Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Slaa amwaga machozi • ASHANGAA WATU KUTESEKA MIAKA 50 BAADA YA UHURU

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, juzi alibubujikwa na machozi baada ya kushuhudia umaskini wa kutupwa na nyumba duni zinazotumiwa na wananchi wa eneo la Katanga Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.
“Nimezunguka sehemu mbalimbali nchini na kushuhudia maisha magumu wanayoishi Watanzania. Lakini leo nimeshindwa kujizuia nisitokwe machozi baada ya kuona nyumba duni wanazoishi wananchi wa Katanga… sasa karibu miaka 50 baada ya taifa hili kupata uhuru, bado kuna Watanzania wanaishi kwenye nyumba za tembe zenye sakafu za udongo zilizojaa mashimo!” alihuzunika Dk. Slaa.

Akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Sabasaba katika eneo la Namanyere, Dk. Slaa alisema muda umefika kwa Watanzania kukataa kuendelea kuishi maisha duni ya umaskini wa kutupwa, licha ya taifa kuwa na utajiri wa kupindukia.

“Hatuwezi kuendelea kuishi kwenye hali hii, lazima Watanzania tufanye mabadiliko kwa nguvu ya kura… yapata miaka 50 tangu tupate uhuru tumeendelea kuwa maskini wa kutupwa,” alisema Dk. Slaa.

Alisema suala la nyumba duni linamgusa kila Mtanzania bila kujali itikadi za vyama na kuwahimiza wapiga kura kujitokeza kwa wingi Oktoba 31, mwaka huu, kuchagua viongozi wenye uchungu na maisha na wananchi.

Dk. Slaa, alisema wakati wananchi wa mkoa wa Rukwa na mkoa mpya wa Katavi wakiishi kwenye maisha ya dhiki, ndani ya nyumba zao wana mamia ya magunia ya mazao waliyovuna mashambani, lakini wameshindwa kusafirisha kutokana na miundombinu ya barabara kuwa mibovu.

Aliahidi iwapo wananchi watampa ridhaa ya kuingia Ikulu, serikali yake itahakikisha inawawezesha kujenga nyumba bora na za kisasa kwa kuwaondolea kodi kwenye vifaa vya ujenzi, kama bati na simenti ili ziuzwe sh 5,000 kama ilivyokuwa kabla ya uongozi wa awamu ya nne.

“Ukiwa na elimu bora kazi yoyote utaweza kuifanya kwa mafanikio na ubora unaokubalika hata ukiwa mama ntilie… hata kilimo chenye tija kitafanikiwa kwa kuwa na elimu bora. Ndiyo maana (CHADEMA) tunasema Elimu Bora Kwanza na siyo Kilimo Kwanza kama wanavyosema wenzetu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),” alisema Dk. Slaa.

Alisema bila kuwawezesha kielimu vijana wa Kitanzania, watageuka kuwa vibarua ndani ya nchi yao, baada ya kufunguliwa Soko la Pamoja la Afrika Mashariki.

Akiwahutubia wananchi wa mji wa Mpanda katika mkutano mwingine, Slaa alisema taifa limepoteza imani na Rais Jakaya Kikwete kwa sababu hana uchungu na nchi na amekuwa akishirikiana na mafisadi kutapanya rasilimali za nchi.

Dk. Slaa ambaye amekuwa akikumbushia jinsi alivyomtaja Kikwete miongoni mwa orodha ya mfisadi iliyotolewa Septemba 15, 2007, Mwembeyanga Dar es Salaam, alisema Kikwete anawalinda mafisadi, huku akijidai mbele ya umma kwamba anapigana na ufisadi.

Alimtaka Rais Kikwete atoe maelezo ya sh 29 bilioni, ambazo serikali ilipeleka TANROADS, ambayo imekuwa inatuhumiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma, ambazo nyingine zinasemekana kupelekwa kusaidia kampeni za CCM badala ya kujenga barabara zilizokusudiwa.

“Aseme hizi shilingi bilioni 29 zilizotolewa CRDB kwenda TANROADS zimejenga barabara gani? Tumepoteza imani na Rais. Anashindwa hata kusimamia barabara za nyumbani kwao, atawezaje kusimamia hizo anazoahidi kujenga kwingine?” alihoji.

Dk. alisema barabara ya Bagamoyo–Msata ambayo ilitengewa shilingi bilioni 12 kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) miaka mitatu iliyopita, kwa mkataba wa awali, haijajengwa, lakini Kikwete anaahidi barabara mpya kwingine bila kufuatilia ujenzi wa barabara hiyo.

“Aseme, walipewa ngapi, zimetumika ngapi, kwa nini mkataba umevunjwa…kama za jimboni kwake zimeliwa anatangaza za majimbo mengine…kwa nini tusiseme kuna ulaji wake katika barabara hizo?” alihoji.

Dk. Slaa alisema katika kudhihirisha kwamba Kikwete hayuko makini, anafanya njama kumrejesha ofisini Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Ephraim Mrema, ambaye amekuwa akilalamikiwa kwa tuhuma mbalimbali zinazohusu ubadhirifu wa fedha za barabara, huku zikiwapo tetesi kwamba aliwekwa pale ili kufanikisha kukusanya pesa za uchaguzi kwa ajili ya CCM.

Alisema amepata taarifa kuwa katika siku za karibuni, Rais Kikwete amemtonya Mrema kuwa ameagiza nafasi hiyo itangazwe gazetini ili kuwazuga watu wanaolalamikia uteuzi na utendaji wake.

“Kikwete amemwambia Mrema wa TANROADS kuwa ‘nimeagiza nafasi yako itangazwe ili kina Dk. Slaa wasipate hoja ya kuongea’, anamwambia chinichini…kumbe ndiyo maana Kikwete amekuwa akishindwa kuchukua hatua kila tulipomlalamikia bungeni kuhusu ufisadi TANROADS … sasa tunataka maelezo kutoka kwake,” alisema.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na wakazi wengi wa mji huo, Dk Slaa pia aliwaonya polisi kuwa makini katika kusimamia haki na amani katika uchaguzi huu.

“Nchi ikiingia katika machafuko CCM itapata laana, na polisi hamtabaki salama. Mwaka 2001, wananchi wa Zanzibar walipoteza maisha, wengine wakawa wakimbizi kutokana na kauli za viongozi wa CCM na polisi….CHADEMA tunataka uchaguzi wa amani na ulio huru. Amani ikivunjika historia itawahukumu,” alisema.

Dk. Slaa alikuwa akizungumzia vikundi vya vijana wa CCM ambavyo vimekuwa vikifanya fujo kwenye mikutano ya CHADEMA, na taarifa kuwa wana usalama wa taifa wamesambazwa nchi nzima kusaidia uchakachuaji wa kura.

Alisisitiza kuwa, kazi ya usalama wa taifa ni kulinda usalama wa taifa, si usalama wa CCM au wa Kikwete.

Alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kuwa kisheria, wana usalama hawaruhusiwi kukanyaga kwenye mikutano ya siasa au kwenye vituo vya kupigia na kuhesabia kura.

“Mkiwaona, kama hamuwawezi, tupigieni simu tuwashughulikie,” alisema.

Aliwaomba polisi na majeshi yote kujiepusha na siasa, na badala yake kufanya kazi yao kwa uadilifu usiopendelea upande wowote, kwa maana wanaweza kujikuta wanamtetea na kumlinda kiongozi ambaye hatashinda uchaguzi, jambo linaloweza kuwapatia msukosuko baada ya uchaguzi.
Tags:

0 comments

Post a Comment