Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Cheyo atemwa uwaziri kivuli

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter KAMBI ya upinzani kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano imemvua mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo cheo cha Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi baada ya kupiga kura ya kuunga mkono bajeti ya serikali ya mwaka 2010/11.

Cheyo, ambaye ni mwenyekiti wa UDP, pamoja na Shoka Hamisi Shoka wa CUF waliungana na lundo la wabunge wa CCM kuipigia bajeti hiyo ya Sh11.1 trilioni kura ya kuipitisha licha ya kuwepo mapungufu kadhaa yaliyolalamikiwa na kambi ya upinzani. 

Pamoja na kwamba mkutano huu ni wa mwisho kwa Bunge hili, kambi hiyo imeshamteua Ali Said Salim, ambaye ni mbunge wa Ziwani (CUF), kuchukua nafasi ya Cheyo. Awali Salim alikuwa naibu waziri katika wizara hiyo.
Kambi hiyo ya upinzani imesema imeamua kumwondoa Cheyo kwenye wadhifa huo kwa kuwa amesaliti makubaliano ya ya kupinga bajeti ya serikali ambayo ilipitishwa na wabunge 220 juzi jioni.

Katika kura ya wazi iliyopigwa bungeni juzi jioni, Cheyo alipotakiwa kueleza anaikubali au kuipinga, alijibu “ndiyo” na hivyo kuwa mmoja wa wabunge 220 waliopitisha bajeti hiyo, inayolaumiwa kwa kutoweka vyanzo vipya vya mapato huku ikiweka misamaha ya kodi kwa makampuni ya migodi.

Shoka Hamisi Shoka wa jimbo la Micheweni kwa tiketi ya CUF, pia alichukuliwa kuwa ameipitisha bajeti hiyo, jana alikanusha akisema kuwa alijibu "siyo" na hivyo kunukuliwa vibaya.

Kiutar
Cheyo habari kamili soma pembeni
atibu, mbunge hutakiwa kutoa jibu la "ndiyo" anapokubaliana na bajeti hiyo au jibu la "hapana" anapoipinga.

Hata hivyo, Cheyo amepinga uamuzi wa kumvua wadhifa wake akisema kuwa kiongozi huyo wa kambi ya upinzani hana mamlaka hayo.

“Hamad hana uwezo wa kuniondoa... mimi si CUF. Muungano ndio unaniweka pale na si Hamad... tuligawana majukumu... sababu aliyotoa ni ‘nonsense’ (haina msingi)”.

Alisema amepokea nakala ya barua ya Hamad aliyoiandika kwenda kwa Spika wa Bunge, Samuel Sitta ikieleza uamuzi huo, lakini akasema anaandaa barua kwenda kwa kiongozi huyo wa Bunge kuelezea suala hilo na kusisitiza kuwa yeye ndiye msemaji wa kambi ya upinzani kwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Naandika barua kwenda kwa spika kwa kuwa hili limefanyika kinyume,” alisema Cheyo.

Lakini kiongozi huyo wa kambi ya upinzani, Hamad Rashid Mohamed (CUF) alisema amefanya mabadiliko kwa mujibu wa sheria ya Bunge.

"Maamuzi ya baraza la mawaziri ni ya kikatiba. Usipokubaliana nayo unajiuzulu, usipojiuzulu unawajibishwa. Cheyo amekwenda kinyume na maamuzi ya kambi ya upinzani hivyo kwa mamlaka niliyonayo kwa kutumia kanuni ya 15(2) ya Bunge, nimemwondoa Cheyo katika nafasi yake ya Waziri Kivuli wa Ardhi,” alisema Hamad.

Hamad, ambaye alikuwa pamoja na na naibu kiongozi wa kambi hiyo Dk Willibrod Slaa na Shoka Hamis Juma wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, alisema hatua ya kumuondoa Cheyo inaonyesha jinsi walivyo makini katika kutekeleza makubaliano wanayojiwekea kwenye utendaji wao.

Cheyo alionekana kufahamu mapema uamuzi wa kumuondoa na alidhihirisha hilo hata kabla ya kutangazwa kuvuliwa madaraka wakati alipodokeza suala hilo aliposimama kuchangia muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2010/2011 iliyowasilishwa bungeni jana.

Alisema: “Najua naweza kuondolewa kwenye kambi ya upinzani, lakini nataka kusema, tujifunze kuweka mbele maslahi ya taifa. Hii ni ‘vote’ (hoja) yangu, haiwezekani nipiganie kurejeshwa kwa Sh8bilioni za CAG, zirudi nami nipinge bajeti.”
Naibu spika wa bunge Anne Makinda 

alimwambia Cheyo kuwa “watu walichukia sana jana”.
Lakini Cheyo alijibu: “Shauri yao, najua naweza kuondolewa kambi ya upinzani.”

Baadaye mbele ya waandishi wa habari, Cheyo alisema suala la yeye kupiga kura ya kupitisha bajeti hiyo ni la mtu binafsi na siyo la kambi ya upinzani.

Alikejeli kuwa waliopiga kura ya kuikataa, hawakufanya kitu kilichotoka moyoni na kwamba haitashangaza kuona walioipinga ndio wakiwa wa kwanza kwenda kudai mafao ya ubunge.

“Ukiondoa UDP hakuna kambi ya upinzani; “no yao” (hapana) yao haitoki moyoni bali ndiyo yangu. Na wao ingawa walipinga, watakuwa wa kwanza kwenda kudai mafao yao ya kustaafu ubunge,” alisema Cheyo.

Naibu kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Dk Willibrod Slaa alieleza kushangazwa kwake na hatua ya Cheyo kulalamika bungeni hatua ya kuvuliwa wadhifa huo.

“Tangu nikue na kupata akili, ni mara ya kwanza kuona, waziri (Cheyo) akiondolewa, anaenda kulalamika bungeni,” alisema Dk Slaa.
Tags:

0 comments

Post a Comment