Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Vifo vya Mapadri Utata mtupu

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Na Rhobi Chacha
Vifo vya mapadri  wawili waliofariki Januari 12, mwaka huu  ufukweni mwa Bahari ya Hindi eneo la Kasa Beach Kigamboni jijini Dar es Salaam vimedaiwa kuwa na utata baada ya viongozi hao wa dini kufariki katika mazingira ya kutatanisha.

Akizungumza na mwandishi wetu mwishoni mwa wiki iliyopita katika Ofisi ya Benedictine Farthers iliyopo Kurasini Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Habari wa Ndanda, Father  Abate  alisema kuwa, Padri John Rockslon (59), raia wa Ujerumani na mwenzake walikufa kifo cha kutatanisha.
Alisema, marehemu alikuwa Mhasibu katika ofisi yao na Padri Alen Maxime (35), raia wa Ivory Coast,  mkazi wa Msasani alikuwa Katibu wa Ubalozi wa Papa Mtakatifu.

Akifafanua zaidi Padri Abate alisema: “Siku ya Januari 12, mwaka huu Padri John aliniaga anakwenda Kimbiji Kigamboni katika ‘Bichi’  ya Kasa kupumzika na Padri Alen na waliniambia watarudi saa 11 jioni, tulishangaa muda ulipita tukaanza kupatwa na wasiwasi.

“Ilipofika saa mbili usiku baada ya chakula tulipata simu kutoka kwa rafiki yetu akitutaarifu kuwa wamefariki huko katika bichi.
 “Taarifa ya pili tulipata kwa njia ya simu kutoka kwa polisi wa Kituo cha Kigamboni ambao walituambia wanataka kupeleka miili ya marehemu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili hivyo tukutane hospitalini hapo.

Tulipofika tulikaa hadi saa 4 usiku ndipo miili ilipofika kwa gari la polisi na tukaambiwa tutie saini kama marehemu hao tunawafahamu.

“Hapo ndipo tulianza kusimuliwa na polisi kuwa mapadri walipofika Kasa walimuita mhudumu wa hoteli na kumuagiza kuwa ikifika saa 7:30 mchana awapelekee chakula, ilipofika muda huo (mhudumu)  alifanya kama alivyoagizwa lakini hakuwakuta badala yake aliona nguo zao zipo pembezoni mwa Bahari.

“Hivyo akajua kuwa wameenda kuogelea, baada ya muda mfupi aliona gogo linakuja nchi kavu na wakaona mwili mmoja baada ya mwingine. Haijulikani nini kiliwaua humo baharini. 
“Mwili wa Padri John tulipanga kukutana Ijumaa saa 11 alifajiri kwa ajili ya kuuaga kwa misa fupi ambapo tulifanya hivyo  na tuliusafirisha siku hiyo hiyo kwenda Ndanda wilayani Masasi Mtwara  kwa ajili ya mazishi ambayo  yalifanyika Jumamosi saa nne asubuhi,” alisema Padri Abate.

Kwenye mazishi hayo, kwa mujibu wa Padri Abate, walikuwepo maaskofu wakatoliki wa Lindi na Mtwara na Maaskofu wa Kanisa la Anglikana wa Masasi na Newala pamoja na mapadri 70, masista na waumini wengi.

Kuhusu mazishi ya Padri Alen, kiongozi huyo alisema amewasiliana na ofisi ya Ubalozi wa Papa Mtakatifu jijini   na wamesema hawawezi kuzungumza chochote mpaka uchunguzi wa kipolisi utakapotolewa.

Aidha, mwandishi wetu alienda Ubalozi wa Papa Mtakatifu kwa ajili ya kupata taarifa ya mwili wa Padri Alen ambapo  alipofika hakuweza kupata ushirikiano getini kwani aliambiwa wahusika wana kazi nyingi, hivyo asingeweza kuwaona.
Tags:

0 comments

Post a Comment