IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MGOGORO wa Tucta na serikali umechukua sura mpya baada ya baraza kuu la shirikisho hilo la wafanyakazi kuibuka na hoja kwamba nyongeza ya kima cha chini ya sekta binafsi iliyotangazwa na Waziri Juma Kapuya imeshusha kiwango kilichotangazwa mwaka 2007.
Kauli hiyo ya Tucta imetolewa baada ya baraza kuu kujifungia kwa siku nzima ya jana kujadili ripoti ya matokeo ya mazungumzo baina ya serikali na shirikisho hilo yaliyofanyika Jumamosi iliyopita ambayo yanatarajiwa kutoa picha halisi ya mgomo wa wafanyakazi wote ambao awali ulipangwa kuanza Mei 5.
Tucta pia jana haikuweza kutoa tamko la mgomo kwa maelezo kuwa inasubiri kuisha kwa siku 21 ambazo kwa mujibu wa sheria, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Kapuya anapaswa kutoa tamko la makubaliano yaliyofikiwa.
Shirikisho hilo limesema limeashaanza kuhesabu siku hizo tangu kuisha kwa mkutano huo wa Mei 8.
Tucta imeeleza kuwa kama waziri atashindwa kufanya hivyo katika kipindi hicho, Tucta itakuwa kwenye nafasi ya kutangaza mgomo.
Naibu katibu mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya alisema jana jijini Dar es salaam kuwa baraza hilo limebaini upungufu katika baadhi ya vipengele vya ongezeko la mishahara ya sekta binafsi ambavyo vinapingana na tangazo la ongezeko la kima cha chini cha mshahara la mwaka 2007.
Kutokana na hali hiyo, Mgaya alisema Tucta ilishirikiana na wanasheria wake kupitia upya tangazo la Waziri Kapuya na kubaini kuwa halikufuata taratibu za kisheria ambazo ni pamoja na kutowashirikisha wajumbe wa bodi ya mishahara ya kisekta.
Kwa mujibu wa Mgaya, Waziri Kapuya alipaswa kutangaza kima cha chini cha mishahara baada ya kupokea ushauri na mapendekezo kutoka kwenye bodi za kisekta za mishahara ambazo ndizo zinazotoa mwongozo.
Alisema matokeo ya kosa hilo la kiufundi ni viwango vya mishahara ya sekta binafsi mwaka huu kushuka, ikilinganishwa na viwango vya mishahara vilivyotangazwa mwaka 2007.
“Tucta inapingana na tangazo la serikali la kuongeza viwango vya mishahara kwa sekta binafsi kwa sababu baadhi ya vipengele vinaonyesha wazi kuwa mishahara ya wafanyakazi imeshuka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na tangazo lililotolewa mwaka 2007,” alisema Mgaya.
Mgaya alitoa mfano kuwa kiwango cha kima cha chini cha mishahara cha sekta ya viwanda na biashara cha mwaka 2007 kilikuwa Sh150,000, lakini katika tangazo la Waziri Kapuya kiwango hicho kimeshuka hadi Sh80,000.
Alisema katika tangazo hilo jipya, serikali pia imefuta baadhi ya marupurupu ya wafanyakazi wa sekta hiyo na nyingine, ikiwa ni pamoja na posho ya nyumba, chakula, likizo na usafiri.
"Mabadiliko hayo ya mishahara yanaweza kuzua mgogoro katika maeneo ya kazi, jambo ambalo linaweza kusababisha kuvunjika kwa mahusiano kazini baina ya waajiri na waajiriwa," alisema Mgaya.
"Kutokana na hali hiyo, utendaji wa kazi wa wafanyakazi hao unaweza kupungua kwa sababu wataaamini kuwa waajiri wao wanashindwa kutetea maslahi ya wafanyakazi wake."
Alibainisha kuwa migogoro mingi inayotokea katika baadhi ya maeneo ya kazi, inatokana na maboresho yasiyoridhisha ya mishahara na hivyo serikali ilipaswa kuliangalia suala hilo kwa undani kabla ya kutoa tangazo lake.
Alisema baada ya kubaini upungufu huo baraza la Tucta limeahidi kutoa tamko hivi karibuni baada ya kukaa na bodi na kupitia upya ajenda hizo mbili za nyongeza ya mishahara na mkutano wa Mei 8 ambachpo kitafanyika kesho.
"Kikao hicho kitajadili mikakati iliyoafikiwa baina ya Tucta na serikali katika kikao cha utatu cha majadiliano kilichofanyika tarehe 8 mwezi huu ambayo kwa mujibu wa sheria, Waziri Kapuya anapaswa kutoa taarifa ya makubaliano yaliyofikiwa ndani ya siku 21," alisema.
Awali mgomo wa wafanyakazi ulipangwa kuanza Mei 5, lakini ukaahirishwa kusubiri kikao cha mwisho baina ya serikali na viongozi wa shirikisho hilo kilichofanyika Mei 8.
Tucta, pamoja na mambo mengine, iliitisha mgomo huo ikidai kuwa serikali imekuwa ikipuuzia madai yao ya muda mrefu ambayo ni pamoja na punguzo la kodi inayokatwa kwenye mishahara, kuboreshwa kwa mafao ya uzeeni yanayotolewa na mifuko ya hifadhi ya jamii na nyongeza ya kima cha chini cha mishahara ya sekta zote.
You Are Here: Home - - Tucta sasa yamwumbua Waziri Kapuya
0 comments