Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kikwete ashitukia maandamano, migomo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
RAIS Jakaya Kikwete amesema amegundua kuwapo njama za makusudi za kudhoofisha Serikali yake ionekane haifanyi kitu.

Alisema hayo katika hotuba yake ya kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM yaliyofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

“Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka 2010, nilidokeza taarifa ambazo vyombo vya usalama vinazo, kuhusu mipango ya makusudi ya uvunjifu wa amani kwa kutumia njia ya migomo na maandamano,” alisema Rais.

Kauli hiyo imekuja huku kukiwa na maandamano na migomo katika taasisi mbalimbali hususan za elimu ya juu nchini. Alisema aliwatanabaisha wananchi kutambua njama hizo na kuepuka kushiriki maandamano au migomo ya aina hiyo.

“Wanaoandaa wana ajenda yao ya kisiasa iliyojificha nyuma ya jambo linalotangulizwa kama sababu. Wanataka kujitengenezea mazingira ya ushindi mwaka 2015 kwa vurugu,” alisema.

Rais alisema anakumbuka alihadharisha watu wajiepushe kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa kuendeleza maslahi ya kisiasa ya watu fulani fulani.

“Niliyoyasema yametokea Arusha na dalili zipo za mipango ya namna ile kuandaliwa kutokea sehemu nyingine nchini. Napenda kurudia kuwasihi Watanzania wenzangu msiwasikilize wala kuwafuata wanasiasa hao.

“Wanawasakizia kwenye hatari ambayo mnaweza kuiepuka. Naomba muwakumbushe tena, kuwa wanayo fursa bungeni na kwenye majukwaa mbalimbali kutoa hoja zao, badala ya kuwagombanisha ninyi na vyombo vya Dola,” aliongeza.

Aliwataka wanasiasa wenzake kutumia fursa tele walizonazo badala ya njia ya uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha na mali za watu na kuharibu sifa ya Tanzania.

Hivi karibuni, viongozi na wafuasi wa Chadema, walifanya maandamano haramu mkoani Arusha na kukabiliana na polisi walipotaka kuvamia kituo cha Polisi cha Arusha, ili kuwatoa wenzao waliokuwa wamekamatwa.

Katika purukushani hiyo, wafuasi wao wawili na raia mmoja wa Kenya waliuawa na viongozi wa chama hicho hivi sasa wanakabiliwa na kesi mahakamani ya kutotii amri halali ya Jeshi la Polisi.

Juzi, wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dar es Salaam na Ardhi, walijaribu kuandamana kwenda Ikulu kumwona Rais Kikwete kushinikiza Serikali iwaongeze fedha za kujikimu, lakini maandamano hayo yasiyo na kibali pia yalivunjwa na polisi.

Katika vurugu hizo wanafunzi wawili walijeruhiwa na mmoja kutoka mimba.
Tags:

0 comments

Post a Comment