Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Meya katika hati ya kuvuliwa uanachama

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter MEYA wa Manispaa ya Sumbawanga, Frank Mrema yupo katika hatari ya kuvuliwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kile kinachodaiwa kukabiliwa na kashfa ya wizi wa fedha za pembejeo za kilimo katika mfumo wa vocha za ruzuku zenye thamani kati ya Sh milioni 300 hadi 600.

Habari za ndani kutoka kwa uongozi wa juu wa CCM mkoa zimebainisha kuwa, kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM mkoa huo kilichopangwa kufanyika kesho na ambacho kinatarajiwa kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ndicho kitakachobariki kuvuliwa uanachama kwa mwanasiasa huyo.

Baadhi ya viongozi hao kwa nyakati tofauti wameeleza kuwa Meya huyo ataondolewa rasmi katika chama hicho hivyo kupoteza nyadhifa zake mbalimbali za kisiasa zikiwemo za udiwani na umeya wa manispaa ya Sumbawanga.

Mrema, ambaye ni Diwani wa Kata ya Katandala mjini Sumbawanga, huenda akakumbana na hali hiyo, licha ya mara kadhaa kuombwa na uongozi wa CCM mkoa kujiuzulu nafasi ya umeya, ikiwa ni ishara ya kuwajibika na kutoa fursa ya kuchunguzwa na mamlaka husika.

Habari za uhakika zinaeleza kuwa baada ya mwanasiasa huyo kuonyesha ukaidi huo kwa chama hicho, uongozi wa CCM mkoa ulimvua umeya na kupeleka taarifa kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Yusuf Makamba ambaye alitengua maamuzi hayo kwa madai kwamba taratibu za kumng'oa katika nafasi hiyo zilikiukwa.

Kutokana na hali hiyo, CCM mkoa ndani ya siku tatu ililazimika kumwandikia tena barua Meya huyo ya kutengua maamuzi yake ya awali huku ikifuata taratibu za kuhakikisha anaondolewa katika nafasi hiyo, ikiwa ni hatua mojawapo ya kukisafisha chama hicho kutokana na kashfa hiyo kubwa ambayo tayari imesababisha kufukuzwa kazi kwa aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Thobias Sijabaje.

Mkuu huyo wa wilaya alifukuzwa kazi na Rais Jakaya Kikwete kwa kushindwa kusimamia kikamilifu usambazaji wa mbolea ya ruzuku katika mfumo wa vocha kwa wakulima kwenye wilaya hiyo katika kipindi cha msimu huu wa kilimo ambapo kashfa kama hiyo ndio inayomtafuna meya huyo ambaye kwa sasa amekalia kuti kavu.

Chanzo cha habari cha uhakika kutoka CCM mkoa huo, kilisema kuwa siku za karibuni kiliwaeleza wanahabari kwamba wanachama wa CCM wenyewe ndio wamekuwa na msukumo wa kutaka kuondolewa kwa meya huyo chamani baada jitihada za awali za chama hicho kugonga mwamba wakihofia iwapo atabaki ataendelea kukichafu cha hicho na kuwapa nafasi wapinzani ya kukipaka matope chama hicho kongwe hususani kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

'Chama kimejiridhisha kuwa mwanasiasa huyo anabiliwa na tuhuma hizo nzito za ubadhirifu wa fedha za mbolea ya ruzuku katika mfumo wa vocha, tumemuomba ajiuzulu.... amegoma sasa hatuwezi sote kuchafuka kwa ajili mwanachama mmoja asiyekuwa mwaminifu, lazima tumvue uanachama kisha awajibishwe' kilisema chanzo hicho.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Hipolitus Matete akihojiwa juu ya kashfa hiyo inayomkabili Mrema alisema kuwa ni mapema mno kuzungumzia suala hilo.

Kwa upande wake Meya Mrema akihojiwa kwa njia simu jana kutoka mjini Sumbawanga, alisema kuwa hakuna kitu na hayo yanayozungumzwa ni majungu ya kisiasa na anaweza kukabiliana nayo.

'"Ni kweli chama kilinitaka nijiuzulu lakini nilikataa kwa sababu ni hizo zinazonikabili na kwamba mie sijakikaidi chama isipokuwa natetea haki zangu kama mwanachama ........ inastaajabisha kama wakala katika kata yangu niliuza nilisambaza kwa wakulima vocha zenye thamani ya milioni 21 hivi, hii tuhuma ya kwamba nimeiba vocha zenye thamani ya Sh milioni kati ya 300 hadi 600 inatoka wapi?" alihoji meya huyo.
Tags:

0 comments

Post a Comment