Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mawaziri waendelea kumkimbia Gaddafi, Watanzania Libya walalamika

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WASHIRIKA wa kiongozi wa Libya anayekabiliwa na maandamano ya umma kumtaka aondoke madarakani wameanza kumpa kisogo, kufuatia baadhi ya mawaziri wake na wanadiplomasia waliokuwa wakimwakilisha nje ya nchi, kutangaza kuunga mkono umma unaompinga.

Mawaziri walioachia ngazi ni Waziri wa  Mambo ya Ndani, Abdul Fattah Yones na Waziri wa Sheria, Mustafa Abdul Jalil.

Yones alitangaza kujiuzulu na kujiunga na waandamanaji, ambao alisema wana madai ya haki, huku akieleza kusikitishwa kwake na mauaji ya raia.

"Mimi kuanzia sasa sio Waziri wa Mambo ya Ndani tena, bali mwanajeshi ninayesimama upande wa umma," alisema Yones katika tangazo lake la kujitoa kwenye Serikali iliyoko mashakani ya Gaddafi.

Katika mahojiano ya baadaye na kituo cha televisheni cha Al-Arabiya, Younis alisema kwamba mfuasi mmoja wa Gaddafi, alijaribu kumuua, lakini risasi ilimkosa na kumjeruhi jamaa yake.

Katika hotuba yake ndefu aliyoitoa usiku wa kuamkia jana, ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanza kwa maandamano dhidi ya Serikali yake, Gaddafi ambaye anajaribu kuendelea kutetea utawala wake wa zaidi ya miongo minne, alisema waandamanaji walikuwa wamemuua Waziri huyo wa Mambo ya Ndani.

Mshirika mwingine wa karibu wa Gaddafi ambaye alitangaza kujiuzulu na kuwaunga mkono waandamanaji, ni Youssef Sawani, aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa wakfu wa mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islam, akisema amechukua uamuzi huo kupingana na mashambulizi dhidi ya raia.

Sawani alikaririwa na Reuters akisema kwamba amejiuzulu nafasi hiyo kwa kuwa hakubaliani na hatua za Serikali ya baba wa bosi wake, inavyowakandamiza waandamanaji.

Maofisa wengine waliojiuzulu ni wawakilishi wa Libya katika balozi nchini Australia, China, India na Malaysia na balozi mdogo wa Libya katika Umoja wa Mataifa (UN), Ibrahim Dabbash.

Hao walitangaza kujitenga na Serikali ya Gaddafi  juzi, wakieleza kwamba Serikali hiyo imepoteza uhalali wake mbele ya umma wa Libya.

Pia balozi wa Libya nchini India, Ali al-Essawi aliliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP mjini New Delhi kwamba anajiuzulu kwa sababu ya mauaji makubwa ya raia wasiokuwa na hatia nchini mwake.

Jumuiya ya Kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia wameshutumu vikali matumizi ya nguvu dhidi ya raia nchini Libya, na kutoa wito kwa wale wanaohusika katika uovu huo, kuwajibika kwa makosa yao.

Taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo ya dharura mjini New York yaliyofanyika juzi, imetaka kukomeshwa kwa vurugu hizo mara moja na kutoa wito kwa maofisa kushugulikia malalamishi ya wananchi wa Libya.

Lawama hizo kwa Gaddafi zimetolewa na Italia wakati akiwa ameagiza wafuasi wake kuingia mitaani na kusafisha mitaa kwa kuwaondoa waandamanaji wanaomtaka aondoke madarakani.

Taarifa zilieleza jana kuwa baadhi ya miji tayari iko chini ya udhibiti wa waandamanaji na baadhi ya askari wa jeshi la nchi hiyo wametangaza kutokuwa watiifu kwa Gaddafi.

Mawaziri wa Mambo ya Ndani wa Italia, Cyprus, Ufaransa, Ugiriki, Malta na Hispania wanakutana mjini Roma, Italia kuweka sera ya pamoja, wakati ambapo eneo la kaskazini mwa Afrika, likishuhudia mageuzi.

Mawaziri hao watatoa mapendekezo yao kwa kamisheni ya Umoja wa Ulaya.

Watanzania hawana habari
Wakati huo huo wakati hali ya kisiasa nchini Libya ikizidi kuwa mbaya, Serikali ya Tanzania haijaandaa mpango wa kuwasaidia wananchi wake wanaoishi nchini humo, Mwananchi imeelezwa.

Baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Libya walilieleza gazeti hili jana kuwa hawajapata maelekezo yoyote kutoka Serikali ya Tanzania tangu kuanza kwa machafuko hayo wiki iliyopita

"Kwanza Tanzania haina ubalozi nchini Libya, lakini pia hakuna taarifa yoyote kutoka nchini kwetu (Tanzania) inayotuelekeza nini tufanye katika hali kama hii," alisema Ali Said Juma.

Hata hivyo, Juma ambaye ni mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Kiislamu nchini humo, alisema Watanzania wote hasa wanafunzi wako salama kwa kuwa machafuko hayo hayajafika vyuoni.

"Sisi hapa chuoni hakuna shida kubwa. Mambo bado sio mabaya sana. Lakini hatujapata maelekezo yoyote kutoka Serikali ya Tanzania kuhusu hali hii ingawa wenzetu wa Uganda wameelekezwa cha kufanya," alisema Juma

Kwa mujibu wa Juma, ingawa sasa hakuna mahitaji makubwa ya msaada wa Serikali, inapaswa kujipanga katika kutoa misaada hiyo kama itahitajika badala ya kuwa kimya kana kwamba hakuna jambo lolote limetokea nchini humo.
Tags:

0 comments

Post a Comment