IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
BUNGE la Muungano limedhiria kwa pamoja Azimio la Itifaki ya Pamoja la Soko la Jumuiya ya Afrika Mashariki huku kukiwa na shaka kubwa katika itifaki hiyo.
Azimio hilo lilipitishwa kwa msaada mkubwa wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na Spika wa Bunge, Samuel Sitta ambao muda wote walikuwa wakiwasihi wabunge wasikumbuke vidonda ilivyopata Tanzania katika mkutano wa Doha .
Pamoja na ushawishi mkubwa kutoka kwa viongozi hao, lakini mbunge wa Kahama, James Lembeli alionyesha wasiwasi wake na kutamka kuwa anaunga mkono kwa shingo upande hali iliyoonyesha kuwa hakuridhika lakini haikuwa busara kupingana na Waziri Mkuu.
“Mbele ya safari ni kiza kinene kwani ndoa hii ina shaka sana inaweza kuvunjika muda na wakati wowote kwani inaniuma sana kuona serikali iko kimya hata baada ya mkutano wa Doha imeshindwa kukemea tatizo hilo, ” alisema Lembeleli
Mbunge huyo alisema yako meno ya tembo ambayo yanaigharimu serikali kiasi cha Sh 200 milioni kwa ajili ya kuyatunza kwa kila mwaka, lakini walipotaka kuyauza Wakenya walisingizia kuwa yakiuzwa pesa zake zitatumika kufanyia kampeni za uchaguzi.
Mashaka ya wabunge hao yalielekezwa moja kwa moja katika nchi ya Kenya ambayo walisema imekuwa haionyeshi ushirikiano wa dhati na majirani na kwamba inaoyesha kuwa na tamaa kwa vitu ambavyo vinatoka Tanzania .
Msuguano wa wabunge ulianzia katika semina iliyoitishwa na jumuiya hiyo ambapo Wabunge walichachamaa na kumtaka rais kukataa kupitisha azimio hilo licha ya kuwa rais alishasaini mkataba wa ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Mbunge wa Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe aliwataka wabunge wakubaliane kwa pamoja kupitisha azimio hilo kwa madai kuwa kama Watanzania wataogopa watakuwa wanaonyesha woga kuingia katika soko hilo la ushindani.
Kabwe aliwataka wabunge wawe makini katika kujadili jambo hilo kwa masilahi ya wananchi wao na akatahadharisha kuwa wanasiasa na wafanyabiashara wa Kitanzania wote wamekuwa wakiongea lugha ya woga kwa kuwaogopa Wakenya tu.
Kwa upande wake Rymond Mrope alisema kuwa kitendo kiichofanywa na Wakenya katika mkutano wa Doha hakivumiki na akasema ujirani wao siku zote ni ujirani wa mashaka.
“Ujirani wetu na Wakenya siku zote ni ujirani wa mashaka na hapa tunasema kuwa tukijibu mapigo hawa jamaa wataumia sana lazima wafahamu kuwa ujirani wowote ni kufaana waambieni” alisema Mrope.
Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango Malecela yeye alitahadharisha serikali kuhusu azimio hilo ambapo alisema tayari Wakenya walishaanza mapema kuingia katika soko hilo kwani alisema kabla ya kuridhiwa lakini vijana wengi wa nchi hiyo wanafanya kazi Tanzania .
“Kabla hata ya kipenga kulia lakini Wakenya walishaanza kucheza mpira hii ni aibu kubwa sana tena wanawafedhehesha wananchi wetu kwa kusema eti hawajui kuongea Kingereza bila ya kujua kuwa sisi tunazungumza Oxford yenyewe kuliko hata wao, nasema watimuliwe kwanza ili tuanze utaratibu mpya” alisema Kilango.
Mbunge huyo pamoja na Dk Binilith Mahenge waliitaka serikali kuachana kabisa la suala la ardhi kuingia katika mfumo huo kwa madai kuwa nchi tano zinazoingia katika soko hilo ni Tanzania peke yenye ardhi.
Katika mchango wake mbungewa kuteuliwa na rais Ismail Jusa Radu alionyesha wasiwasi katika Azimio hilo kwani alisema hauonyesha wazi sehemu ya Zanzibar katika soko hilo itakuwa wapi.
Akitoa majumuisho ya michango ya wabunge Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk Diodorus Kamala aliwata wabunge kutokuwa na mashaka juu ya Azimio hilo kwa kusema kuwa Tanzania itakuwa makini katika masuala yote yanayohusu masilahi ya nchi.
Kuhusu suala la ardhi Kamala alisema kuwa hilo halitawezekana kutokana na ukweli nchi nyingi za jumuiya hiyo hazina ardhi hivyo zinaweza kuchukua ardhi ya Watanzania kama viongozi hawatakuwa makini.
You Are Here: Home - - Bunge laridhia Itifaki ya soko la Pamoja
0 comments