Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - REDET yachafua hewa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter SIKU moja baada ya Taasisi ya Utafiti na Elimu ya Demokrasia Tanzania (REDET), kutoa matokeo ya kile kilichoitwa utafiti, hali ya hewa ya kisiasa imechafuka baada ya wananchi mbalimbali wakiwemo wataalam, wanasiasa na wanaharakati, kuupinga vikali utafiti huo, wakidai umepikwa kwa makusudi kukisaidia Chama cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 31.
Akitangaza matokeo ya utafiti huo juzi jijini Dar es Salaam, mmoja wa wakuu wa utafiti huo, Dk. Benson Bana, alisema utafiti huo uliowahoji watu 2600, umeonyesha kuwa Rais Kikwete ndiye anayepewa nafasi ya kushinda urais kwa asilimia 71.2 akifuatiwa na Dk. Willibrod Slaa wa CHADEMA.

Profesa Mwesiga Baregu, ambaye ni Mwenyekiti wa Kampeni za mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, akizungumza na vyombo habari jijini Dar es Salaam jana, alisema utafiti huo, umechakachuliwa kwa makusudi kumweka chini Dk. Slaa anayepewa nafasi kubwa ya kushinda ili kuwakatisha tamaa wananchi wengi wanaomuamini.

Alisema utafiti huo, bado hauwezi kumsaidia mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, wala CCM kurubuni wananchi, kwani wengi wameelimika na chama hicho kinaendelea na harakati zake za kuwaelimisha na kuwatia ujasiri kupitia mikutano ya kampeni inayoendelea. CHADEMA leo wanatarajiwa kutoa tamko rasmi kuhusiana na utafiti huo.

Kwa upande wake Chama cha Wananchi (CUF), kupitia Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Joram Bachange, jana kiliwataka Watanzania kutokubali kurubuniwa na badala yake waendelee kusikiliza sera za vyama, ambazo zinaweza kuwaletea ukombozi kwa kujenga uchumi ulio imara, unaoongeza ajira zenye tija na wenye kuleta neema kwa wote.

“Huo utafiti wao sisi hautusumbui, wao walikwenda kwa wenyeviti wa serikali za mitaa ambao tunajua kwa asilimia 93 zinaongozwa na CCM. Hivyo ni rahisi viongozi hao kuwapeleka watafiti wa REDET kwa wana CCM ambao ndio waliotoa maoni hayo.

“…Hawakuonyesha wasomi waliohojiwa ni wangapi, wafanyakazi wangapi, vijana na wakulima wangapi, mnyumbuliko wa jamii haukuwepo kwa kuwa hawakuonyesha wamemhoji nani, pamoja na maswali yaliyokuwa yanaulizwa. Tunawaomba wananchi wasikubali kuchaguliwa rais na REDET, waendelee na mchakato wa kumchagua kiongozi anayewafaa,” alisema Bachange.

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Xavery Lwaitama, ambaye pia ni mtaalam aliyebobea katika masuala ya tafiti, alisema matokeo ya REDET, sio kamili kwani hayakuainisha vitu ambavyo walivichukua.

Profesa Lwaitama, alisema matokeo hayo yalichukuliwa kwa kiwango cha chini na kushindwa hata kutambulisha waliohojiwa ni watu wa kada gani na wa umri gani na kuonyesha kuyatilia shaka kubwa matokeo hayo.

Mkoani Iringa wagombea wa nafasi za ubunge, wamewataka wananchi kupuuza utafiti huo kwa madai kuwa haupaswi kuaminiwa kwani REDET ni moja ya jumuiya za CCM.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, wagombea ubunge wa jimbo la Njombe Kaskazini Alatanga Nyagawa (CHADEMA), Godfrey Mohongole (CUF) walisema anapingana na REDET kwani asilimia hizo walizompa Kikwete ni maandalizi ya kuhalalisha wizi wa kura.

Hata hivyo, kila mmoja alisema chama chake kimejipanga vizuri kudhibiti hujuma na wizi wowote wa kura.

Aidha, wananchi mbalimbali wameendelea kutoa maoni yao kupitia tovuti ya mtandao maarufu wa ‘Jamii Forum’ kuhusu utafiti huo wa REDET, huku sehemu kubwa sana ya wachangiaji hao wakiwa wameupinga utafiti huo.

Katika mtandao huo wenye kauli mbiu ya “Unapoweza kunena kwa uhuru”, baadhi ya wachangiaji hao walitoa tuhuma nzito dhidi ya REDET wakidai kuwa viongozi wote wa juu wa taasisi hiyo wana uhusiano wa karibu sana na Rais Jakaya Kikwete akiwemo Dk. Benson Bana anayedaiwa kuwa mshauri mwenza wa mkuu huyo wa nchi.

Kama ilivyotarajiwa, Chama cha Mapinduzi (CCM), jana kilitangaza kuunga mkono utafiti huo, licha ya kulalamikia kupunjwa kidogo asilimia za viti vya ubunge wanavyotarajia kuvipata.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni za Rais Kikwete, Abdulrahman Kinana, aliyasifu matokeo ya REDET akidai kuwa yametoa mwelekeo chanya wa ushindi.

“REDET wametoa tathmini yao na sisi leo tunatoa yetu, mnajua uchaguzi ni hesabu na ushindi pia ni hesabu kwa matokeo haya ukizingatia kwamba kuna sehemu mgombea wetu hajafika, tunao uhakika wa kushinda kwa zaidi ya asilimia 80.

“…Tukifanikiwa kumaliza hizi wiki tatu za kampeni mgombea wetu atakua amefika kila mahali hivyo tutavuka takwimu za REDET,” alisema Kinana.

Juzi Mwenyekiti Mwenza wa REDET, Dk. Benson Bana, alitangaza matokeo hayo mbele ya waandishi wa habari na kusema Kikwete anaongoza kwa asilimia 71.2, akifuatiwa na Dk. Slaa kwa asilimia 12.3 huku mgombea urais kwa tiketi ya CUF, Profesa Ibrahim Lipumba akiambulia asilimia 10.1.
Tags:

0 comments

Post a Comment