Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe akizungumza na waandishi wa habari kanisani kwake jana kuhusu kuridhia kupitishwa kwa nyaya za umeme zenye msongo mkubwa mbele ya eneo la kanisa hilo. |
ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zachary Kakobe, amedai kuwa baadhi ya watendaji wa serikali, wana ajenda za siri za kuhujumu Ukristo na kwa hiyo, ameamua kubadili mbinu za mapambano.
Askofu Kakobe alitoa madai hayo jana siku moja baada ya serikali kuridhia hatua ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupitisha njia ya umeme mkubwa mbele ya kanisa lake na kusisitiza kuwa haitarudi nyuma katika hilo hasa kwa kuzingatia kuwa mradi huo ni kwa manufaa ya wengi.
Kwa zaidi ya miezi miwili sasa, kiongozi huyo wa kanisa na waumini wake, wamekuwa wakivutana na Tanesco kuhusu mpango wa kupitisha njia kubwa ya umeme ambayo wamekuwa wakidai kuwa utaathiri kituo chao cha televisheni wanachotarajia kukianzisha.
Hata hivyo malumbano hayo yalifikia tamati juzi baada ya mshauri ambaye serikali ilimtumia katika kupata vipimo sahihi na kuziridhisha pande zote katika malumbano hayo, kuthibitisha kuwa njia hiyo ya umeme, haitakuwa na athari kwa watu wala vifaa vya kanisa.
Lakini akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana, Askofu Kakobe alisema amekubali njia hiyo ipitishwe lakini alisistitiza kuwa uamuzi uliofanywa na serikali si halali.
"Sasa hivi hatuna kipingamizi chochote, waje waendelee na kazi yao," alisema Kakobe ambaye Desemba mwaka jana alitangaza eneo hilo kuwa ni la hatari kwa wafanyakazi wa Tanesco na tangu wakati huo likawa linalindwa na waumini wa kanisa wake waliovalia fulana za njano zenye maandishi "Tanesco mwogopeni Mungu."
Pamoja na kuridhia Tanesco waendelee na mradi huo, Askofu Kakobe alisisitiza kwamba kwenye uamuzi huo haki ilifinyangwa na uamuzi wa kibabe uliochochewa na mambo ya udini, lakini akasema sasa amebadili mbinu na mikakati ya kukabiliana nao.
Akionekana kuzungumza kwa utaratibu na uangalifu mkubwa, alitaja miongoni mwa mbinu zake za sasa kuwa ni kuwasiliana na makanisa mengine ya Kikristo nchini kutaka wajadili hujuma dhidi yao na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Alidai kuwa hujuma hizo ni pamoja na baadhi ya waumini wa kanisa lake kuanza kubaguliwa kwenye maeneo ya kazi, jambo ambalo alilielezea kuwa "ni la hatari na linaotesha mbegu ya ubaguzi wa udini, kinyume na Katiba ya nchi."
"Hili siyo siri limefanyika, muumini wetu aliyekuwa anafanya kazi Wizara ya Nishati aliitwa na kuulizwa anasali wapi na ilipobainika ni muumini wa kanisa hili kwa muda mfupi tu, akakabidhiwa barua ya uhamisho. Huu ni ubaguzi," alidai.
Kakobe alidai kwamba kuna baadhi ya makanisa ya Kikristo yaliyowasiliana naye tangu awali na kumtahadharisha asiendelee kuvutana na serikali kwa maelezo kwamba kuna njama za udini dhidi ya Ukristo.
Alidai kuwa mvutano huo ulianza tangu ulipoibuka mvutano juu ya Mahakama ya Kadhi na suala la ama Tanzania kujiunda au kutojiunga na Jumuia ya Kimataifa ya Kiislamu (OIC).
Juzi, Ngeleja alitoa tamko la serikali akisema kwamba pingamizi la kanisa hilo halina msingi kwa sababu njia hiyo ya umeme inapita umbali wa mita 5.6 kutoka kwenye kanisa hilo umbali ambao ni zaidi ya kiwango cha kimataifa cha mita tatu kwa mradi wa kilovoti 132.
Waumini wa kanisa hilo walikuwa wakilalamika kuwa njia hiyo ya umeme huo itapita umbali wa mita 2.8 mbele ya kanisa hilo hivyo wakadai kwamba kitaalamu wataathirika kiafya pamoja na mitambo ya elektroniki inayotumika kanisani.
Askofu Kakobe alikuwa akitaka njia hiyo ipite ipite umbali wa mita zisizopungua 7.5 akidai kwamba ni umbali unaokubalika kitaalamu kwa kilovoti 134, ili mawimbi yake yasiathiri waumini pamoja na mitambo yao ya elektroniki.
Kuhusu namna ya kujikinga na madhara ambayo yanaweza kutokea kutokaa na kuridhia umeme huo upite mbele ya kanisa lake, alisema anawasiliana na wataalamu ili kujua tahadhari za kuchukua.
0 comments