IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
HOMA ya uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani inazidi kupanda kila siku katika maeneo mbalimbali nchini, na hususan katika Jimbo la Mtera.
Dalili za kuzidi kupanda kwa homa hiyo zilijidhihirisha jana baada ya wazee 48 wa jimbo hilo lililoko mkoani Dodoma kujitokeza hadharani na kueleza kupinga uamuzi wa mkongwe wa siasa nchini, John Malecela, wa kutaka kuendelea kuwa mbunge wao kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Wazee hao waliokuwa wakizungumza na waandishi wa habari katika baa maarufu ya Kibarua eneo la Uhindini mjini Dodoma walijitambulisha kuwa wanachama wa CCM, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Chama cha Wananchi (CUF) na Tanzania Labour Party (TLP) walisema Malecela ambaye amekuwa bungeni kwa miaka 35 sasa amechoka kiakili na kimbinu.
Uamuzi wao wa kuzungumza katika baa ya Kibarua umekuja miezi kadhaa baada ya wazee wengine wanaomuunga mkono Malecela kulitumia eneo hilo hilo kutetea uamuzi wa mbunge huyo kuendelea kugombea.
Katika maelezo yao, wazee hao mbali ya kumtaka Malecela kung’atuka kwa kuachana na mikiki mikiki ya siasa ya majukwaani, walimshauri awe mshauri wa masuala ya kisiasa.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wenzake alioandamana nao, Moses Masaka aliyetambulishwa kuwa ni msemaji wao, alisema Malecela anapaswa kupumzika kwa kuwa amekuwa kiongozi wa juu kisiasa nchini tangu serikali ya awamu ya kwanza.
“Tunaamini wazi kuwa kipindi chote alichokaa madarakani kinatosha kabisa, amechoka anapaswa kuwaachia wengine akapumzike na kuwa mshauri wa masuala ya siasa jimboni,” alisema Masaka.
Mzee huyo alisema inasikitisha na kushangaza kuona Malecela bado akijinadi kutaka kugombea nafasi ya ubunge huku akiwa kiongozi wa siku nyingi ambaye ameshindwa kuwaletea maendeleo yanayofanana na kipindi kirefu alichoongoza.
Alisema pamoja na Malecela ambaye amepata kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kujinadi kuwa kazi ya siasa siyo kazi ngumu kama vile kubeba zege, ukweli unabaki pale pale kuwa kila jambo linafanyika kwa kutegemea umri pamoja na mazingira ya wakati husika.
Alibainisha kuwa wana Mtera wana kila sababu ya kubadilisha mwelekeo na kuchagua mbunge mwingine mwenye mawazo na nguvu mpya ili kuliendeleza gurudumu la maendeleo.
Wazee hao walikwenda mbali na kumuomba mmoja wa makada wa CHADEMA anayejulikana kwa jina la John Lameck kujitokeza na kugombea nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa wazee hao walioonekana wakiwa na ajenda ya kumuunga mkono Lameck ambaye ni mtu mwenye msimamo tofauti na viongozi wengine ambao wamekuwa wakiyumbishwa kwa tamaa zao na kujikuta wanawasaliti waliowaweka madarakani na kuwafanya kuwa maskini wa kutupwa.
Alipoulizwa kuhusiana na madai ya wazee hao, Malecela alisema yeye haogopi mtu yeyote atakayejitokeza kupambana naye kwa kuwa anaamini wananchi wa jimbo hilo ndiyo watakaopima kazi na maendeleo aliyoyafanya.
Alisema wakati huu taifa linapoelekea uchaguzi mkuu, kila mtu ana haki na wajibu wa kuingia kwenye siasa pamoja na kutangaza nia lakini mwisho wa yote wapiga kura ndiyo waamuzi.
“Kwa mtu anayekataa maendeleo ya Mtera anapaswa kuzungumzia jimbo la Mtera na kujionea maendeleo ya zahanati, shule za msingi na sekondari nilizojenga,” alisema Malecela.
Alisema kukosekana kwa barabara za lami jimboni humo, si kosa lake bali ni suala lililoko chini ya Wizara ya Miundombinu ambayo imepewa jukumu la ujenzi huo.
You Are Here: Home - - Miaka 35 ya ubunge wa Malecela yageuka kero
0 comments