Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - TANESCO cna Kamati ya Makamba zazozana vikali

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KAMATI ya Bunge ya Nishati na Madini jana ilichukua zaidi ya saa tano kukutana na uongozi wa Tanesco kujadili na kutafuta ufumbuzi kuhusu mgawo wa umeme unaoendelea, huku taarifa zikionyesha kuwepo mvutano mkubwa baina ya pande hizo na Tanesco kukataa kujadili suala la Dowans.

Hali hiyo inaonyesha kuwa Dowans bado ni kaa la moto kwa Tanesco na Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na January Makamba, ambaye ni mbunge wa Bumbuli.

Awali akizungumza katika utambulisho, Makamba alisema dhumuni la ziara ya kamati yake pamoja na mambo mengine ni kutaka kujua mgawo wa umeme utaisha lini na wao kusaidia mawazo katika kutatua tatizo hilo.

"...Tunataka kujua mgawo wa umeme utaisha lini na utaishaje? Na katika hili muwe wazi na sisi tuweze kusaidia mawazo yetu kuondoa tatizo, pia tujue mnaendeshaje Tanesco, matatizo ili tusaidie kwa manufaa ya Watanzania," alisema Makamba.

Mvutano ndani ya kikao
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa ulizuka mvutano mkubwa baina ya wabunge na viongozi wa Tanesco huku ikielezwa kwamba shirika hilo limeshindwa kutoa kwa kamati hiyo mikakati yake ya kumaliza mgawo wa umeme.

Tanesco pia ilidaiwa kukataa kuzungumzia suala la Dowans nje ya Mahakama na kuwashwa kwa mitambo hiyo ili itoe megawati100 za umeme kwa lengo la kupunguza makali ya mgawo wa umeme unaondelea sasa.

"Mvutano mkubwa humo ndani, moto unawaka, Tanesco hawataki hata kuzungumzia suala la Dowans, mvutano unaendelea. Nimechoka maana huku ni kupoteza muda, hatuelewani ili kutatua tatizo," alisema mmoja wa wabunge ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini na kuongeza:

"Tumeomba mikakati yao (Tanesco) katika kumaliza mgawo wameshindwa, wamesema eti bado ipo katika Bodi yao ya Wakurugenzi".

Tanesco wakaa faragha
Ujumbe wa Tanesco ulitoka nje ya ukumbi wa mkutano saa 8:51 mchana na kufanya kikao cha faragha huku baadhi ya wajumbe wake wakionekana kuhaha kuweka sawa mambo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Makamba alikiri kugawanyika kwa pande hizo, lakini akasema kulifuata kanuni.

"Kutoka nje si tatizo, sisi tumefanya kikao kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, inaruhusiwa na imetokana na mwenendo wa mjadala," Makamba alisema.

Alisema kamati yake imepokea taarifa ya Tanesco na kwamba wao wamejikita katika hatua za dharura.

Kuhusu Dowans, alisema kama taarifa zilizokuwepo, wamiliki wa Dowans walikuwepo nchini na wameanza mazungumzo na Tanesco ambapo mazungumzo na taratibu zinaendelea bila kuathiri kesi iliyo mahakamani ili mitambo hiyo itumike.

Hata hivyo, alikiri kuwapo kwa mvutano katika suala hilo na kwamba kazi ya kamati yake ni kushauri hatua za haraka kumaliza mgawo, pia kuishauri Tanesco waingie biashara ya kuwasha umeme na siyo kuzima.

Alisema Jumatatu ijayo kamati yake itakuwa na taarifa na mapendekezo ya kumaliza mgao wa umeme.

Majumuisho ya Kamati
Jana jioni, Makamba alizungumzia majumuisho ya kikao hicho ambapo alisema kuwa wameihimiza Tanesco waharakishe utekelezaji wa miradi ya umeme.

Miongoni mwa miradi hiyo ni ule wa wa megawati 260 kwa njia ya gesi unaotakiwa kukamilika Juni mwaka huu na mingine ambapo alisema tayari Tanesco imeipa kamati hatua zilizofikiwa na wadau wa miradi husika.

Makamba alisema kazi ya kamati yake sasa ni kuisukuma Serikali itoe fedha haraka kukamilisha miradi iliyopo kwenye hatua nzuri ili iweze kukamilika katika muda  uliopangwa na kuondoa kabisa tatizo la umeme.

Kuhusu Dowans, Makamba alisema Kamati yake imeiagiza Tanesco kuhakikisha hakuna utata wowote wa kisheria na kwamba iwapo wataingia mkataba na kampuni hiyo basi mkataba huo uwe mfupi na usivuke mwezi Juni mwaka huu.


Nafasi za vigogo wazi
Wakati hayo yakiendelea shirika hilo la umma linajipanga kuwabadili wakuu wote wa vitengo vinavyounda menejimenti yake.

Uamuzi huo wa kuifumua Tanesco pamoja na mambo mengine, umekuja kipindi ambacho shirika hilo limepigwa mawimbi mazito huku wimbi la Dowans, likionekana kutikisa zaidi.

Katika tangazo lake lililotolewa jana kwenye vyombo vya habari, lenye Kichwa cha habari, '' Ajira kwa Nafasi Nyeti za Uongozi,'' Tanesco imeweka bayana kuwa nafasi zote za wakuu wa vitengo ziko wazi na zinahitaji kujazwa.

Nafasi hizo ni pamoja na Meneja Rasilimali Watu, Mkuu wa Kitengo cha Fedha, Meneja Mwandamizi wa Mipango Mikakati, Meneja Mwandamizi wa Utafiti na Meneja Mwandamizi wa Miradi.

Nafasi zingine zilizotangazwa katika tangazo hilo ni Meneja Mwandamizi wa Uangalizi wa Mfumo na  Meneja Mwandamizi Mfumo wa Usambazaji.

Zingine ni Meneja wa Uzalishaji Umeme kwa kutumia Maji, Meneja Mwandamizi Uzalishaji Nishati na  Meneja wa Mauzo na Masoko.

Pia anatafutwa mtu wa kujaza nafasi ya Meneja Mwandamizi Usambazaji, na nafasi ya Meneja Uhusiano wa shirika hilo.Mwisho wa kutuma maombi ya kujaza nafasi hizo ni Machi 8, mwaka huu 2011.
    
Tanesco imekuwa ikitajwa kukabiliwa na matatizo ya menejimenti kwa muda mrefu, hali inayotajwa kama moja ya chanzo cha kuzorota kwa utendaji wa shirika hilo nyeti la umma.

Matatizo mengine yanayoikabili Tanesco ni mikataba mibovu kama ule ulioingiwa kati yake na Richmond ambao baadaye ulirithiwa na Dowans Tanzania Ltd, ambayo sasa inaidai Tanesco Sh94 bilioni kwa kukatisha mkataba kinyume cha taratibu.

Jana Makamba alisema ukaimu wa nafasi mbalimbali ndani ya Shirika hilo kuwa moja ya tatizo la kiutendaji linaloliyumbisha.Makamba alitoa kauli hiyo katika utambulisho wakati kamati yake ilipofanya ziara Makao Makuu ya Tanesco, Ubungo Dar es Salaam."Kaimu wengi, inawezekana hili ni moja ya matatizo,"alisema Makamba.

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Nishati na Madini, alijikuta akitoa kauli hiyo ghafla baada ya mkurugenzi wa Tanesco, William Mhando, kujitambulisha na kutoa nafasi kwa ujumbe wake kujitambulisha.

Katika utambulisho huo zaidi ya nusu ya wakuu wa idara na vitengo vya Tanesco, walijitambulisha kuwa ni makaimu.
Tags:

0 comments

Post a Comment