IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
JAJI Mkuu anayemaliza muda wake, Agustino Ramadhan amezungumzia tena umuhimu wa kuandikwa kwa katiba mpya, safari hii akitaka uundwaji wake uharakishwe ili kukabiliana na changamoto zinazoikabili nchi.
Ramadhan alishawahi kukaririwa akisema kuwa suala la katiba mpya linazungumzika, akiungana na wanasiasa wa kada mbalimbali, wanasheria na wanaharakati ambao walieleza kuwa suala hilo sasa haliepukiki.
Jana, Jaji Ramadhan, ambaye ameshamaliza muda wake, alikiambia Kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na katiba mpya. “Kuna umuhimu wa kubadilisha katiba ya nchi yetu ili kuondoa upungufu uliopo katika katiba ya sasa ambayo inalalamikiwa na wengi,|” alisema jaji Ramadhan.
Jaji Ramadhan alitoa mfano wa upungufu uliopo kwenye muda wa kustaafu wa jaji mkuu na majaji wengine akisema ni moja ya mambo yanayoweza kuangaliwa wakati wa kuandika katiba mpya. "Katiba inasema Jaji Mkuu atastaafu kwenye muda wanaostaafu majaji wengine. Muda huo ni miaka 65, huu unaweza kuwa upungufu mwingine kwenye katiba," alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Radhaman, katiba ya sasa ina upungufu mkubwa ambao hauna budi kuangaliwa kwa jicho la kuusahihisha kwa maslahi ya Watanzania.
Jaji Ramadhan alisema kuna umuhimu wa kubadilisha katiba ili kukidhi mapungufu yaliyojitokeza katika katiba ya awali.
Suala la mabadiliko au kuandikwa katiba mpya limezungumziwa na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wastaafu.
Baadhi ya viongozi hao ni Rais wa Serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye na majaji kadhaa ambao walishazungumzia umuhimu wa katiba mpya. Lakini msisitizo mkubwa uliwekwa na msajili wa vyama vya siasa, John Tendwa ambaye alisema bayana kuwa katiba mpya iandikwe mapema kabla ya mambo kuwa mabaya, akitoa mfano wa mapungufu ya katiba ya sasa kuwa ni rais kupewa madaraka makubwa.
You Are Here: Home - - Jaji mkuu ataka katiba mpya iharakishwe
0 comments