Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mnyika kuwasilisha hoja ya katiba mpya

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Mbunge wa Ubungo, John MnyikaMBUNGE 

wa Ubungo, John Mnyika amesema kuwa atawasilisha bungeni hoja binafsi ya kutaka mabadiliko ya katiba na kupinga moja ya mapendekezo ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda la kuunda tume ya kuangalia mchakato huo.
Tangu kumalizika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, Chadema imewasha moto wa mabadiliko ya katiba na kufufua mjadala wa kutaka kuandikwa kwa katiba mpya kiasi cha Waziri Pinda kuamua kutoa tamko mwishoni mwa wiki kuwa atamshauri Rais Jakaya Kikwete aunde tume kuchunguza madai hayo.

Miongoni mwa viongozi waliojiunga kwenye mjadala huo wa kutaka katiba mpya ni mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Sinde Warioba na Frederick Sumaye, Jaji Mkuu Agustino Ramadhan na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ambaye alitahadharisha kuwa bila ya katiba mpya nchi inaweza kuingia kwenye vurugu.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mnyika ambaye ni mmoja wa wabunge vijana kwenye Bunge la Kumi, alisema atatimiza ahadi yake katika kipindi cha wiki moja kwa kuwasilisha taarifa kuhusu hoja binafsi ya katiba mpya kwa katibu wa bunge.
"Ibara ya 8 kifungu kwanza cha katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na mapungufu yake inaeleza wazi umuhimu wa wananchi kushirikishwa katika uundwaji wa katiba. Pia Ibara ya 63-(2) nayo inaeleza wazi," alisema  Mnyika.
Aliongeza kuwa kama mbunge ana haki ya kuwasilisha hoja binafsi kuhusu katiba mpya na kwamba ni vyema suala la uundwaji wa katiba likarejeshwa mikononi mwa Bunge kwa kuwa ni mhimili wa dola unaofanya kazi kwa niaba ya wananchi.

"Ibara ya 98 ya katiba ndio sehemu  pekee inayozungumzia marekebisho ya katiba hivyo ni wakati muafaka suala hili la katiba likapelekwa bungeni ili wananchi wawakilishwe," alifafanua Mnyika.
Mwanasiasa huyo kinda, ambaye pia ni mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Chadema, alieleza sababu za kutaka kupeleka hoja hiyo bungeni ni kutaka chombo hicho lipitishe mchakato wa kuundwa kwa katiba mpya.

"Unajua katiba ni sheria na kwa kuwa bungeni ndiko kunakotungwa sheria basi wanaopaswa kutoa mwelekeo wa katiba mpya ni Bunge," aliongeza.
"Pia katiba ni mkataba kati ya wananchi na watawala... ikumbukwe kuwa anayeandika mkataba ni mwenye mali, na hapa mwenye mali ni mwananchi na Bunge lipo kwa ajili ya wananchi. Kutokana na hilo, ipo kila sababu ya suala hili kurudi bungeni."

Lakini Mnyika alipingana na moja ya mapendekezo ya Waziri Pinda ya kuunda tume ya kuangalia mchakato wa kuandikwa kwa katiba mpya.
"Sikubaliani na kauli ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuhusu katiba,” Mnyika aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana.
“(Waziri Mkuu) Amesema atamshauri rais kuunda timu itakayoangalia mapendekezo ya tume zilizoundwa na pia kuanzisha utaratibu wa marekebisho ya katiba. Naona kauli yake haijalenga kuwepo kwa katiba mpya, bali inalenga zaidi marekebisho ya katiba."

Mnyika alifafanua kwamba, hoja hiyo ya Pinda ina mwelekeo wa kuchukua suala la katiba mpya mikononi mwa wananchi na kulipeleka kwa kundi fulani.
Waziri Pinda aliwaeleza wahariri wa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki kuwa kuna njia mbili za kushughulikia kilio cha wananchi cha katiba mpya, akiitaja ya kwanza kuwa ni kumshauri rais aunde kamati ya watu ambao wataangalie maeneo gani ya kuingiza katika katiba.

Alisema njia ya pili ni rais kuunda timu yake ya kiserikali itakayoangalia mapendekezo ya tume zilizoundwa awali kuangalia marekebisho ya katiba na kuchukua mapendekezo yaliyojirudia yatakayoonekana kufaa kuingia katika katiba.

Lakini Mnyika alipingana na mapendekezo hayo akisema haoni sababu ya kuundwa kwa tume nyingine kwa kuwa tangu nchi ipate uhuru, zimeshaundwa tume nyingi kushughulikia suala la katiba.
Alitoa mfano wa Tume ya Jaji Nyalali ambayo ilipendekezwa kufutwa kwa sheria kadhaa ambazo zinaonekana kukandamiza haki za binadamu na Tume ya Jaji Kisanga, akisema matokeo ya uchunguzi wa vyombo hivyo viwili hayajafanyiwa kazi.

"Kutokana na hoja hii napendekeza kwamba, Bunge liweke mfumo wa tume ya kikatiba pamoja na kupitisha azimio ili nchi ifanye mkutano mkuu wa kikatiba kujadili suala hili na kisha zipigwe kura za maoni," alisema.
Alisisitiza kuwa katika suala la katiba mpya, ni lazima wananchi washirikishwe kwa kuwa sasa Watanzaania wanataka katiba mpya.

"Kwanza, katiba inayotumika hii leo ni ya mwaka 1977, tangu kipindi hicho kuna mabadiliko mengi yameshatokea kama ya kiuchumi, kiteknolojia; pili uundwaji wa katiba hiyo haukuwashirikisha wananchi; tatu katiba hii inakabiliwa na changamoto nyingi, mfano suala la Muungano na Tume ya Uchaguzi," alisema.

Chadema ilionyesha kwa vitendo dhamira yake ya kudai katiba mpya wakati wabunge wake walipoondoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akianza kutoa hotuba ya ufunguzi. Viongozi wa chama hicho pia walisusia hafla ya kutangazwa kwa matokeo na sherehe za kuapishwa kwa rais na wiki mbili zilizopita hawakuonekana kwenye sherehe za uhuru.

MAONI....

#9 mdanganyika 2010-12-20 12:51
Kikwete na CCM yake wameshavunja katiba waliyoapa kuilinda. Katiba inasema yetu inatakiwa iwe ya UJAMAA na KUJITEGEMEA. Nchi ni ya kibepari sio kijamaa na tunawategemea wahisani kwa zaidi ya 40% ya bajeti ambapo kwa bajeti ya maendeleo utegemezi ni mpaka 95%!
Quote
 
 
+1#8 Elly Ngailo. 2010-12-20 12:49
Hongera Mnyika, 2nataka viongozi wenye fikra za kimapinduzi kama zako. Wenye uwezo wa ku-analyse mambo kwa upeo kwa faida ya wananchi wa Tz. Tupo nyuma yako kamanda. Together we shall win !!
Quote
 
 
-4#7 kyungululukanswita 2010-12-20 11:26
pinda alichosema kitekelezwe haraka,kwa hekima bila kuathili jamii ya waTZ.watanzania tusiwe na haraka,haraka haraka haina baraka.
Quote
 
 
+1#6 roberti 2010-12-20 11:06
no.4.U like it or not .Chadema Mwaka huo ndiyo walianza na moto so sorrrrrrrrrry.
Mnyika go, chadema goooo.
Quote
 
 
0#5 k- Basil 2010-12-20 10:37
Mzee Pinda(PM)namhes him kwa vile ni Mzee wetu mwenye busara kati ya wachache waliopo.Ninachomwomba kwa busara alizonazo,amsha uri JK kuirejea ripoti ya tume ya JAJI NYALALI(Mungu amrehemu) na si kuunda tume nyingine.Tme yake iliundwa wakati ambapo vuguvugu la vyama vingi ndo lilikuwalimepam ba moto, nami wakati ndo nilikuwa Olevel,na hatujarudi nyuma tangu wakati huo.
Quote
 
 
-14#4 freshmind 2010-12-20 08:32
Fidelis Butahe....ivi unataka kuueleza umma wa watz kua chadema tu ndo chama kinachowasha moto wa katiba mpya?
Ivi kwa nini nyinyi waandishi mnaonyesha utashi wa moja kwa moja kwa chama fulani? Mr.Fidelis hayo ndiyo maadili ya uandishi wa habari?
Ebu angalia iyo statement yako uliyoanza nayo
"Tangu [NENO BAYA]lizika uchaguzi mkuu wa Oktoba 31, Chadema imewasha moto wa mabadiliko ya katiba"
Siku izi hakuna tena waandishi wa habari kuna vibaraka(makada ) wa vyama
Quote
 
 
+5#3 Brigedia General 2010-12-20 08:32
Huu u[NENO BAYA] wa kumuomba raisi aunde tume ndiyo ule ule u[NENO BAYA] unaotukwamisha. Katiba ya safari hii itaundwa na wananchi na wala siyo tume iliyoteuliwa na de facto prsident. Way to go Mnyika, change you can believe in!
Quote
 
 
-12#2 fgkjfdkjgfdgh 2010-12-20 07:53
alichosema Pinda ndio sahihi kwanza zifuatwe ripoti zilizopita na pia yatolewe maoni mapya kama yapo. Anchofanya Mnyika ni kutaka kujipatia umaarufu. Hoja yake haitapita bungeni hata yeye mwenyewe anajua. Bunge linatumia hela nyingi ambazo zingeweza kufanya shughuli nyingine za maendeleo. Wabunge tumieni muda kujadili mambo yanye kunufaisha wananchi sio kutafuta sifa binafsi
Quote
 
 
+9#1 nkwazi mhango 2010-12-20 06:28
Kama kuna kitu kinachoweza kumpa legacy Jakaya Kikwete kilichobakia ni kuridhia na kusimamia uandikwaji wa katiba mpya. Najua CCM na Kikwete mwenyewe wanaliogopa hili sawa na alivyowahi kufanya Daniel arap Moi pale Kenya.
Alipokuja Mwai Kibaki alichafuka na kuvuruga kila kitu. Alishiriki ufisadi na kuulinda kama anavyofanya Kikwete. Aliiba kura na kupora urais kama Kikwete.
Baada ya kuona amechafuka kiasi cha kutoweza kutamanika, Kibaki alichomoa karata moja iliyomfanya aheshimike na kuacha legacy ya kizalendo. Alichofanya ni kuridhia na kuhakikisha katiba mpya inaandikwa. Naamini asingefanya hivyo angepelekwa The Hague kama watuhumiwa wengine.
Nimalizie kwa msihi Kikwete asiache fursa hii ikampita na kupotea kwa kuhofia wana-CCM wenzake ambao wengi licha ya kuwa na mawazo chakavu ni mafisadi wa kutupwa.
Tags:

0 comments

Post a Comment