Makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa ambaye anadaiwa kugawa kadi za chama chake usiku nchini Uingereza. |
MAKAMU mwenyekiti wa CCM Bara, Pius Msekwa juzi alikaa hadi usiku wa manane katika mkutano wake na Watanzania waishio Uingereza akigawa kadi za chama hicho tawala.
Habari kutoka Uingereza zimelieleza gazeti hili kuwa katika mkutano huo Msekwa alikabidhi katiba ya CCM kwa tawi la CCM la jijini London, kadi kwa zaidi ya wanachama 70 na vifaa vingine kadhaa.
Habari zilizolifikia gazeti hili kutoka Uingereza zimeeleza kuwa Msekwa alikabidhi vifaa hivyo katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Warehouse mjini Reanding ulioanza saa 11:00 jioni ambao pia ulihudhuriwa na balozi wa Tanzania nchini humo, Mwanaidi Maajar.
Kwa mujibu wa habari hizo, Msekwa alishangazwa na jinsi Watanzania hao walio ughaibuni walivyoweza kuimudu salamu ya chama hicho ya ‘kidumu Chama Cha Mapinduzi,… Kidumu,… CCM mshikamano mnatoa’.
Katika hafla hiyo Msekwa aliinadi CCM kwa kueleza historia yake na kuwataka Watanzania hao wakienzi chama hicho kwa vitendo.
“Mkutano wetu na Msekwa ulianza saa 11:00 jioni na kumalizika usiku wa manane, alikabidhi kadi mpya za uanachama zaidi ya 70, katiba ya CCM na vifaa mbalimbali kwa ajili ya matawi mapya yaliyofunguliwa huku," chanzo cha habari kutoka Uingereza kilidokeza.
"Wakati akikabidhi vitu hivyo alikuwa na Balozi Maajar na kabla ya yote hayo alitoa historia yake na ya chama kisha akatuhimiza tukidumishe chama hicho, lakini alishangazwa sana na salamu ya wanaCCM wa huku ya ‘kidumu Chama Cha Mapinduzi... Kidumu. CCM mshikamano mnatoa" alieleza mtoaji huyo wa habari.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, miongoni mwa wanachama waliohudhuria ni kutoka katika matawi ya Manchester, Reading, Birmingham, na London.
Hata hivyo kwa ujumla wanaCCM wote wanaoishi Uingereza wanajulikana kama CCM tawi la London.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, John Chiligati alisema Msekwa alikwenda London kwa mwaliko wa wanaCCM wanaoishi Uingereza kwa ajili ya kusherehekea kutimiza miaka 33 ya chama hicho.
"Huu ndio wakati wenyewe wa maandalizi... kila chama kinahangaika kutafuta ushindi. Hakuna anayelala," alisema Chiligati juzi.
Aliongeza kusema: “CCM ina wanachama wengi nje ya nchi na hasa katika bara la Ulaya. Pia ina mashina na viongozi wake huko na hata hii safari ya Msekwa ni mwaliko maalumu kutoka kwa wanachama wetu wa Uingereza. Wamemwita kwa ajili ya kusherehekea CCM kutimiza miaka 33.â€
Awali baadhi ya vyanzo vyetu vilidai kuwa Msekwa alikwenda nchini humo kwa ajili ya kufanya kampeni juu ya uchaguzi mkuu wa Oktoba.
"Ukweli ni kuwa Watanzania wengi waishio huku, wamepanga kurudi nyumbani Tanzania kabla ya Oktoba ili kupiga kura kwa ajili ya kuchagua viongozi," kilisema chanzo chetu.
"Kutokana na sisi (Watanzania) kujuana mahali tulipo huku na pia viongozi wa CCM kujua hilo ndio maana wamewaita viongozi hao ili waweke mambo sawa."
Uamuzi huo wa CCM kufanya kampeni nje ya nchi umekuja huku bado sheria zikiwa haziruhusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupiga kura.
Hata hivyo, Chiligati alisema mchakato wa utaratibu wa jinsi Watanzania waishio nje ya nchi watakavyoshiriki kupiga kura wakiwa nje ya Tanzania upo katika hatua nzuri.
"Mchakato wa uwekaji utaratibu wa jinsi Watanzania waishio nje ya Tanzania kupiga kura wakiwa huko unakwenda vizuri japokuwa sina uhakika kama hili litafanyika uchaguzi huu wa Oktoba," alisema Chiligati.
Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Birmingham, Uingereza, Peter Gabagambi alithibitisha kufanyika kwa sherehe hizo pamoja na kutolewa kwa kadi mpya kwa ajili ya wanachama pamoja na kukabidhiwa kwa vifaa na katiba ya CCM kwenye matawi mapya.
Alipotakiwa kuzungumzia taarifa za awali kwamba moja ya mambo yaliyompeleka Msekwa Uingereza ni kampeni za uchaguzi mkuu, Gabagambi alijibu, "Haa haa, sio kweli, ni sherehe tu za CCM."
0 comments