Jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika magharaibi, ECOWAS inasemekana kufanya mipango ya kumuondoa kiongozi wa Côte d'Ivoire, Laurent Gbagbo kwa nguvu ikihitajika, iwapo hatoondoka madarakani na kutoa nafasi kwa kiongozi anayetambulika kimataifa kama rais mchaguliwa, Alassane Outtara. Ouattara hii leo ameliambia gazeti la Ufaransa La Croix, kwamba uvamizi wa kijeshi umepangwa.Wapatanishi wa Umoja wa Afrika wamesema muda unamalizika kwa Gbagbo kusuluhisha mkwamo huo kwa amani.
Umoja wa Mataifa waongeza wanajeshi Cote d'Ivoire
Mjini New York, Marekani, katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la umoja huo, limeagiza kwamba wanajeshi 2,000 waongezwe katika kikosi chake cha UNOCI nchini Cote d'Ivoire. Hii ni kufuatia taarifa za makamanda wake walioko mjini Abdijan, ambao wanahofia mapigano kati yao na vikosi vitiifu kwa Laurent Gbagbo, ambavyo vinayazingira makao makuu ya Alassane Ouattara yaliyo kwenye hoteli ya Golf mjini humo.
Kwa wiki kadhaa sasa, vikosi vya Gbagbo vimeizingira hoteli hiyo na Gbagbo amekataa kuviondosha licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Umoja wa Mataifa, na mwenyewe kuahidi mara mbili kwamba angeliviondoa.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamesema kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mauaji ya maangamizi na uhalifu dhidi ya binaadamu nchini humo, ikiwa mgogoro huu haukuzuiwa haraka.
Odinga atoka mikono mitupu
Kiongozi anayetambuliwa kama mshindi wa uchaguzi wa Cote d'Ivoire, Alassane Ouattara (kushoto) akiwa na Waziri Mkuu wa Kenya, Raila OdingaMapema hapo jana, mjumbe maalum wa Umoja wa Afrika katika kutafuta suluhu ya Cote d'Ivoire, Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, alitoka mikono mitupu katika ziara yake ya mwisho nchini humo, baada ya kuambiwa na utawala wa Gbagbo, kwamba asikanyage mguu wake tena Abdijan.
"Bwana Odinga amefeli kwenye ujumbe wake na hatuko tayari kumpokea tena hapa Cote d'Ivoire. Tunamkataa moja kwa moja." Alseima Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Gbagbo, Alcide Djedje.
Odinga mwenyewe alishatangaza tangu jana kwamba, hakuna uwezekano wowote wa Gbagbo kuondoka madarakani kwa hiari yake, kwani amekuwa akivunja kila ahadi anayoiweka, ikiwemo ile ya kuondoa vizuizi kwenye makao makuu ya Ouattara.
"Licha ya majadiliano ya kina na Bwana Laurent Gbagbo na Rais mteule Alassane Ouattara, ambayo yaliendelea mpaka usiku wa manane, nasikitika kutangaza kwamba ule uwezekano uliotarajiwa kuutatua mzozo huu, haukufanikiwa." Alisema Odinga.
Hii ilikuwa ni safari ya pili kwa Odinga mjini Abdijan, na mara hii alikuwa amemwendea Gbagbo na ahadi ya kinga na ulinzi, ikiwa angelikubali kuondoka madarakani, ili kuinusuru nchi isiingie kwenye machafuko zaidi, ambayo hadi sasa yameshasababisha vifo kadhaa vya watu.
Maandalizi ya Operesheni ya Kijeshi
Uamuzi huu wa sasa wa Umoja wa Mataifa kuongeza wanajeshi hawa 2,000, ambao unaifanya idadi ya wanajeshi wa kikosi cha UNOCI kufikia 11,500, umekuja katika wakati ambao, wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika ya Magharibi, walikuwa wanakutana nchini Mali, kupanga mikakati ya mwisho ya kumuondoa madarakani Gbagbo kwa kutumia nguvu.
Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kijeshi wanasema kwamba, ili uvamizi huu wa ECOWAS uwe na mafanikio, ni lazima ushirikishe, kwa uchache, wanajeshi 20,000, ingawa hadi sasa jumuiya hii ina wanajeshi 3,500 tu katika akiba yake.
Odinga akatisha ziara yake Cote d'Ivoire
Msemaji wa Raila Odinga, Salim Lone amesema kuwa waziri huyo mkuu wa Kenya anatarajiwa kuondoka mjini Abidjan baada ya ziara yake ya saa 48 kutopata majibu sahihi kuhusu swali la nani anatakiwa kuiongoza Cote d'Ivoire. Bwana Lone amesema Odinga jana alikuwa akiwasiliana na kiongozi anayeng'ang'ania madaraka katika taifa hilo la Afrika Magharibi, Laurent Gbagbo na mpinzani wake Alassane Ouattara anayetambuliwa kimataifa kama mshindi wa uchaguzi wa mwezi Novemba, mwaka uliopita, lakini hadi sasa hakuna jambo muhimu ambalo limejitokeza.
Bwana Odinga alitarajiwa kwenda moja kwa moja Accra, Ghana leo baada ya Jumatatu kusema kuwa atakwenda kwa mazungumzo nchini humo pamoja na Angola na Burkina Faso. Pendekezo la mazungumzo lilitolewa siku ya Jumatatu, huku viongozi wa kanda hiyo wakiimarisha msimamo wao wa kujiingiaza kijeshi ili kuondoa hali hiyo ya mkwamo. Awali, Gbagbo alisema yuko tayari kufanya mazungumzo na mpinzani wake, lakini amekataa ahadi zote alizopewa ili aondoke madarakani, ikiwemo ya kwenda kuishi uhamishoni na kupewa kinga ya kutoshtakiwa kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu.
Mpatanishi huyo wa mzozo wa kisiasa nchini Cote d'Ivoire awali alikuwa na matumaini ya ziara yake ya sasa na anasubiri majibu yaliyotolewa Jumatatu. Lone amefafanua kuwa Bwana Odinga hana tena mpango wa kurudi Cote d'Ivoire, hadi atakapohitajika kufanya hivyo. Aidha, mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi-ECOWAS, ambaye pia ni rais wa Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambaye pia ni mwenyekiti wa ECOWASNigeria, Goodluck Jonathan amesema katika taarifa yake kuwa jumuiya hiyo inataka kupatikana suluhuhisho kwa njia ya amani.
Hata hivyo, ameongeza kusema kuwa hawajabadilisha msimamo wao walioutangaza kwenye kikao chao kilichopita, kuwa huenda wakatumia nguvu za kijeshi iwapo itahitajika kufanya hivyo. Rais Jonathan amefafanua kwamba kura za wananchi lazima zihesabiwe mara baada ya kupigwa, la sivyo demokrasia haitakuwepo barani Afrika. Naye afisa wa ngazi ya juu wa ECOWAS, Olusegun Petinrin amesema wako tayari kutumia nguvu iwapo itahitajika na kwamba lazima hilo lieleweke wazi. Nao wakuu wa majeshi katika nchi za Magharibi mwa Afrika wanakutana kwa siku mbili ikiwa ni katika kukamilisha mpango wa kijeshi wa kumuondoa madarakani Gbagbo kinguvu. Angola kwa upande wake imetoa msimamo wake kuhusu mzozo wa kisiasa wa Cote d'Ivoire.
Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Michelle Alliot-Marie ameonya matumizi ya nguvu yatumike tu kama hatua ya mwisho kabisa, kwa sababu yanaweza kukasababisha maafa makubwa zaidi. Zaidi ya watu 200 wameuawa katika mapigano tangu kumalizika kwa uchaguzi. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo linatarajiwa kupiga kura ya kuamua iwapo ipeleke wanajeshi 2,000 zaidi nchini Cote d'Ivoire baada ya Urusi kupinga. Hata hivyo, kuongezwa kwa wanajeshi hao kunahofiwa kunaweza kuhatarisha zaidi hali ya mambo kutokana na Gbagbo mara kadhaa kuvitaka vikosi vya Umoja wa Mataifa kuondoka nchini humo. Endapo wanajeshi wengine watapelekwa, basi kutakuwa na hadi wanajeshi 11,500.
0 comments