiwani wengi wa Chadema na Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi.

Moja kati ya masuala yanayoitikisa halmashauri hiyo ni pamoja na hatua ya madiwani wa Chadema kutaka kurejesha mali zinazodaiwa kuporwa na CCM, suala ambalo limeibua mvutano.

Mali hizo ni kiwanja chenye hati namba 056038/94 cha ukubwa wa futi za mraba 18,790 zilipo ofisi za CCM Moshi mjini na eneo la ekari 2.7 lenye hati namba 15686 linalotumiwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) mkoa.

Tayari madiwani wote 24 wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wanaotokana na Chadema wamewasilisha kizuizi cha kisheria (caveat) ili kuzuia mtu yeyote au taasisi kuhamisha umiliki wa maeneo hayo.

Habari kutoka vyanzo vya kuaminika ndani ya halmashauri hiyo zinadai baadhi ya watendaji wamepoteza morali ya kufanya kazi kwa kile wanachodai kuwa ni hatua ya Madiwani wa Chadema kuamua ‘kutafuta mchawi’.

“Hivi kama Rais Mkapa (Benjamin) alivyoingia madarakani mwaka 1995 angeamua kutafuta madhambi ya mtangulizi wake nchi ingetawalika?...au leo Rais Kikwete atafute madhambi ya Mkapa itakuwaje?”alihoji ofisa mmoja wa halmashauri.

Ofisa huyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe,alidai maamuzi yaliyofanywa na mabaraza yaliyopita yalikuwa ni halali kisheria na haamini Serikali itakaa kimya ikiangalia Madiwani wa Chadema wakibatilisha maamuzi hayo.

“Tukiruhusu kila Chama kinachokuja kibatilishe maamuzi ya mabaraza yaliyopita kwa sababu za kulinda maslahi ya kisiasa ni jambo la hatari sana, Chadema walipaswa kuendeleza yale mazuri si kuendesha siasa za chuki”,alidai.

Wakili mmoja  ambaye alisema si mfuasi wa chama chochote cha siasa, alisema anachokiona siku za usoni ni kwa halmashauri hiyo kuvunjwa na kuundwa tume kama ilivyotokea Jiji la Dar es Salaam wakati wa awamu ya tatu.

“Machi 31 mwaka huu baraza la madiwani litakutana kupitisha azimio la kuwanyang’anya CCM majengo waliyonayo sasa. Je unafikiri serikali ya CCM itakubali?”,alihoji wakili huyo na kusema hiyo litachochea kuvunjwa kwa halmashauri.

Wakili huyo alifafanua kuwa kuna kila dalili manispaa hiyo itaporomoka katika nafasi ya kwanza kitaifa katika suala la usafi kwa kuwa wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga) sasa wanafanya shughuli zao maeneo wanayotaka.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Bernadette Kinabo alipoulizwa na Mwananchi jana kuhusu halmashauri yake kuelekea kuparanganyika alikataa kuzungumza lolote akisema kauli yake inaweza kutafsiriwa tofauti.

Hata hivyo Katibu wa Chadema Mkoa  wa Kilimanjaro, Basil Lema alipoulizwa kuhusu tuhuma za baadhi ya madiwani wake kuendesha siasa za chuki alikanusha na kudai wanachokifanya ni kutekeleza kile walichowaahidi Wananchi.

“Wakati wa kampeni tuliahidi kurejesha mali za umma zilizoporwa na CCM na watu wenye uwezo kifedha yakiwamo maeneo ya wazi na majengo hayo ya CCM na tarehe 31.03.2011 tutatamka rasmi kuyarejesha”alisema Lema.

Katibu huyo alisema wao kama Chadema wanafahamu fika kuwa serikali ya CCM haitakubali hilo litokee na watakachokifanya ni kuivunja halmashauri na kuiweka chini ya Tume na wao Chadema wamejiandaa kwa hilo.
Tags:

0 comments

Post a Comment