Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Vijana wa Chadema wataka maandamano nchi nzima

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
SIKU chache baada ya kutokea vurugu huko Arusha na kugharimu maisha ya watu na uharibifu wa mali, Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limekiomba chama hicho taifa kutangaza maandamano ya nchi nzima kupinga na kudai mambo mbalimbali kwa maslahi ya umma.
“Tunakiomba Chadema taifa kitoe tamko zito ili kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa kwa wote waliohusika na pia uchaguzi huo wa Arusha unarudiwa,” alisema Katibu wa Kamati ya Taifa wa Bavicha, Ally Chitanda katika taarifa yao kwa vyombo vya habari.

Chitanda aliongeza kuwa, “Sisi tuko tayari kushajihisha vijana nchini kushiriki katika maandamano yatayoitishwa na chama nchi nzima, kwa ajili ya suala hili na kuunganisha nguvu ya umma katika mambo mengine yanayoligusa taifa,” alisema Chitanda.

Aliyataja mambo hayo kuwa ni kupandishwa kwa bei ya umeme, jaribio la kutaka kuilipa kifisadi kampuni ya Dowans, maslahi ya wanafunzi na madai ya katiba mpya.

Baraza la Vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) taifa limelitupia lawama jeshi la polisi nchini kwamba limefanya vurugu na mauaji mjini Arusha kwa maelekezo ya serikali ya CCM, chini ya mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.

Wakati huohuo Bavicha ililaani  mauaji na vurugu za  Arusha sambamba na kueleza kusikitishwa kwao na tamko la Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) kwa vyombo vya habari lenye mwelekeo kuunga mkono vitendo vya mauji na vurugu hizo.

Chitanda alisema hajashangazwa na kauli hiyo ya UVCCM kwa kuwa lilitolewa na Ridhwan Kikwete ambaye pia ni mtoto wa Rais Kikwete.

“Vurugu na mauji hayo yamefanywa kwa ajili ya manufaa ya CCM na kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Kikwete katika hotuba yake kwa taifa Desemba 31 mwaka jana,” alituhumu Chitanda.

Chitanda alisema Rais Kikwete alionyesha kukwerwa na migomo na maandamano yanayofanywa na vyama vya siasa na wadau wengine nchini kupinga au kudai mambo mbalimbali.

Rais Kikwete aliyasema hayo siku chache baada ya vijana wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kufanya maandamano ya kudai haki zao za msingi, Chadema na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) nao kutangaza maandamano ya kupinga matokeo ya umeya Arusha na  ongezeko la bei ya umeme.

“Hivyo UVCCM wametoa tamko kwa lengo la kukisafisha chama chao na mwenyikiti wao wa taifa ambaye pia ni mzazi wa mmoja wa waliotoa tamko hilo,” alisema Chitanda na kuongeza:

“Hata hivyo imetulazimu kutoa tamko kutokana na lugha ya utovu wa maadili waliyoitumia ambayo imepingana na kauli za viongozi wa dini ambao wametoa kauli za wazi za kukemea matukio ya Arusha yaliyofanywa na jeshi la polisi.”

Chitanda alisema wamefadhaishwa na UVCCM kuupotosha umma wa Watanzania kwa kueleza kuwa, viongozi wa Chadema wamefanya vurugu wakati ushahidi unaonyesha wazi kwamba polisi kwa manufaa ya CCM ndio waliofanya vurugu hizo.

“Ushahidi wa mikanda mbalimbali ya vituo vya ndani ya nchi yetu vya televisheni umeonyesha wazi kuwa, polisi walikuwa wakiharibu mali kwa kuvunja vioo vya magari na lipo jengo lililochomwa moto kutokana na kutupiwa bomu la machozi,” alisema Chitanda.

Alisema Bavicha inafahamu kuwa viongozi wa Chadema hawafanyi maandamano kujitafutia umaarufu kama ambavyo UVCCM imewatuhumu kwenye tamko lao; bali wanatimiza wajibu wa kidemokrasia wa kudai haki na kutetea maendeleo kwa kutumia nguvu ya umma. 
Tags:

0 comments

Post a Comment