Viongozi wa mataifa ya Afrika Magharibi wamemaliza ziara yao nchini Ivory Coast ya kumshawishi Laurent Gbagbo kuachia madaraka, kufuatia kumalizika kwa uchaguzi wa urais wenye utata.
Bw Gbagbo anagoma kuachia madaraka kwa Alassane Ouattara, ambaye anatambulika kimataifa kama rais aliyechaguliwa.
Ujumbe wa viongozi hao umesema iwapo ataendelea na msimamo wake, anaweza kutolewa kwa nguvu za kijeshi.
Hatarini
Televisheni ya Ivory Coast ambayo inamtii Bw Gbagbo imewashambulia wanaomlaani kiongozi huyo kwa uamuzi wake wa kusalia madarakani.
Imesema, wananchi wa mataifa mengine ya Afrika wanaofanya kazi nchini humo huenda wakawa hatarini iwapo vitisho vya nguvu ya kijeshi vitaendelea kutolewa.
Mapema, askari wa kulinda usalama wa Umoja wa Mataifa alijeruhiwa mkononi kwa kupigwa na panga, wakati msafara wake uliposhambuliwa na kundi la watu katika ngome ya Bw Gbagbo.
Kuondoka
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema moja kati ya magari matatu kwenye msafara huo, lilichomwa moto, katika eneo la magharibi mwa mji wa Abidjan.
UN, ambayo ina zaidi ya wanajeshi 9,500 nchini Ivory Coast, imetuhumiwa na Bw Gbagbo kwa kuingilia masuala ya Ivory Coast, na kutakiwa kuondoka nchini humo.
UN imekataa kutii amri hiyo na kutaka utawala ukabidhiwe kwa Bw Ouattara.
Taarifa iliyotolewa na Rais wa Cape Verde Pedro Pires ambaye ni mmoja wa viongozi watatu wa mataifa wa Afrika Magharibi, imesema ziara yao imemalizika na watakwenda Nigeria kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Kiuchumi wa Afrika Magharibi, Ecowas, Goodluck Jonathan.
Marais wa mataifa matatu waliofanya ziara ni, Rais Pires, Bon Yayi wa Benin, na rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma. Waliwasili asubuhi mjini Abidjan katika kile kinachoonekana kama hatua ya mwisho ya kumtaka Bw Gbagbo kuachia ngazi kwa njia ya amani.
Baada ya mkutano, rais wa Benin Boni Yayi alisema kila kitu "kimekwenda vizuri". Lakini mshauri wa Laurent Gbagbo, Abdon Bayeto, baadaye aliiambia BBC kuwa "ujumbe ambao Bw Gbagbo amewaambia ni kuwa yeye amechaguliwa kidemokrasia, na anatambuliwa kikatiba".
Marais hao watatu pia walikwenda kumuona Bw Ouattara, katika hoteli anayoishi, akiwa na baraza lake la mawaziri, huku wakilindwa na wanajeshi 800 wa UN.
0 comments