IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
LICHA ya kutangaza kutogombea urais mwaka 2010, waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye bado anatajwa katika anga za kisiasa baada ya kuelezewa kuwa ni mmoja wa watu wanaoweza kujitokeza kupambana na Jakaya Kikwete katika kinyang'anyiro cha urais.
Sumaye, ambaye alikuwa waziri mkuu kwa kipindi cha miaka kumi, alijitokeza kuwania kuteuliwa na CCM kuwania nafasi hiyo mwaka 2005, lakini hakuweza kufua dafu.
Baada ya kumalizika kwa uchaguzi, alikwenda masomoni nchini Marekani na aliporejea aliweka bayana kwamba elimu yake ya juu zaidi aliyokwenda kuipata haikuwa na uhusiano na urais wa 2010 na mara kwa mara amekuwa akisisitiza kutokuwa na mpango wa kugombea kiti hicho mwaka huu.
Alisema hata utaratibu wa CCM wa kumuachia mshindi wa kiti cha urais kuachiwa aendelee ngwe ya pili, unamzuia kujitokeza kuwania urais.
Lakini, taarifa za kuaminika kutoka vyanzo mbalimbali zinasema Sumaye ni mmoja wa watu wanaoweza kubadili hali ya kisiasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi wa Oktoba mwaka huuu.
Alipoulizwa jana kwa njia ya simu, alisema: "Nimetoa msimamo wangu mara kwa mara kuhusu jambo hili (la urais), kwa hiyo kama kuna watu wananitaja na kuniona nafaa, mimi nasema bado sijawaona wala kuwasikia."
Sumaye, ambaye alizungumza katika hali inayoashiria kuwa ni mwenye furaha, aliongeza: "Kama wakitokea watu wakiniambia nigombee urais, nitawauliza kwa nini wanataka mimi nigombee; wanafikiri nina kitu gani ambacho naweza kukifanya?"
Alipoulizwa kama kutatokea watu na kumtaka abadili msimamo wake ili aweze kugombea urais, alicheka kisha akajibu: "Aaaa... sasa tatizo hao watu hawajajitokeza na kuniambia hivyo, wangekuwa wapo tayari ningeweza kuwapa jibu baada ya kuwauliza.
"Pia ningeweza kuwa na jibu kwako, lakini siwezi kujibu kitu kwa jambo ambalo sijalipata rasmi wala sijui ni nani anazungumza hivyo, ila wakiniambia siku nitawapa jibu."
Huku akiendelea kucheka Sumaye alihoji : "Au wewe (mwandishi) ndiyo unataka mimi Sumaye nigombee urais? Ninachoweza kusema hadi sasa sijamsikia mtu akitaka nigombee urais. Ila wewe kama ndiyo unasema Sumaye nigombee urais sawa ni maoni yako."
Sumaye alisema anafahamu kuwa hadhi yake ni mali ya umma na umma unaweza kumwomba afanye kitu fulani, lakini bado alisisitiza: "Sijawasikia hao watu wanaonitaja mimi nigombee urais."
Sumaye alisema hadi sasa bado yuko CCM na kwamba kama kuna mipango yoyote ni ile inayofuata taratibu za chama. Waziri mkuu huyo mstaafu alisema kwamba umma ni sehemu kubwa na kwamba hadi sasa hajaelewa genge hasa ambalo linamtaka yeye kugombea nafasi hiyo na mantiki inayokusudiwa.
Vyanzo vyetu vimebainisha kuwa uamuzi wa kumtaka agombee kiti hicho ni ombi maalumu kutoka kundi maalumu la watu wa kada mbalimbali nchini. Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, tayari kundi hilo limejipanga vema ikiwa ni pamoja na kufanya hadi utafiti kuhusu asilimia za kura za urais ambazo Sumaye anaweza kuzipata kama ataingia katika kinyang'anyiro hicho kwa kumvaa Rais Kikwete.
Ingawa tafiti mbalimbali ikiwemo za Synovate zinamuonyesha Rais Kikwete kuweza kupata asilimia zaidi ya asilimia 50 katika uchaguzi ujao, vyanzo hivyo vinaonyesha kama Sumaye ataingia anaweza kupata asilimia 40 ya kura za urais huku Kikwete akipata asilimia 52.
Vyanzo hivyo vya habari vilifafanua kwamba Sumaye amekuwa akiandaliwa mipango mbalimbali ambayo kwa sasa imefikia katika hatua ya juu ya kiutekelezaji kumwezesha kutimiza azma hiyo ya kumvaa Kikwete.
Katika taarifa hizo, vyanzo hivyo vinasema Sumaye anaonekana kuwa mtu makini na mwenye maono na ana uzoefu unaoweza kuleta changamoto kubwa za maendeleo kutokana na kukaa madarakani akiwa ni waziri mkuu kwa kipindi kirefu cha miaka 10.
Siku za karibuni Sumaye amekuwa akijitokeza hadharani katika matukio mbalimbali na hata mwishoni mwa mwaka jana alishiriki kikamilifu katika kongamano la hali ya kisiasa nchini lililoandaliwa na Taasisi ya Mfuko wa Mwalimu Nyerere na kufanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Katika kongamano hilo Sumaye alikuwa akitaka kusomwa kwa maazimio yaliyotolewa na wananchi bila kuchelewesha, lakini mwenyekiti wa kongamano, Dk Salim Ahmed Salim alishauri ufanyike uhariri kidogo kutokana na maazimio hayo kuwa makali zaidi kwa serikali ya Rais Kikwete.
Kongamano hilo hadi sasa limebaki kuwa tukio kubwa ambalo serikali na CCM iliwaelezea waliohudhuria kwamba ni watu ambao walikuwa na chuki kutokana na kukosa madaraka baada ya uchaguzi wa chama wa mwaka 2005.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, kundi hilo la watu mashuhuri wakiwamo viongozi wa dini, wanasheria, wanaharakati na viongozi wa vyama vya upinzani wamekwishaweka mkakati maalum wa kumshauri Sumaye kugombea urais kupitia chama kimojawapo cha upinzani.
Hatua hiyo ya kumshauri Sumaye kugombea inaweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya CCM na hata wale ambao watatoswa kwenye kura za maoni. Hata hivyo, CCM kwa kujua hilo imeweka tarehe ya kuteuliwa kwa wagombea siku mbili kabla ya siku ya mwisho kwa Tume ya Uchaguzi kupokea majina rasmi.
You Are Here: Home - - Sumaye atajwa kumvaa Kikwete uchaguzi 2010
0 comments