Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Pinda ajiweka matatani

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amesuluhisha mgogoro uliokuwepo baina ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na wahadhiri wa chuo hicho kuhusu maslahi yao na wamekubali kuingia madarasani kuanzia leo.

Wahadhiri hao wamekubali kusitisha mgomo na kutoa sharti kuwa madai yao yawe yameshughulikiwa hadi ifikapo mwezi Februari mwaka huu.

Waziri Mkuu ataingia matatani iwapo serikali itashindwa kutekeleza ahadi hiyo, kwani wahadhiri hao wamemtahadharisha kuwa iwapo madai hayo hayatafanyiwa kazi katika kipindi hicho, wataitisha mgomo mkubwa ambao utakuwa mkali zaidi.

Vyanzo vya habari vya kuaminika vimeeleza kuwa serikali imekuwa na kawaida ya kuahirisha migomo na kero mbalimbali zinazotokea kwa ahadi ya kushughulikia, lakini utekelezaji wake umekuwa si wa uhakika.

Akizungumza na wanajumuiya ya wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) jana kwenye ukumbi wa Chimwaga, Pinda alisema matatizo yaliyojitokeza katika chuo hicho ni mlundikano wa mambo ambayo yamekuwepo siku nyingi, lakini mengi ni ya kiutendaji na yanaweza kuisha bila kupoteza muda mwingi.

"Nimeongea na viongozi wa UDOMASA na kuwaahidi kuwa madai yenu ya posho yanaweza kukamilika mwezi Februari, nilitaka yaishe mwezi huu lakini kwa taratibu za HAZINA sasa hivi wameshaanza kushughulikia mishahara ya Januari kwa hiyo marekebisho yenu hayawezi kuwahi…wameniahidi mwezi ujao yatakamilika," alisema huku akishangiliwa.

Alisema amemwagiza Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aende kukagua taarifa za mahesabu ya chuo hicho ili kubaini tuhuma zilizojitokeza za watu kulipwa hundi mbili za mishahara, walioacha kazi kuendelea kuwemo kwenye malipo ya mishahara na wengine kukosekana kabisa.

"Taarifa nilizonazo ni kwamba CAG atakuwa hapa kesho… mpeni ushirikiano ili aifanye kazi kwa urahisi…, nia yetu ni kuangalia mfumo mzima wa fedha na utawala ukoje ili ikibidi uweze kurekebishwa," alisema.

Mbali na kusuluhisha mgogoro huo, Pinda alieleza kusikitishwa na uozo mkubwa na ufisadi unaofanywa na uongozi wa chuo hicho ambao umesababisha kutokea kwa mvutano mkubwa kati ya uongozi wa chuo na wahadhiri.

Katika mgogoro huo pia imebaini kuwa tatizo kubwa linatokana na uongozi wa chuo kushindwa kusimamia mipango ya malipo ya wahadhiri huku ikibainika kuwa wapo watumishi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara mara mbili.

Aidha, alisema kitendo cha watumishi kushindwa kulipwa mishahara mipya kutokana na waraka wa serikali ni ukiukwaji wa taratibu na kanuni za sheria serikalini na kinachotokea ni walimu kuendelea kulipwa mishahara ambayo haiendani na waraka huo.

Alisema kitendo cha kutowalipa watumishi hao mishahara ambayo inaendana na viwango vyao vya kazi ni ufisadi mkubwa ambao unafanyika kwa njia ya uonevu na kusababisha migogoro ambayo inaweza kuleta majanga makubwa katika jamii wanayofanya nayo kazi.

"Nasikitika kuona uongozi wa chuo umekuwa ukikata pesa za watumishi bila maelezo yoyote kwa watumishi hao na kujifanya miungu watu, jamani ninyi viongozi wa chuo kwa nini mnashindwa kufanya kazi na watumishi katika njia ya uwazi?" alihoji Pinda.

Mbali na hilo, Waziri Mkuu alieleza matatizo makubwa yanayotokea chuoni hapo yanasababishwa na uongozi wa chuo kutokuwa na ushirikiano mzuri na watumishi na zaidi umekuwa ukikiuka taratibu za ulipaji mishahara kwa watumishi kwa mujibu wa waraka wa serikali kutoka hazina.

Alisema kitu kingine ambacho kimekuwa sababisho kubwa la chuo kuingia katika migogoro ni kutokana na viongozi wa chuo kujifanya miungu watu kwa kutumia vibaya madaraka yao ikiwa ni pamoja na kushindwa kukaa meza moja na watumishi juu ya malalamiko yao.

Pamoja na juhudi za Pinda kutatua mgogoro huo uongozi wa umoja wa wahadhiri na wataaluma ulimtaka Kaimu Mkuu wa chuo, Profesa Idris Kikula, kuomba radhi kutokana na kutokuwatendea haki ikiwa ni pamoja na kutoa maneno ya kejeli kwa wahadhiri hao.

Akizungumza kwa niaba ya wahadhiri, Mwenyekiti wa UDOMASA, Paul Louisulie, alisema, Profesa Kikula, amekuwa akishindwa kutoa ushirikiano huku wakidai uongozi wa chuo umekuwa ukifanya kazi kwa mabavu.

Aidha, mwenyekiti huyo wa UDOMASA, alitoa tamko la kusitisha mgomo kwa sharti kuwa iwapo madai yao hayatafanyiwa kazi hadi Februari mwishoni wataitisha mgomo mkubwa ambao utakuwa mkali zaidi.

Kuhusu madai ya wanafunzi ya tatizo la maji, Pinda alisema amemwagiza Naibu Katibu Mkuu (Fedha), John Haule, afuatilie uhamisho wa ndani wa fedha (reallocation) katika Wizara ya Maji, ili zipatikane sh bilioni 1.66 zinazohitajiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dodoma (DUWASA) kuchimba visima maeneo ya Ng'ong'ona na Ihumwa ikiwa ni pamoja na kutandaza mabomba hadi chuoni.

Alisema katika mipango ya muda mrefu, DUWASA pia wanatarajia kupata dola milioni 26 za Marekani ambazo zitatumika kuchimba visima vingine na kujenga matanki yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 12 za maji, hivyo kuondoa kabisa tatizo la maji chuoni hapo.

Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula, alimweleza Waziri Mkuu kwamba mahitaji halisi ya maji chuoni hapo ni lita milioni 3.5 kwa siku ambazo kati ya hizo, lita milioni 1.5 ni kwa matumizi ya wanafunzi peke yao na lita nyingine milioni 2 ni kwa matumizi ya ujenzi wa majengo unaoendelea chuoni hapo.

Akifunga mkutano huo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Idris Kikula, alimwahidi Waziri Mkuu kwamba maagizo yake yatafuatiliwa na kwamba leo menejimenti, idara ya uhasibu na UDOMASA watakutana ili kuunda timu ya pamoja ambayo itakaa na kubainisha stahili za walimu wote ili orodha hiyo iwasilishwe kwa Waziri Mkuu mapema iwezekanavyo kwa ufuatiliaji.

Wakati huohuo, Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), kimeipa serikali wiki tatu kulipa malimbikizo yote na mishahara mipya ya wafanyakazi wa umma hasa wa Elimu ya Juu, vinginevyo wataiburuza mahakamani.

Fedha zinazodaiwa ni kuanzia Julai hadi Oktoba, ambapo kuchelewa kwake kumesababishwa na serikali pamoja na kutowajibika kwa menejimenti za taasisi.

Onyo hilo limetolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Raawu, Adelgunda Mgaya, alipozungumza na waandishi wa habari.

"Kugoma kwa wahadhiri katika vyuo vikuu nchini ikiwemo Dodoma kumesababishwa na jeuri, umangimeza na uzembe katika kushughulikia haki zao kwa haraka na ufanisi unaofanywa na serikali.

"Raawu kwa mara nyingine tena tunaitaka serikali kukamilisha haraka zoezi la ulipaji wa mishahara mipya na malimbikizo yake na kuondoa kasoro zote zilizojitokeza ifikapo mwishoni mwa Januari.

"Pia haitasita kuwachukulia hatua za utetezi wanachama wake kulingana na sheria za kazi endapo malalamiko hayo hayatashughulikiwa na kumalizwa ndani ya kipindi cha kuanzia sasa hadi mwisho mwa Januari," alisema Adelgunda.

Alisema serikali itambue kuwa wafanyakazi wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu ingawaje uvumilivu unaelekea ukingoni.

Alisema Julai mwaka jana, serikali ilipandisha mishahara ya wafanyakazi wake viwango tofauti kulingana na maafikiano katika vikao vya majadiliano ya pamoja baina yake na vyama husika vya wafanyakazi.

Alifafanua kwa kawaida ulipaji huanza mara moja kwa watumishi wa serikali kuu na serikali za mitaa ambapo kwa taasisi za serikali huanza baada ya kipindi cha miezi miwili hadi mitatu kuruhusu kufanyika kwa marekebisho.

Katika maelezo yake alisema wamefuatilia utekelezaji wake wa malipo hayo, ambapo wamegundua baadhi ya taasisi hazijalipwa hadi sasa.

Alisema katika taasisi zilizolipwa kumejitokeza kasoro mbalimbali ikiwa ni pamoja na mapunjo yanayotokana na makosa ya ukokotoaji na kukosewa kwa kumbukumbu za wafanyakazi uliofanywa na menejimenti.


Tags:

0 comments

Post a Comment