WAKATI wakazi wa Arusha wakiwa bado na kumbukumbu ya machungu ya kupotelewa na wenzao watatu waliouawa na Jeshi la Polisi kwa kufyatuliwa risasi za moto kwenye vurugu za kisiasa zilizotokea Januari 5 mwaka huu, Jeshi la Polisi mjini hapa limekumbwa na kashfa nyingine nzito kwa askari wake mmoja aliyekuwa amevaa sare za jeshi hilo kumfyatulia risasi ya shingoni dereva teksi mmoja na kumjeruhi vibaya.
Dereva huyo amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya Selian mjini hapa.
Taarifa za tukio hilo zimeeleza askari huyo ambaye polisi bado wanafanya uchunguzi juu ya tukio hilo, alifika katika eneo la Shivaz Kaloleni majira ya saa 10 usiku ambapo dereva teksi huyo huegesha gari lake hapo na kumtaka ampeleke katika Kituo cha Polisi cha Ngarenaro baada ya makubaliano ya kulipwa shilingi 3,000.
Imeelezwa mara baada ya kufika karibu na kituo hicho, askari huyo alimwamuru dereva huyo kusimama na alimtaka ampatie shilingi 7,000 ili ampe noti ya shilingi 10,000.
Wakati dereva huyo aliyetambulika kwa jina la Jamal Abdul (32) akijaribu kutoa noti hiyo ya shilingi 10,000, askari huyo aliyekuwa ametoka nje ya gari hilo ghafla aliikoki silaha hiyo na kumfyatulia risasi moja iliyompata sehemu ya shingo na kutokeza upande wa pili na kumjeruhi pia katika bega la kushoto.
Aidha, kwa mujibu wa maelezo ya dereva huyo aliyekuwa akiongea kwa taabu hospitalini hapo, alisema anamtambua mtu huyo kuwa ni askari polisi na kwamba mara baada ya kukumbwa na masahibu hayo aliamua kufika katika kituo hicho cha polisi Ngarenero kuomba msaada.
Alisema chakushangaza mara baada ya kufika kituoni hapo askari waliokuwa zamu siku hiyo waligoma kumfungulia mlango na kumtaka aende kituo kikuu cha polisi mjini kwa ajili ya kupata msaada zaidi.
0 comments