Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Dk. Slaa atema cheche, atishia kuwafichua VIMADA wa Vigogo. ahoji kwa nini Makamba alifukuzwa ualimu miaka ya nyuma

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa amesema hakuna kiongozi yeyote wa juu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mwenye ubavu wa kumnyoshea yeye kidole katika masuala ya yanayohusu maisha yake binafsi.
Dk. Slaa alitoa maelezo hayo jana wakati akihutubia maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza kwenye uwanja wa mpira wa Kwara, uliopo Babati Mjini, mkoani Manyara wakati akiendelea na mikutano yake ya kampeni.

Mgombea huyo wa urais ambaye amekuwa akivuta umati mkubwa wa wasikilizaji katika maeneo mbalimbali anayopita alieleza kukerwa na tabia ya viongozi wa juu wa CCM akiwamo Katibu Mkuu wake, Yusuf Makamba kwa namna wanavyojaribu kumchafua kwa kuingilia masuala yake binafsi.

Akiwahutubia wananchi hao huku akishangiliwa muda wote wa hotuba yake, Dk. Slaa aliwataka viongozi hao wa CCM na wapambe wao kuacha kumchagulia mke wa kufunga ndoa naye kwani masuala yake binafsi ya maisha hayawahusu.

Akisisita Dk. Slaa mwanasiasa ambaye ana rekodi ya kipekee ya kurusha makombora mazito ya tuhuma dhidi ya CCM na viongozi wake ambayo takriban yote yamekuwa yakithibitika kuwa na ukweli alimtaka Makamba na wenzake kutambua kuwa amechukua fomu ya kugombea kiti cha urais wa nchi na si uaskofu wa kanisa.

Aliwageukia Makamba na vigogo wengine wa CCM wanaojaribu kuingilia ndoa yake akisema iwapo angekuwa akiutaka uaskofu wa kanisa basi alikuwa na uwezo wa kuupata miaka 20 iliyopita.

Alisema endapo Makamba na wenzake wataendelea kumsakama kuhusiana na maisha yake binafsi, atawalipua vimada wa vigogo wa juu wa CCM na jinsi wanavyotumia fedha nyingi za serikali kuwatunza.

Slaa ambaye alitumia mkutano huo wa hadhara kumtambulisha mkewe, Josephine alisema ameamua kuzungumzia maisha yake binafsi kutokana na Makamba na baadhi ya vyombo vya habari alivyosema vinatumika na CCM
kuzungumzia maisha yake binafsi, hususan ndoa yake na kufikia hatua ya kutaka kumchagulia mke.

“Niwaambie ukweli, Dk. Slaa hateswi na ndoa yake. Nani ananichagulia nifunge ndoa na nani. Hakuna mtu anayeweza kuingia katikati ya ndoa ya mtu mwingine. Nikisema nianze kuwalipua vigogo wenye nyumba ndogo (vimada) hapa, hakuna atakayesimama,” alisema Dk. Slaa kwa kujiamini na kushangiliwa.

Mgombea huyo wa urais alimgeukia Makamba na akamtaka ajitokeze hadharani na kueleza umma wa Watanzania ni kwa nini alifukuzwa kazi ya ualimu miaka ya nyuma.

“Mimi namtaka Makamba aseme hadharani, kwa nini alifukuzwa ualimu ni kwa sababu gani … mwache aendelee, nitaweka hadharani uchafu wao na nitaanza na Makamba
mwenyewe,” alisema.

Hii ni mara ya kwanza kwa Dk. Slaa kuweka hadharani msimamo wake tangu baadhi ya vyombo vya habari na vigogo wa CCM waanze kumshambulia kwa maisha yake binafsi.

Mbali ya kutoa kauli hiyo, Dk. Slaa pia alimtaka mke wa Rais Kikwete, Mama Salma kuacha kufuja fedha za serikali kwa kuwa na msafara mrefu wa magari ya serikali pamoja na askari wengi wa kumlinda.

Alisema mke huyo wa Kikwete ambaye jana alikuwapo mjini hapa na kufanya mikutano ya ndani ya CCM, anapaswa kutambua kuwa yeye si rais wa Tanzania kwani kwa sasa kuna rais mmoja tu.

“Mgombea urais wa CHADEMA, anatembea kwa basi, lakini mke wa rais anatembea na msafara wa magari 21, yenye thamani ya sh milioni 400 kila moja, ambazo ni sawa na fedha za kujenga zahanati nne, hili jambo ni la hatari sana na kulikomesha hili ni kutompigia kura Kikwete katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Akichambua sababu za kwa nini Kikwete hafai kuchaguliwa tena mwaka huu, Dk. Slaa alisema pamoja na ahadi nyingine, ameshindwa kutimiza ahadi yake ya maisha bora kwa kila Mtanzania.

Alisema katika kipindi cha uongozi wa Kikwete, maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mabaya kwani gharama za maisha hasa bei za bidhaa na huduma za jamii, zimeongezeka mara dufu na kufanya maisha ya wengi kuwa duni badala ya kuboreka.

“Bei ya sukari, nauli za mabasi, chumvi, nyama, soda na hata bia, zimeongezeka mara dufu katika kipindi chake cha miaka mitano. Aliingia madarakani kwa kuwadanganya Watanzania, leo anarudi tena kuomba ridhaa yenu ili awatumikie eti kwa kasi zaidi, nguvu zaidi na ari zaidi. Mwaka 2010, msidanganyike,” alisema Dk. Slaa.

Kuhusu ahadi za ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Mbeya kwa kiwango cha kimataifa, Dk. Slaa alisema ahadi hiyo ni ya uongo kwani kiwanja hicho kimefungwa na serikali imekuwa ikiahidi kukijenga kwa miaka 10 iliyopita bila mafanikio.

“Ahadi hiyo ni usanii mwingine. Hii ni Serikali ya wasanii, kiwanja kimefungwa kwa miaka 10 sasa, yeye anazungumzia kujenga kiwanja cha kimataifa, kwanza Shirika la Ndege la Taifa la (ATC), wamelifanyia ufisadi, wameua ndege zote,
hivyo viwanja vya ndege anavyoahidi leo kuvijenga kwa kiwango cha kimataifa, zitatua ndege gani kama Serikali yenyewe haina hata ndege moja?” alihoji Dk. Slaa na kushangiliwa na maelfu ya wananchi waliofurika kumsikiliza.

Akizungumzia nyongeza ya mishahara kiduchu waliyopewa wafanyakazi badala ya kiwango cha sh 315,000 walichopendekeza, Dk. Slaa aliwataka wasidanganyike na
kiasi hicho na kuamua kumpigia kura wakati alishatangaza kutozihitaji kura zao na badala yake wampigie kura kwani Ilani ya CHADEMA inazungumzia kuboresha mishahara na maisha ya wafanyakazi.

Kuhusu hatua ya CCM kumsimamisha Kisyeri Chambili aliyepata kuwa mbunge wa Tarime kugombea ubunge katika jimbo la Babati, Dk. Slaa aliwataka wananchi kuhoji rekodi yake.

Alisema Chambiri aliyebwagwa katika ubunge wa Tarime na marehemu Chacha Wangwe (CHADEMA), amekimbia jimbo la asili yake kwa kuwa anajua hawezi kushinda kutokana na rekodi yake isiyofaa.

“Chambili nilikuwa naye bungeni akiwa Mbunge wa Tarime, namjua ubovu wake na jinsi alivyoshindwa kuwatumikia wananchi wa nyumbani kwao alikozaliwa, leo amekuja kufanya biashara zake Babati anaomba kura kwenu. Muulizeni aliwafanyia nini Tarime,” alihoji.

Badala yake aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea ubunge wa CHADEMA, Pauline Gekul, kwani ni mwanamke msomi, jasiri mwenye uwezo wa kuliongoza jimbo la Babati Mjini na Francis Qamara anayegombea udiwani.

“Nawaombeni mnipe kura zetu Oktoba 31 na vijana hawa, Pauline na Francis na madiwani wao ili tuweze kufanya kazi nzuri kama tuliyoifanya Karatu,” alisema.

source: http://www.freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=18974
Tags:

0 comments

Post a Comment