Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Ikulu lawamani vita ya ufisadi

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter YADAIWA KUIKWAMISHA TAKUKURU KUSHUGHULIKIA WALA RUSHWA

Felix Mwagara

RIPOTI ya Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mpango wa Kutathmini Utawala Bora nchini Tanzania (APRM), imebainisha kuwa kitendo cha kuiweka Taasisi ya Kupambana na Rushwa (Takukuru) chini ya ofisi ya Rais Ikulu, kinasababisha utendaji wake kuwa mbovu.

Baraza hilo limesema hiyo imedhihirika katika utafiti wake huo ulifanyika kati ya mwaka 2007 na 2009 kwa kuwashirikisha wananchi na watalaamu mbalimbali.

Kwa mujibu wa baraza hilo, katika utafiti huo unaojulikana kama 'Demokrasia na Utawala Bora', wenye mada tisa, wananchi na wataalam walitoa maoni yao kuhusu na demokrasia na utawala wa kisiasa.

Akisoma ripoti ya utafiti huo jana katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Dk Mohamed Bakari wa Idara ya Siasa na Demokrasia katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kitendo cha kuiweka Takukuru chini ya ofisi ya Rais kinasababisha udhaifu katika utendaji wa taasisi hiyo.

Wataalam na wachambuzi wa masuala ya utawala bora, wanadhani kitendo cha Takukuru kuwa chini ya Ofisi ya Rais Ikulu, kunaifanya taasisi hiyo ishindwe kushughulikia rushwa kubwa; hasa za viongozi wa juu wa serikali na waliostaafu kwa sababu za mgongano wa kimaslahi.

Sababu nyingine ambayo imekuwa ikitolewa kwa chombo hicho kuwa chini ya Ikulu ni kukosa uhuru wa kuchukua hatua dhidi ya baadhi ya watuhumiwa.

Hata hivyo, tayari taasisi hiyo imeshawapeleka mahakamani vigogo kadhaa waliokuwa serikalini kujibu mashtaki ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na mali za umma.

Vilevile utafiti huo ulibaini kwamba, kitendo cha Takukuru kutakiwa kupata idhini ya Mkurugenzi wa Mashitaka ili ifungue kesi kubwa za rushwa, kunasababisha utendaji wa usiwe imara.

Dk Bakari pia alibainisha kuwa hatua ya kuvizuia vyombo vya habari na asasi za kiraia kuripoti taarifa za kesi zilizoko chini ya uchunguzi wa Takukuru, kunakwamisha misingi ya utawala bora.

Alisema mambo hayo na mengine, yanasababisha kuongezeka kwa kiwango cha rushwa nchini, huku Takukuru ikishitumiwa kwa kujihusisha zaidi na kesi ndogo na kukwepa kesi kubwa za vigogo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo ufanisi wa Takukuru hauridhishi kabisa.

Kuhusu hali ya rushwa nchini, Dk Bakari alisema katika kipindi cha kati ya mwaka 2003 na 2007 kulikuwa na tuhuma 22,184 za rushwa zilizofikishwa Takukuru.

Alisema hata hivyo, ni majalada ya tuhuma 5,240 tu ndiyo na kwamba, ni kesi 427 tu zilizokuwa zimefikishwa mahakamani katika kipindi hicho. Kwa mujibu wa Dk Bakari ni kesi 74, tu ambazo washitakiwa wake walitiwa hatiani.

Alisema kwa maoni ya wananchi na wataalam, huo ni udhaifu mkubwa ulioonyeshwa na Takukuru katika utendaji wake.

Kuhusu mgawanyo madaraka kati ya Serikali na Bunge, Dk Bakari alisema una utata na mapungufu hasa kwa kitendo cha mawaziri na manaibu wao kutoka miongoni mwa wabunge, jambo ambalo alisema linakwamisha uwajibikaji wa Baraza la Mawaziri kwa Bunge.

Taarifa hiyo inasema, licha ya kukiukwa kwa maadili ya viongozi, Tume ya Maadili (Ethics Secretariat) haijaonyesha uwajibikaji wa kiongozi wowote wa umma kwa kukiuka maadili.

Kuhusu uwajibikaji na ufanisi wa watendaji wa sekta ya umma, maoni ya wataalamu yameonyesha kuwa uwajibikaji ni wa kiasi kidogo kwa asilimia 83.4 kati ya wataalamu 102 waliohojiwa, huku asilimia 16.6 ikitoa maoni kuwa ufanisi ni wa juu.

Kwa upande wa raia wa kawaida 2,538 waliohojiwa kuhusiana na uwajibikaji na ufanisi wa watendaji wa sekta ya umma, 1,862 sawa na asilimia 72.4 hawakuridhishwa na ufanisi wa watendaji hao, huku 676, sawa na asilimia 26.3 walilidhishwa.

Kuhusu maoni ya wataalamu juu ya kiwango cha uhuru na haki katika ushindani wa kisiasa, maoni ya raia wa kawaida yalionyesha kuwa asilimia 71.9 ya chaguzi zinazofanywa zinakuwa huru na haki na asilimia 18.6 haziwi huru na haki, huku asilimia 10.3 ya wataalamu wakiwa hawajui.

Maoni ya raia juu ya mgawanyo wa madaraka kikatiba na kisheria yalionyesha kuwa mgawanyo unaridhisha kiasi kwani asilimia 62.6 ya raia walisema sheria zinatosha, 37.2 walisema hazitoshi na0.2 hawajui.

Kwa upande wa wataalamu, asilimia 45.1 kati yao walisema sheria zinatosha kabisa, 30.4 walisema zinatosha kiasi na 24.5 wakitoa maoni kwa sheria hazitoshi.

Kuhusu maoni yalionyesha zina uhuru, lakini hazina ufanisi kutokana na rushwa na matatizo mengine kama upungufu wa watendaji na vitendea kazi wa mahakama na raia waliohojiwa asilimia 82.7 walisema kuwa mahakama ziko huru na asilimia 17.3 walisema kuwa mahakama hazina uhuru, upande wa maoni ya wataalamu, asilimia 85.3 ya waliohojiwa walisema ziko huru na 14.7 wakisema zina uhuru kidogo.

Maoni kuhusu uhuru wa Bunge asilimia 88 ya raia wa kawaida walisema Bunge lina uhuru wa kufanya maamuzi na 17.3 walisema inategemea kwa upande wa wataalamu asilimia 89.2 walisema kuwa Bunge ni huru na asilimia 10.8 wakidai Bunge lina uhuru kidogo.

Utatuzi wa migogoro baina ya mihimili mitatu ya dola utafiti umependekeza kuwa kuna haja ya kuwa na chombo maalumu ambacho kinaweza kutatua migogoro baina ya mihimili mitatu ya dola.

Pia umependekeza mahakama maalum ya kikatiba kama ilivyobainishwa na ibara ya 125 ya Katiba ipewe mamlaka ya kutatua migogoro ya aina hiyo mbali na mamlaka iliyopewa chini ya ibara ya 126.

Hata hivyo, ripoti imeonyesha kuwapo tatizo ambapo Katiba iliyopo haikidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi. Vyama vya upinzani vinadai kwamba mfumo wa vyama vingi Tanzania, kimsingi unaendeshwa chini ya katiba ya chama kimoja iliyofanyiwa mabadiliko machache ambayo hayatoshelezi.

Ripoti pia imebaini kutokuwepo kwa uwajibikaji na uwazi ndani ya vyama na usimamizi na udhibiti mzuri wa fedha wakati wafanyabiashara wakubwa wanachangia fedha nyingi kwa chama tawala CCM, kuna madai kwamba, wafanyabiashara wanaodhaniwa kuunga mkono vyama vya upinzani wanaandamwa na serikali.
Tags:

0 comments

Post a Comment