IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAKATI zikiwa zimebakia siku nne kabla ya kuanza kwa mgomo wa wafanyakazi wote ulioitishwa na Tucta, serikali jana ilitangaza viwango vipya vya kima cha chini cha mshahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi, lakini hali inaonekana kuwa ngumu kwa wafanyakazi wa serikalini.
Awali Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Prof Juma Kapuya alitangaza kuwa serikali ingetoa tamko kuhusu kima cha chini cha mshahara wa wafanyakazi wa serikalini kabla ya Mei mosi, lakini hakuweza kufanya hivyo jana na badala yake aliibuka na mishahara ya sekta binafsi.
Lakini, jana Kapuya alisema walikuwa wakiendelea na mazungumzo kati ya serikali na wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi kwenye kikao cha utatu kilichoitishwa na Baraza la Upatanishi (Lesco), ili kujadili hoja hizo saba zilizotangazwa na Tucta.
Waziri Kapuya aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa tamko namba 233 la serikali la kima cha chini cha mshahara lililotolewa mwaka 2007 limefutwa na kuanzia leo linatumika tamko jipya namba 172 la kima cha chini cha mshahara la mwaka 2010.
Alisema viwango hivyo vya mishahara ya wafanyakazi wa sekta binafsi, linawagusa wafanyakazi wote katika sekta hiyo.
Profesa Kapuya alisema kuwa katika sekta ya kilimo kima cha chini cha mshahara ni Sh70,000 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh50,000, wakati sekta ya biashara na viwanda kima cha chini ni Sh80,000, kima cha chini kwa sekta ya mawasiliano na usafirishaji wa huduma za anga mshahara ni Sh350,000 na wasafirishaji wa mizigo (clearing and forwarding) ni Sh230,000.
Kwa mujibu wa tamko hilo, kima cha chini kwa sekta ya mawasiliano ya simu ni Sh300,000, wakati kima kipya cha chini kwa sekta ya usafiri wa nchi kavu (makondakta na madereva) Sh150,000 na meli za uvuvi ni Sh165,000.
Wafanyakazi wa majumbani wamegawanywa katika makundi matatu ambayo ni wanaofanya kazi kwa mabalozi kima cha chini ni Sh90,000; wanaowafanyia maofisa wanaolipiwa huduma hiyo na waajiri wao ni Sh 80,000 na wengine Sh65,000.
Kima cha chini kwa wanaofanya kazi za hoteli za kitalii ni Sh150,000 na hoteli za kati Sh100,000 wakati hoteli ndogondogo, baa, nyumba za wageni na migahawa ni Sh80,000.
Katika sekta ya madini, upande wa migodi mikubwa, wafanyakazi watalipwa Sh350,000, wachimbaji wadogo, ambao walikuwa wakilipwa Sh80,000, sasa watalipwa Sh150,000, wakati kima cha chini kwa sekta ya biashara na usafirishaji madini ni Sh250,000, huku madalali katika sekta ya madini wakilipwa Sh150,000.
Katika sekta ya biashara na viwanda, kima cha chini ni Sh80,000, sekta ya ulinzi binafsi, kampuni za kigeni ni Sh105,000 na kampuni nyingine Sh80,000, huku kima cha chini kwenye huduma ya afya kikipangwa kuwa Sh80,000
Alisema katika sekta ambazo hazikutajwa, kima cha chini kitakuwa Sh80,000.
Profesa Kapuya alisema mwajiri haruhusiwi kulipa chini ya viwango vilivyotajwa, lakini anaweza kukiongeza kwa kadri anavyopenda ili kuboresha hali za wafanyakazi wao.
“Waajiri wajitahidi kutekeleza kama vilivyotangazwa na serikali ili kuepusha migogoro mbalimbali sehemu za kazi,” alisema Profesa Kapuya.
Kuhusu mgomo wa wafanyakazi wote uliopangwa kuanza Mei 5, Kapuya alisema serikali ilikuwa inaendelea na mazungumzo na Tucta juu ya kima cha chini cha wafanyakazi wa serikalini. Awali, Kapuya aliahidi kutoa tamko hilo kabla ya Mei mosi.
You Are Here: Home - - Mchanganuo mshahara kima cha chini watangazwa
0 comments