Rais Mstastaafu, Ali Hassan Mwnyi, ambaye anakumbukuka umhimu wa Azimio la Arusha. |
Amesema kulikuwa na sera nzuri ya Azimio hilo, lakini ili iweze kutekelezwa, ilihitaji viongozi wa makanisa na misikiti, kufinyanga watu wanaomcha Mungu ili kuitekeleza.
Mwinyi alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizindua benki ya Mkombozi iliyoanzishwa na Kanisa Katoliki nchini, ambapo pamoja na mambo mengine, alizungumzia baadhi ya watu wanaolilia Azimio la Arusha.
Alisema baadhi ya viongozi wanalilia Azimio hilo, baada ya kuona mambo yanavurugika, lakini ifahamike kuwa halikufutwa bali lilizimwa na baadhi ya mambo.
“Azimio la Arusha halikufutwa, wala lile la Zanzibar halikufuta la Arusha, lilizimwa na baadhi ya mambo ambayo hayakwenda vizuri,” alisema Mwinyi na kuongeza:
“Hakuna siasa nzuri na bora kwa Watanzania kama ya Ujamaa, ile ambayo ililetwa na marehemu Mwalimu Nyerere, lakini inaelekea kwamba nia hiyo ilitangulia uwezo wa Watanzania,” alisema Mwinyi.
Mwinyi alisema kwa mfano wakati ule kulikuwa na mashirika ya umma yapatayo 400, lakini yalikuwa magamba tu, ‘yamegunguliwa (yametafunwa)’ kama mchwa anavyotafuna mti wa msonobari, huku kwa nje ukibaki mzuri kumbe kwa ndani hauna kitu.
“Viongozi hao wamegungua mashirika hayo kama kunde inavyotafunwa na wadudu, nje nzima kumbe ndani gamba tupu … watu bado walikuwa hawajapatikana, ndiyo maana mashirika yaliuzwa baada ya kuonekana ni mzigo kwa Taifa,” alisema.
Alisema wengi walioendesha mashirika hayo hawakumwogopa Mungu na kwamba katika uongozi uliopo, ipo haja ya kuomba taasisi za dini kufinyanga vijana wanaomwogopa Mungu ndipo wapewe dhamana.
Kuhusu benki, alipongeza jitihada zilizofanywa na Kanisa kutokana na kwamba mtaji wake ulitokana na Watanzania na si wafadhili wa nje ya nchi na kuitaka Serikali kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani.
Alisema uanzishwaji wa benki hiyo, ni jambo muhimu kwa kuwa litasaidia jitihada za Serikali za kukuza uchumi.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kanisa Katoliki Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, alisema Kanisa halitajihusisha moja kwa moja na benki hiyo, ila waendeshaji wake watakuwa wataalamu ambao wataendesha kwa misingi ya Kanisa Katoliki.
Naye Mtendaji Mkuu wa Benki hiyo, Edwina Lupembe, alisema benki hiyo ilianza kutoa huduma Agosti 28 mwaka jana, ikiwa na mtaji wa Sh bilioni sita na hadi sasa imetoa mikopo ya Sh. milioni 637 na ina akiba ya zaidi ya Sh. bilioni mbili
0 comments