Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Pinda amweka kitimoto mkuu wa Jeshi la Polisi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter Chanzo: MWANANCH
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ameingilia kati vurugu zilizotokea Arusha kutokana na mvutano wa kisiasa baina ya CCM na Chadema kuhusu suala la Meya wa Jiji la Arusha akitaka kuwapo suluhisho la kudumu baina ya pande mbili hizo.
Taarifa za ndani ya kikao alichokiitisha Waziri Mkuu Pinda zilizolifikia Mwananchi jana zilieleza kuwa alikutana na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema ambaye analaumiwa na jamii kwa kuwa moja ya chanzo cha vurugu hizo na Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha ofisini kwake kuanzia saa saba mchana hadi saa kumi na moja jioni.


"Waziri Mkuu amekutana na viongozi hao, lakini kikubwa alichokuwa akitaka ni kukutana na Chadema na akataka kujifahamu katika sakata hilo nini ushiriki wa polisi katika mauaji ya raia na hasa kutokana na tuhuma mbalimbali zinazoelekezwa kwao ambapo watu watatu waliokuwamo katika maandamano hayo walipigwa risasi za moto na jeshi hilo," kilisema chanzo hicho cha habari kutoka ndani ya kikao hicho.


Viongozi hao walimpa taarifa Waziri Mkuu Pinda ya jinsi tukio zima la Arusha lilivyotokea wakibainisha baadhi ya mambo ambayo yalijitokeza katika sakata hilo zima.


Januari 5, mwaka huu, Jeshi la Polisi liliwaua watu watatu kwa kuwapiga risasi na kuwajeruhi wengine zaidi ya 20 katika harakati za kudhibiti maandamano ya amani yaliyofanywa na wafuasi wa Chadema mkoani humo kupinga utaratibu uliotumika kupata meya wa jiji hilo.




Chanzo cha habari cha Mwananchi kilieleza kuwa katika suala hilo, Waziri Mkuu alisema kuwa aliamua kuchukua hatua hiyo ili kuweza kupata suluhisho la kudumu katika sakata hilo ambalo lilmesababisha ukosefu wa amani ndani ya jiji hilo na athari zake kuenea maeneo mbalimbali nchini.


Katika kukabiliana na tatizo hilo, chanzo hicho cha habari kililieleza Mwananchi kwamba Waziri Mkuu alitoa kauli kuwa atakutana na Chadema na kuzungumza nao ingawa hakueleza ni lini atafanya hivyo kwa lengo la kumaliza mgogoro huo wa kisiasa ambao unazidi kuchukua sura mpya kila siku.


"Unajua suala hili lilionyesha kumkera Waziri Mkuu na akatoa mfano wa suluhisho linaloweza kuchukuliwa kuwa ni mfano wa ilivyotokea katika manispaa ya Kigoma katika uongozi uliopita ambapo CCM waliongoza kipindi cha miaka miwili na nusu ya mwanzo na hatimaye miaka miwili na nusu ya mwisho kikaongoza Chadema,"kilieleza chanzo hicho.


Ilielezwa pia kwamba lengo la kikao hicho cha Waziri Mkuu Pinda ni kuondoa utata uliopo sasa kwenye sakata zima la umeya wa Arusha na kurejesha hali ya kisiasa katika hali ya kawaida.


Waziri Mkuu anachukua hatua hiyo wakati tayari kukiwa kumeshaibuka sintofahamu baada ya maaskofu wa makanisa ya Kikristo mkoani Arusha, kutoa tamko la pamoja la kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha aliyeteuliwa na CCM, Gaudence Lyimo,  Januari 7 mwaka huu.


Serikali kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha alishatoa tamko kwamba vurugu zilizotokea Arusha ni tatizo la kisiasa ambalo pia litapaswa kushughulikiwa kisiasa.


Lakini, Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Arusha, kikawataka maaskofu mkoani Arusha kuvua majoho na kutangaza kuingia katika siasa, badala ya kuingilia mambo ya siasa yasiyowahusu ya Meya wa Jiji la Arusha.


Wakati katibu huyo wa mkoa wa CCM akieleza hayo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba alienda mbali zaidi na kuwataka maaskofu hao waende mahakamani au wawashauri Chadema kufanya hivyo kwa lengo la kupinga matokeo ya umeya.


Makamba alisisitiza kuwa msimamo wa CCM ni kwamba chama hicho ndicho kilichoshinda katika uchaguzi huo wa umeya Arusha.


Tofauti na Makamba na Chatanda, juzi Waziri Mkuu wa zamani, John Malecela, akakemea vikali akisema kuwa CCM imewakosea adabu maaskofu hivyo inapaswa kukutana nao na kuwaomba radhi.


Akizungumza na Mwananchi, Malecela alisema kitendo cha kuwashambulia maaskofu hao kilichofanywa na CCM mkoani Arusha ikiwa ni pamoja na kuwataka wavue majoho na kuingia kwenye siasa, ni utovu wa nidhamu. Malecela alitaka juhudi za haraka kumaliza mzozo huo zifanyike.


Mbali na Malecele, mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa CCM, Peter Kisumo juzi hiyo hiyo alivitaka vyama vya Chadema na CCM kuacha kiburi na kukaa meza moja kutafuta muafaka wa mgogoro wa kisiasa jijini Arusha.


"Arusha ni tukio moja baya sana na ni baya kwa maana kwamba mimi kama raia wa Tanzania ninashituka kuona tunashindwa kitu tunachokiita political management (utawala wa siasa) na hili ni jambo baya sana,"alisema Kisumo.


Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amesema kwamba amesononeshwa na tukio la vurugu zilizotokea Aruisha wiki iliyotokea na kusababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi zaidi ya 20.


Rais Kikwete alisema atahakikisha hatua zinachukuliwa ili kujenga mazingira ambayo hayataruhusu tukio jingine kama hilo kutokea tena siku zijazo.


Azimio hilo la Kikwete lilielezwa jana na Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mpainduzi (CCM), Pius Msekwa katika mahojiano na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kupitia kituo chake cha televisheni cha TBC1.


"Mheshimiwa Rais Kikwete amesononeshwa sana na kile kilichotokea katika Manispaa ya Arusha," alisema Msekwa akinukuu kauli ya Rais Kikwete kuhusiana na tukio hilo lililotokana na maandamano ya Chadema kutawazwa umeya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo wa CCM.


Kwa sababu hiyo, Msekwa alisema wameamua kikao cha Kamati Kuu ya CCM kukutana haraka iwezekanavyo ili kujadili suala hilo na kuliwekea msimamo utakaotoa suluhishio la kudumu.


Msekwa alikataa kata kata kutoa maoni yake kuhusiana na tukio hilo ambalo limeonekana kulitikisa taifa na kuwafanya wanasiasa, wasomi, viongozi wa kawaida kulizungumzia kwa hisia tofauti.




Sent from my iPhone
Tags:

0 comments

Post a Comment