Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - TANESCO yapumulia mashine • YAJIPANGA KUNUNUA MITAMBO YA DHARURA

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAKATI hatma ya malipo ya sh bilioni 94 kwa kampuni ya kuzalisha umeme wa dharula ya Dowans iko mikononi mwa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), shirika hilo la umma liko katika hali mbaya kifedha kutokana na kushuka kwa mapato yake.
Hali hiyo imetokana na mgao wa umeme unaoendelea nchini ambao husababisha hasara ya sh bilioni tatu kila mwezi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Felchesmi Mramba, alisema kuwa mgao wa umeme unaoendelea sasa, umetokana na kushuka kwa kina cha maji katika mabwawa yanayozalisha nishati hiyo.
“Mgao wa umeme una athari kubwa kwa shirika na taifa kwa ujumla. Kwa upande wa shirika mapato yake hupungua sana na hivyo kufanya uendeshaji wa shirika kuwa mgumu. Vile vile miundombinu ya umeme huathirika na hivyo kusababisha kukatika katika umeme hata pale ambapo mgao haupo na pia taswira ya shirika kwa jamii huathirika sana,” alisema.
HALI YA UZALISHAJI UMEME KWA SASA
Kwa mujibu wa Mramba, umeme unaozalishwa na shirika hilo kwa sasa na kuingizwa kwenye gridi ya taifa ni megawati 470 badala ya megawati 1006.
Akifafanua hali ya uzalishaji umeme kwa sasa nchini, Mramba alisema mitambo ya maji ina uwezo wa kuzalisha megawati 561, lakini kutokana na kushuka kwa kina cha maji kwenye vyanzo vya umeme, uzalishaji umepungua hadi kufikia megawati 180 tu.
“Mitambo ya gesi na mafuta, ina uwezo wa kuzalisha megawati 445, lakini sasa inazalisha megawati 290. Hii inafanya jumla ya umeme wote unaopatikana kwenye gridi ya taifa kuwa wastani ya megawati 470 tu ambayo ni sawa na asilimia 67 tu ya mahitaji ya wastani ya umeme au asilimia 57 ya mahitaji ya juu katika gridi ya taifa,” alisema Mramba.
Aliendelea kusema kuwa hali hiyo ndiyo inayoleta upungufu wa wastani wa megawati 230 kwenye gridi ya taifa na ndio unaosababisha mgao wa umeme unaoendelea.
“Upungufu huo mkubwa wa maji katika mabwawa yetu umetokana na ukweli kwamba hakukuwa na mvua za kutosha za vuli mwaka jana katika maeneo mengi ya nchi yetu na pia mvua za masika ambayo huanza mapema katika mikoa ya kanda ya kati na kusini magharibi, zimechelewa kuanza,” alisema.
JUHUDI ZA KUTATUA UPUNGUFU HUO.
Akizungumzia juhudi zinazofanywa na serikali kukabili hali hiyo, Mramba alisema tatizo la mgao wa umeme unaoendelea sasa ni la muda kwani linatarajia kumalizika hivi karibuni kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na TANESCO.
Alizitaja juhudi hizo kuwa ni pamoja na kununua mafuta ya ya kuendeshea mtambo wa IPTL ili kuzalisha megawati 80 kwa siku na tayari mafuta hayo yameshanunuliwa na yameanza kuwasili nchini. Hatua hiyo itapunguza mgao wa sasa kwa megawati zipatazo 70.
“Pia tunatarajia kuwa msimu wa mvua za masika, utaanza punde nah ii itafanya uzalishaji umeme katika mitambo ya maji kuongezeka, hivyo kuliondoa tatizo hilo kwa sasa.”
Kwa mujibu wa Mramba, jitihada nyingine ni shirika hilo kuwasiliana na serikali kuangalia uwezekano wa kupata mitambo ya dharura ili kukabiliana na hali inayoweza kujitokeza endapo mvua za masika zitakuwa chini ya wastani.
Alisema, tangu mwaka 2006, juhudi kadhaa zimefanyika ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Alisema juhudi hizo ni pamoja na ujenzi wa mtambo wa megawati 100 wa Ubungo uliokamilika mwaka 2008 na ujenzi wa mtambo wa kuzalisha umeme wa Tegeta wa megawati 45 uliokamilika mwaka 2009.
Kaimu mkurugenzi huyo, alitumia nafasi hiyo kuwaomba radhi wananchi kutokana na usumbufu mkubwa wanaoupata kutokana na adha ya mgao huo.
“Pia shirika linawaomba wananchi kushirikiana nasi na kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha upungufu wa umeme. Tunaahidi kwamba tutafanya kila jitihada kurekebisha upungufu huo,” alisema.
Tags:

0 comments

Post a Comment