IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo ametangaza Idara tatu za Kurugenzi zitakazosimamiwa na maaskofu wasaidizi wapya wa Jimbo hilo aliowaweka wakfu, huku yeye akibakiwa na idara nyeti za kusimamia mapadri, watawa na Mahakama ya Kanisa.
Sambamba na hilo kati ya maaskofu hao wawili, Salutaris Libena, amepewa idara inayohusu waandishi wa habari na mawasiliano yote ya Jimbo huku Askofu Eusebius Nzigilwa akipewa mkoba wa fedha.
Kadinali alitangaza utaratibu huo wa utendaji kazi juzi, katika viwanja vya Parokia ya Msimbazi kwenye ibada ya misa ya kuwaweka wakfu maaskofu hao wasaidizi walioteuliwa mapema mwaka huu na Baba Mtakatifu Benedict wa XIV, ili wachukue nafasi ya Askofu Method Kilaini aliyehamishiwa Jimbo la Bukoba.
Baada ya Pengo kugawa kazi za kichungaji kulingana na maeneo mawili ya upande wa kushoto na kulia wa Barabara ya Morogoro ukitokea Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph, alitangaza usimamizi wa idara za kurugenzi kwa kuanza na zitakazosimamiwa na maaskofu hao na kisha alitangaza kurugenzi zake mwenyewe.
“Mimi nitakuwa nasimamia Mapadri (akaweka kimya kidogo na kuwageukia waumini hali iliyosababisha watu kushangilia, kisha akaendelea) watawa (wa kike na wa kiume), Utoto Mtakatifu wa Yesu, Uwata, Wawata, Halmashauri ya Walei, Jimbo na Mahakama ya Kanisa,” alisema Pengo.
Alisema anachukua jukumu la kusimamia Idara hizo kwa kuwa yeye ni baba wa Jimbo hivyo anawafahamu vyema watoto wake ‘mapadri’ na pia yeye ni Hakimu Mkuu wa Kanisa (Jimbo), hivyo ni vema akasimamia Mahakama ya Kanisa katika eneo lake.
“Mgawanyo huu ni katika shughuli zote zinazohitaji huduma ya Uaskofu…nikisema ndoa ya mtu bado inaishi, hata Baba Mtakatifu naye ataniunga mkono kwamba bado inaishi hivyo mimi ni hakimu mkuu kwa eneo langu,” alisema Pengo na kushangiliwa.
Baadhi ya waumini waliozungumza na gazeti hili mara baada ya kumalizika kwa ibada hiyo iliyochukua zaidi ya saa tano, walisema mgawanyo huo umelenga kufanikisha utendaji kazi wa karibu zaidi kwa kila idara na kumsifu Pengo kwa uamuzi wake wa kubaki kuwasimamia mapadri kwa kuwa mzoefu na mwenye hekima nyingi.
“Unajua Kadinali anajua kuishi na vijana wake, hawa mapadri wetu wanahitaji uangalizi wa baba hasa kwa kuwa changamoto dhidi yao ni nyingi, wengine wanataka kukata tama labda, kama unavyojua maneno kuhusu tabia na mwenendo wao ni mengi mitaani, mengi ya uzushi lakini mengine yana ukweli, hivyo akibaki nao, itasaidia kuweka kanisa katika maadili mema,” alisema John Urio wa Parokia ya Tabata.
Naye Flora Enjalika wa Parokia ya Tegeta, alisema busara za Kadinali ndizo zimemwongoza kugawa idara hizo na anategemea maaskofu hao watamsaidia kufanya kazi nyingi za kichungaji hasa kuwalea mapadri katika mwito wao kuliko awali.
Idara nyingine za Nzigilwa ni kusimamia miito, elimu, haki na amani, afya, ardhi na Shirika la Misaada la Wakatoliki la Karitasi. Libena amekabidhiwa liturjia, vyama vya kitume, uchungaji, vijana, katekesi na katekumeni.
Viongozi waliyohudhuria ibada hiyo ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Jaji Mkuu, Augustino Ramadhan, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo aliyemwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, William Lukuvi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, John Magufuli na Askofu Mkuu wa KKKT, Dk Alex Malasusa.
You Are Here: Home - - Pengo apangua muundo wa uongozi Jimbo Kuu la Dar
0 comments