WANANCHI wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamefanya maandamano hadi ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo kulaani kitendo cha askari polisi kumuua raia mmoja kwa kukutumia risasi.
Mbali na hilo wananchi hao pia waliandamana kupinga baadhi ya askari kuwabambikiza kesi wananchi.
Tukio la kuuawa kwa raia huyo lilitokea wakati polisi walipowavamia baadhi ya vijana waliokuwa wakinywa pombe katika eneo la mnada wa Mhunze Desemba 16, mwaka jana.
Wananchi hao waliandamana wakiwa wamebeba mabango yaliyotoa ujumbe kwa serikali, wakiitaka ichunguze tukio hilo kwa umakini na kusikiliza kilio cha wananchi hao na kudai kuwa wao hawana hatia.
Kufuatia tuko hilo wananchi hao wameiomba serikali kuwachukulia hatua askari waliohusika na uonevu huo sanjari na kukomesha unyanyasaji kwa raia na kuongeza kuwa hali hiyo inawatisha wananchi kushirikiana na polisi katika kukabiliana na uhalifu.
Akizungumzia hilo Diwani wa Kata ya Kishapu Daudi Matungwa alikiri kutokea kwa tukio hilo lililosababisha mmoja wa wananchi hao aliyejulikana kwa jina la Luhende kupoteza maisha baada kupigwa risasi na polisi siku chache zilizopita.
Alisema kabla ya kifo chake, alipelekwa hospitali ya rufaa Bugando Mwanza na alifariki Desemba 19, mwaka jana.
Kufuatia kifo cha raia huyo diwani huyo alisema wananchi wa kijiji hicho baada ya kupewa taarifa ya kifo cha mwananchi mwenzao waliamua kususia mazishi hadi pale ambapo serikali ingetoa muafaka wa tatizo hilo ambapo baadaye mwili huo ulizikwa.
Kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Shinyanga, Hussein Kashindye, alipoulizwa alikiri kupokea taarifa hizo na kwamba ofisi yake inayafanyia kazi.
Naye mkuu wa wilaya ya Kishapu Abudullah Lutavi alithibitisha kupokea maandamano ya wananchi na aliwaasa kuwa wavumilivu wakati serikali ikiendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
0 comments