Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wananchi wang'ang'ania wakabidhiwe polisi aliyeua

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SAKATA la polisi kuua raia  kwa risasi katika kata ya Ubaruku Wilaya ya Mbarali Mkoani Mbeya limeingia katika sura Mpya baada ya wananchi kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo Kanali Kosmas  Kayombo kumkamata na kumpeleka kwao askari polisi aliyemuua mwenzao kwa risasi, ili wamchukulie hatua za kisheria.

Wakizungumza kwenye mkutano na mkuu huyo wa wilaya jana, wanachi hao walisema kitendo alichokifanya askari huyo ni cha kinyama na haawamini kwamba kingeweza kufanywa na mtu kama huyo ambaye kazi yake ni kulinda usalama wa raia na mali zao.


Walimtahadharisha Mkuu huyo wa Wilaya kuwa endapo kama hatua hazitachukuliwa haraka ikiwa ni pamoja na kuwadhibiti wanaochochea uhasama wa kuwanyima haki wananchi, hali inaweza ikizidi kuwa mbaya kwa sababu wengi wao wana hasira.

Walidai kwamba baadhi ya viongozi wa wa serikali ngazi ya wilaya pamoja na baadhi ya polisi, ndiyo chanzo cha vurugu hizo zilizosababisha mauaji ya mtu mmoja.

Wakielezea jinsi mwezao alivyouawa, walisema kuwa aliyeuawa alikuwa akibiashana na polisi na baada ya mvutano ndipo alipochukua bunduki  na kumpiga risasi kwenye paji la uso.

Walimweleza mkuu huyo wa wilaya kwamba tukio hilo liliwafanya wananchi wapandwe na hasira na kuanza kurusha mawe na polisi kurusha mabomu ya machozi na risasi za moto ambapo mwananchi mmoja alipigwa risasi kiunoni.

Majeruhi huyo ambaye risasi ilipenya kiunoni  kwa nyuma na kutokezea mbele, Hassan Masila, amelazwa katika  hospitali ya Wilaya ya Mbarali kwa matibabu.

Hassan aliliambia Mwananchi kuwa "nilipigwa risasi wakati nikikimbia baada ya kuona mwenzetu mmoja  kauwawa kwa risasi".

Wananchi hao walionekana kujawa na jazba kwenye mkutano huo ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya, na kupaaza sauti zao huku wakipiga kelele kiasi cha kufanya kutokuwepo kusikilizana.

Hali hiyo ilimpa wakati mgumu Mkuu wa Wilaya na kumfanya mbunge wa jimbo hilo Dickson Kilufi na Diwani wa kata ya Ubaruku George Mbila  kunyanyuka na kufanya kazi ya kuwatuliza na kuwasihi wapunguze jazba.

“Tunakuambia Mkuu sisi tunataka shamba letu na huyo polisi aliyefanya mauaji kwa sababu tunamfahamu. Nyie serikai ndiyo mmechangia haya mauaji kwani mmekuwa mkitunyanyasa sisi weusi na kuwapendelea weupe. Sasa tunasema tumechoka, tupo tayari kufa kwa lolote hivyo tunalitaka shamba letu na huyo polisi aliyeua,” walilalamika.

Shamba hilo ni moja kati ya yale yaliyokuwa yakimilikiwa na serikali wilayani Mbarali ambayo wamepewa wawekezaji mbalimbali.

Mkuu huyo wa Wilaya alipata nafasi finyu ya kuzungumza na wananchi hao ambapo alisema kuwa malalamiko yao ameyachukua na atakwenda kuyafanyia kazi.

Alisema serikali tayari imeruihusu magari ya aina yoyote kuingia Wilayani humo kauli ambayo hata hivyo wananchi waliendelea kupaza sauti zao za kumataka Mkuu huyo atoe kauli ya mwisho ya mkumuondoa Mwekezaji huyo.

Akizungumzia tukio hilo kwa ujumla Mbunge Kilufi alisema wananchi wa Ubaruku wana kero kubwa mbili ikiwa ni pamoja na polisi kuzuia magari  makubwa yasichukue mazao yao na kupeleka katika masoko ya nje na nadani ya nchi.

Kero nyingine akasema ni mwekezaji  mmoja kung'ang'ania mashamba yaliyopo nje ya shamba alilokabidhiwa na serikali, huku akionekana kulindwa na baadhi ya watendaji serikalini.

Alisema kuwa vurugu hizo ni matokeo ya baadhi ya watendaji wa serikali  kutokuwa makini na kutosikiliza ushauri ambao wanapewa kabla ya kutokea matukio ya hatari na badala yake kusikiliza maneno ya watu wachache kwa masilahi yao binafsi.

Kilufi alisema awali alimhoji Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) kuwa nani ametoa kibali cha kuzuia magari makubwa yasiingie kubeba mazao ya wakulima ambapo alijibu kuwa, amepewa amri kutoka kwa wakubwa.

“Baada ya kupata majibu hayo nilikwenda kwa mkuu wa Wilaya na kuuliza kama kuna barua yoyote  yenye tamko la ambayo inaeleza kuzuia magari hayo.

"Lakini naye alinijibu kuwa hakuna barua yoyote na ndipo tilipomdhirishia Mkuu wa Mkoa wa Mbeya John Mwakipesile ambapo aliruhusu kwa siku saba magari hayo uandelee kuingia Wilayani humo ambapo baada ya kupita siku hizo polisi walianza tena kuzuia magari hayo,” alisema Kilufi.

Alifafanua kuwa hadi kufikia juzi, akiwa njiani akitokea nyumbani alifika njia panda ya Madibira na Rujewa ambapo alikuta lori la kubeba mafuta likiwa limezuiwa na Askari mmoja wa usalama barabarani ambaye alimshirikisha mbunge huyo kwa kumwambia kuwa gari hilo lilikotoka kwani haliruhusiwi kuingia huko.

“Yule Askari alivyonieleza hivyo nami nikamueleza kuwa asiende na gari lake huko kwani wananchi hawatakubali kutokana na kuwa wiki iliyopita walilizuia gari la mwekezaji lililokuwa limebeba kokoto," alisema Kilufi na kuongeza.

"Mimi niliwasihi waliache lakini dereva huyo alisema yeye ameruhusiwa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) basi mimi nikaendelea na safari yangu,” alisema

Mbunge huyo aliendelea kufafanua kuwa akiwa mjini alipigiwa simu kuwa kuna vurugu zimetokea Ubaruku ambapo alirudi na kukutana na yule askari na kumhoji  sababu za kuruhusu gari hilo liondoke na kwamba alimjibu kuwa ni OCD.

“Magari ya kubeba mazao yetu yanakataliwa kuingia lakini haya ya wenzetu (wawekezaji) yanaruhusiwa hivyo sisi kama wananchi tulikuwa tunamuhitaji OCD na Mkuu wa wilaya wafafanue kuhusu hali hiyo.

"Lakini polisi wao walivyokuja hawakutaka kutusikiliza na badala yake wakawa wanalitaka hilo gari liondoke hapo na sisi wananchi hatukutaka na ndipo mabishano yalipoanzia hapo,” alisema mmoja  aliyejitambulisha kwa jina John Mwambuku
Tags:

0 comments

Post a Comment