Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Makamba atoboa siri ya mgawo. Dowans yapendekeza kuisamehe TANESCO deni la Bil. 94/=

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
•  DOWANS YAWEKEWA NGUMU TANESCO, LHRC



IMEBAINIKA kuwa makali ya mgawo wa umeme yamekuwa yakichangiwa na serikali kushindwa kutoa mafuta ya kuzalishia umeme katika mtambo wa IPTL.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini na Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba (CCM) alisema kuwa kukosekana kwa mafuta hayo kumesababisha mtambo huo kuzalisha chini ya kiwango.
Alisema serikali kupitia hazina haina budi kutoa fedha kwa ajili ya kuagiza mafuta ya kuzalishia umeme ili kuwezesha mtambo huo kuzalisha megawati 100 ili kupunguza tatizo la mgawo wa umeme.
Makamba alisema kupatikana mafuta kidogo kumesababisha IPTL kwa sasa kuzalisha kati ya megawati 10 mpaka 50 zinazopelekwa katika gridi ya taifa kwa siku.
“Kuna mafuta yapo eneo la Kurasini ambapo yanahitajika kubebwa na kusafirishwa hadi katika mitambo hiyo …bado Hazina inahitajika kuhakikisha inatoa fedha kwa ajili ya kupata mafuta ili mitambo hiyo iweze kuzalisha megawati 100,” alisema.
Alisema kutokana na serikali kushindwa kutoa mafuta kwa kiwango halisi mitambo hiyo ya IPTL imeshindwa kuzalisha umeme ambao ungesaidia kupunguza tatizo lililopo sasa.
Makamba alisema kwa mwezi mitambo hiyo inatumia mita za ujazo elfu 15 ambapo hadi kufikia juzi ilizalisha megawati zipatazo 50.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo alisema walikutana na wadau mbalimbali wa masuala ya gesi ambapo pamoja na majadiliano bado kamati hiyo imeombwa kupatiwa taarifa za bei ya gesi kwa maandishi ili kuweza kulitazama suala hilo kwa upana zaidi.
Alisema ni kweli wadau hao walikiri kuuza gesi hiyo kwa dola za Marekani lakini kamati imehitaji kupatiwa taarifa hiyo kwa maandishi.
Makamba alisema walijadili pia tatizo lililojitokeza ambapo kuna mashaka na mtambo wa bomba la kusafisha na kusafirisha gesi inayodaiwa kuwa imefikia mwisho wa uwezo wake.
“Tumeliangalia pia tatizo lililojitokeza la kuwepo kwa matatizo katika mtambo wa bomba la gesi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ambapo kwa hivi sasa kuna viwanda kama vitatu vikubwa vinavyotumia gesi kuzalisha umeme,” alisema.
Alisema pia mitambo ya mabomba hayo ilijengwa miaka 15 iliyopita na mahitaji ya gesi yameongezeka hivyo wamejitahidi kuliangalia hilo na wadau wote na taarifa yote itatolewa wiki ijayo.
Wakati huo huo, siku moja baada ya kampuni ya Dowans Tanzania Limited, kutangaza kuwa iko tayari kusamehe deni la sh bilioni 94 kadhalika kukiwa na msukumo wa kulitaka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuingia mkataba nao ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme, hatua hiyo imeonekana kutiliwa shaka.
Hivyo TANESCO imesema inahitaji kutafakari juu ya hatua hiyo ya Dowans kuwafutia deni kwani jambo hilo ni la kisheria na si la makubaliano ya kawaida.
Uamuzi wa Dowans kuifutia deni TANESCO, ulitangazwa juzi na Mkurugenzi wa Fedha wa Kampuni hiyo, Stanley Munai, ambaye alisema kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kusikia kilio cha Watanzania, lakini TANESCO imeshindwa kuitikia wito huo wa kusamehewa.
Akizungumza na Tanzania Daima, kuhusu kauli hiyo ya Dowans, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Wiliam Mhando, alisema ni muhimu kwa sasa kuzingatia masuala ya kisheria kuliko kukurupuka na kuonekana wao ndio waliovunja sheria na kusababisha kuibuka kwa mjadala mpya.
“Hili suala linazungumzika lakini kinachosababisha haya ni kauli za kisiasa, jambo la kisheria huenda kisheria ni muhimu kwanza tukae na timu yetu ya wataalamu kuliko kukubali na kukurupuka, ni mchakato kufikia makubaliano nao na tunahitaji ufafanuzi wa kina,” alisema Mhando.
Juzi, Munai alisema kuwa licha ya kutoa msamaha huo, TANESCO bado walishindwa kujibu kama imeukubali au la ili mazungumzo yaanze.
Akifafanua zaidi kuhusu ombi la Dowans kutaka kukutana na TANESCO, Mhando aliwataka Watanzania kuvuta subira ili kuona juhudi zinazofanywa na TANESCO katika kukabiliana na hali ya mgao wa umeme nchini na hata kuondokana nao kabisa.
Dowans ilishinda kesi dhidi ya TANESCO katika Mahakama ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC), na hivyo kuamriwa ilipwe shilingi bilioni 94, uamuzi ambao ulizusha malumbano makubwa nchini na kusababisha Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu Nchini (LHRC)
kuwasilisha pingamizi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, kupinga usajili wa tuzo iliyotolewa na Mahakama ya ICC.

Hata hivyo, uamuzi wa Dowans kutaka kuifutia deni TANESCO haujaweza kubadilisha mawazo ya LHRC ambao wameapa kuendelea na msimamo wao mahakamani.
Tanzania Daima iliwasiliana na mkurugenzi mkuu wa kituo cha sheria na haki za binaadamu nchini (LHRC), Francis Kiwanga, kuhusu uamuzi wa kuendelea na kesi hiyo au la, alisema ni vizuri mahakama ikaheshimiwa kwani ndicho chombo muhimu katika kusimamia na kutafsiri sheria.
“Kimsingi hebu tuheshimu mahakama suala la kufuta kesi au vinginevyo mahakama ndiyo yenye uwezo wa kuamua lakini sisi bado tutaendelea na kesi yetu ya msingi,” alisema Kiwanga.
Januari mwaka huu kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na wanaharakati wa haki za kijinsia nchini waliwasilisha pingamizi Mahakama Kuu kupinga serikali kuilipa kampuni ya Dowans sh bil. 94.
Mahakama hiyo ya kimataifa ilikuwa imesikiliza malalamiko ya Dowans dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kuamua iilipe fidia kampuni hiyo baada ya kubaini kuwa ilivunja mkataba kinyume cha taratibu.
Hata hivyo Februari 22, mwaka huu, Mahakama Kuu ya Tanzania ilipokea na kusajili kesi nyingine ya kikatiba kupinga malipo ya kampuni ya umeme ya Dowans.
Kesi hiyo ya kikatiba ilifunguliwa mahakamani hapo na Watanzania saba wakiwemo wabunge watatu na kupewa namba tano ya mwaka 2011 chini ya Kampuni ya Mawakili ya Mpoki na Lukwaro.
Msingi wa kesi hiyo ni kwamba malipo ya Dowans ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 sehemu ya tatu kifungu cha 27 Ibara ya kwanza na ya pili. Hivyo katika kesi hiyo Watanzania hao wanaiomba Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa malipo hayo kwa kuwa yanakwenda kinyume na katiba ya nchi.
Hali kadhalika, deni ambalo Dowans wanaidai TANESCO hivi sasa limeongezeka na kufikia sh bilioni 99 badala ya sh bilioni 94 za mwaka jana.
Kwa mujibu wa maelezo ya Dowans wenyewe, ongozeko hilo linatokana na kampuni ya Dowans kuitoza TANESCO kila siku Dola za Marekani 11,800 (ambazo ni sawa na sh milioni 15.3) kama gharama za uzalishaji umeme ambapo nyongeza hiyo ilianza kutozwa kila siku tangu Januari 15, mwaka 2010 hadi sasa.
Tags:

0 comments

Post a Comment