Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Membe: Polisi walikiuka maadili mauaji Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema Jeshi la Polisi lilikiuka maadili ya kazi yao, lilipokuwa likikabiliana na raia waliokuwa wakiandamana kupinga suala la uteuzi wa meya wa Arusha.Waziri Membe aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusiana na vurugu zilizozuka baada ya polisi kukabiliana na wafuasi wa Chadema waliokuwa wanaandamana jijini Arusha wiki iliyopita na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine zaidi ya 20 kujeruhiwa kwa risasi za moto. 

 “Jeshi la Polisi linatakiwa kufanya kazi kwa mipaka ili kuhakikisha kuwa linadumisha amani nchini,” alisema Membe akielezea kuwa ni maoni yake binafsi kuhusiana na tukio hilo linaloelekea kuliwekea doa Tanzania ambayo inajulikana kuwa ni kisiwa cha amani.
 
Vurugu hizo zilitokana na Chadema kuamua kuandamana kwa amani licha ya kuwepo na amri ya polisi iliyokuwa inawazuia wakishinikiza uchaguzi wa  Meya wa jiji la  Arusha urudiwe kwa sababu kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu zilizomsimika Gaudence Lyimo  wa CCM kwenye madaraka hayo.  Membe alisema kuwa mabalozi wa nchi mbalimbali hapa nchini walimbana wakitaka Serikali iweke wazi suala la mauaji hayo ili dunia ifahamu ukweli badala ya tetesi.  

“( Wamenibana (mabalozi) kweli kweli ili Serikali itoe tamko rasmi… Nimewajibu kwamba ndani ya wiki hii Serikali itatoa tamko kwa kuwa nayo haijafurahia mauaji hayo,” alisema Membe.  Aliongeza kuwa waliokufa katika tukio hilo ni Watanzania hivyo bila kujali itikadi ya chama, msiba huo ni wa kitaifa.  

“Natoa pole kwa wafiwa wote ambao wamepoteza ndugu na rafiki kutokana na tukio lile, pia na wale waliolazwa hospitali, nawatakia kila la kheri wapone na kuendelea na shughuli zao kama kawaida,” alisema Membe.  

Membe alisema kuwa jana alikutana na mabalozi hao kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine walijadili kuhusu tukio hilo la mauaji yaliyofanywa na polisi kwenye maandamano hayo ya wafuasi wa Chadema, Januari 5, mwaka huu.  Habari za ndani ya kikao hicho ambazo gazeti hili lilizipata zilieleza kwamba  mabalozi hao walilituhumu  Jeshi la Polisi wakisema kuwa halikutenda haki kwa sababu waandamanaji hawakuwa na silaha na walikuwa wakiandamana kwa amani.

 Walipendekeza pia kuwa ni vyema jeshi hilo likapatiwa mafunzo ya kukabili maandamano ili kujua ni wakati gani wa kutumia silaha za moto, mabomu ya machozi au vifaa vingine vya kutuliza ghasia.

 Chanzo hicho kilieleza kwamba kauli za mabalozi hao kwa kiasi kikubwa zinaweza kuwa zimechangiwa na msimamo wa CCM na Chadema.  Makatibu wa vyama vyote wamesikika wakikebehi kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsa Vuai Nahodha ya kusema tatizo hilo la Arusha ni la kisiasa hivyo linapaswa kutatuliwa kisiasa kwa vyama vyote viwili kukutana na kumaliza tofauti zao.  

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk  Slaa alisema hawawezi kukaa na CCM kwa kuwa chama hicho na Serikali yake ni katili na ya kihuni.  Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba akasema hawezi kukutana na Chadema kwa sababu suala la meya wa Arusha liko nje ya uwezo wa vyama hivyo viwili.  

Makmba alisema kwamba uchaguzi wa meya ulisimamiwa na Serikali na kwamba wao CCM kama ilivyo Chadema, walichofanya ni kupeleka jina la mtu wanayeona anafaa.  Makamba alifafanua zaidi kuwa kulingana na taratibu, meya huyo wa CCM alichaguliwa kihalali na kwamba kama kuna aliye na malalamiko anapaswa kufungua kesi mahakamani. 

Wakati mabalozi wakitoa maoni yao tayari  maaskofu wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha wameshatangaza kutomtambua meya  huyo wa CCM na kwamba hawatampa ushirikiano.
  Kutokana na mazingira hayo ya kuwepo kwa watu waliopoteza maisha na hata shutuma hizo za viongozi wa dini, aliyechaguliwa Naibu Meya, Michael Kivuyo wa TLP, alitangaza kujiuzulu kwenye nafasi hiyo. 
 
Hata hivyo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameingilia kati sakata hilo kwa kukutana na  Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema na Nahodha. Vilevile, Pinda anatarajiwa kukutana na viongozi wa Chadema.
Tags:

0 comments

Post a Comment